Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Riziki Shahari Mngwali

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kushukuru kuwa nimepata nafasi ya kuchangia kwa kuzungumza kuhusu hoja hii jana tarehe 2 Novemba, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la kuwa na mpango wenye malengo mapana yasiyopimika limejitokeza tena katika Mpango wa 2017/2018 kama ilivyokuwa kwa mpango wa 2016/2017. Inasikitisha sana kuona kuwa Serikali inadhani inajua kila kitu na kwamba inachokisema na inachoandaa ni sahihi. Tunapochangia hoja za Serikali, nia huwa ni kuboresha hoja husika kwa maslahi ya nchi yetu na si vinginevyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tatizo la kukosekana utengamano (integration) wa Wizara mbalimbali linaonekana tena katika mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2017/2018, kama ulivyokuwa kwa ule uliotangulia. Hili ni tatizo kubwa kwani ndicho chanzo cha kuwa na mipango isiyotekelezeka na bajeti isiyowezeshwa. Vipaumbele vinakuwa vingi mno kutekelezeka katika mwaka mmoja na hata kwa miaka mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu Mpango unarudia kusema kuwa miongoni mwa misingi inayoisimamia na kuendelea kuidumisha ni amani, usalama, utulivu na utengamano wa ndani wakati ukweli ni kuwa yote hayo hayapo. Serikali ya Awamu ya Tano inatumia mabavu na vitisho kukandamiza mfumo wa Vyama Vingi na demokrasia iliyojengeka nchini kwa miongo miwili sasa. Vyama vya Upinzani viko katika mazingira magumu sana na mara nyingi inatokea misuguano isiyo na lazima na vyombo vya dola.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kuwa Serikali haioneshi kuwa na utashi wa kujenga utengamano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Tatizo la kuvurugwa kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kesi ya Mashehe wa Zanzibar walioko mahabusu ya Tanzania Bara ni vielelezo tosha vya hali hiyo. Kilichojitokeza kwa suala la Mashehe ni kuwa Tanzania Bara inatumika kama Guantanamo ya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kiongozi Mwandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alisikika akisema hadharani kuwa wataoleta fujo Zanzibar watapelekwa bara kama wenzao akina Farid waka…
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali kama hii, huwezi kusema nchi ina amani, amani ni neno pana na halina maana ya kutokuwepo vita tu. (Peace is not absence of war) mifumo ya kuleta amani na utulivu inavunjwa na kuharibiwa na Serikali zote mbili zilizo madarakani. Naamini Wazanzibari wengi hawafurahishwi na hali hii, kinachotisha zaidi wamekaa kimya. Serikali inajiaminisha kuwa ukimya huu unaashiria amani, mimi siamini hivyo kwa sababu hiyo. Naishauri Serikali kujenga amani ya kweli nchini ili kujenga mazingira mazuri (wezeshi) kwa utekelezaji wa masuala muhimu mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini ukiwemo Mpango wa Maendeleo unaopendekezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi wamezungumzia suala la mdororo wa uchumi, na mimi naunga mkono. Nashauri Serikali isijivunie takuwimu za kupanda uchumi bila ya kuangalia ni vipi takwimu hizo zinajionesha katika maisha ya wananchi. Ni lazima mabadiliko au hali ya uchumi mkubwa (Macro-economy) ihusiane na uchumi mdogo (micro-economy) ambao unagusa hali ya maisha ya mwananchi mmoja mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alilizungumzia suala hilo wakati alipokutana na watendaji wa Benki Kuu, kwa kweli ni jambo lenye mantiki. Haiwezekani Serikali ijivunie kuimarika hali ya uchumi wa nchi wakati hali ya maisha ya wananchi walio wengi inadidimia au haiendani na hali hiyo ya nchi/Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, namsihi Mheshimiwa Waziri husika na Serikali kwa ujumla kuzingatia mapendekezo mbalimbali yanayotolewa na Waheshimiwa Wabunge ambayo kama nilivyosema awali yanatolewa kwa nia njema na kwa manufaa ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, siungi mkono hoja na badala yake namshauri Waziri Mpango, aisome kwa umakini taarifa ya maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.