Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Risala Said Kabongo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RISALA S. KABONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2017/2018 ni uhuishwaji wa viwanda nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda haviwezi kuwa endelevu kama hakutakuwa na malighafi ambazo kimsingi zinatokana na kilimo. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba bila kuwa na mapinduzi ya kilimo ndoto ya Tanzania ya viwanda haitafanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu kilimo chetu bado ni duni sana kuweza kuzalisha malighafi za kulisha viwanda hivyo vinavyokusudiwa. Hivi karibuni nimetembelea Mkoa wa Songwe, wakulima wanapata shida sana kutokana na ukosefu wa pembejeo za kilimo na zile chache zinazotolewa kwa mfumo wa vocha na mawakala zinakuwa za urasimu mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali kwa mapendekezo ya Mpango huu wa 2017/2018 iweke bajeti ya kufanya tathmini ya idadi ya wakulima ili pembejeo zinazotolewa ziendane na idadi ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, masoko ya mazao ya wakulima hayaeleweki, naomba Waziri atuambie kwa mpango huu wa 2017/2018 Serikali imejipangaje kufungua masoko ya wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika. Kumekuwa na changamoto nyingi sana kwenye suala la afya nchini, kwa mfano Hospitali ya Wilaya ya Vwawa inayotegemewa na Mkoa mzima wa Songwe ina upungufu mkubwa wa madawa, Madaktari na vifaa tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilifanya ziara kuangalia huduma ya mama na mtoto, wanawake 14,695, sawa na wanawake 15 – 20 kwa siku wanajifungulia hapo. Wagonjwa 150 – 200 wanahudumiwa kama outpatient kila siku katika hospitali ya Wilaya. Huku idadi ya Madaktari wakiwa watatu na uhitaji ni Madaktari 23. Sambamba na watumishi 507 na uhitaji ni watumishi 1,112. Watoto wa umri wa miaka 0 – 28 wanafariki kwa siku na kupelekea idadi yao kuwa 180 kwa takwimu za 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Waziri anahitimisha aniambie kwa mpango huu wa 2017/2018 wana mkakati gani wa kupandisha hadhi hospitali ya Wilaya ya Vwawa kuwa hospitali ya mkoa ili kuwa na bajeti ya kutosha kukabiliana na changamoto katika hospitali hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako majengo yaliyoachwa na wakandarasi waliojenga barabara ya Sumbawanga – Tunduma ambayo yapo kilomita tatu kutoka Tunduma Mjini eneo la Chipaka na Serikali ilitoa commitment ya kufanya majengo yale kuwa hospitali ya Wilaya naomba commitment hiyo iwekwe kwenye mpango ili kusaidia kupunguza tatizo la huduma za afya, ukizingatia kwamba Tunduma ni mpakani na watu wanaohitaji huduma ya afya ni wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la Black market. Soko hili lipo ndani ya mpaka wa Zambia na wafanyabiashara wengi, zaidi ya 1000, wa upande wa Tanzania wanafanya biashara zao katika mpaka huo; hii inasababisha ukosefu wa mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kufahamu je, katika mpango huu wa 2017/2018, Serikali imeweka utaratibu gani wa kuwarudisha wafanyakazi katika eneo la Tanzania ili kuongeza mapato katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma?