Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, utangulizi; awali ya yote napenda kunukuu katika kitabu Kitakatifu cha Biblia, Mithali, Sura ya 11, mstari wa 14; mstari huo unasema: “Pasipo mashauri Taifa hupotea, bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.”
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya afya nchini; ni dhahiri hali ya uchumi wa nchi unayumba. Kuyumba huku kwa uchumi ni hatari sana katika sekta nzima ya afya. Kumekuwepo na malalamiko makubwa katika sekta ya afya kwa muda mrefu sasa na hayajatatuliwa. Takwimu zinaonesha huduma za afya na ustawi wa jamii zilikua kwa asilimia 8.1 mwaka 2014, lakini kwa mwaka 2015 ni asilimia 4.7 pekee. Hii ina maana kwamba, utoaji huduma za afya na ustawi wa jamii umepungua kwa asilimia 3.4. Hivi karibuni nilifanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Musoma, Mara ni kilio kwa kweli! Vitanda havitoshi, madawa hakuna, kiasi kwamba wanaokwenda hospitali wakiwa wanaugua malaria wanatoka na typhoid au kifua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kauli tata sana na za aibu kwenye sekta hii ya afya. Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekiri kuwepo kwa ukosefu wa dawa nchini, ndani ya Bunge hili, Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu wake wanasema kuna dawa za kutosha katika Bohari ya Dawa Nchini (MSD). Wananchi nao wanalalamika kwa kukosa dawa mahospitalini. Huduma za tiba zinadorora kwa kuwa hakuna vifaatiba katika mahospitali mengi. Pamba na gloves zimeadimika, wagonjwa wanalazimika kwenda na pamba na gloves; akinamama na watoto wamekuwa wahanga wakubwa katika hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka kuna siku hapa Mheshimiwa Mbunge mmoja aliuliza swali kuhusu Mpango wa Serikali kupambana na ugonjwa wa fibroid kwa wanawake. Ni ajabu sana Mheshimiwa Naibu Waziri alijibu kwa kubeza kuwa, fibroid siyo ugonjwa tishio kwa kiasi hicho. Lakini sisi akinamama tunajua ni kwa namna gani akinamama wenzetu wanasumbuliwa na ugonjwa huo. Fibroid kwa akinamama ni tishio na ni tishio kubwa sana maana sasa linawakumba mpaka mabinti wadogo. Hili suala siyo la kuchukulia kimzaha tu! Tunapoteza nguvukazi ya Taifa ha hatuoni mpango madhubuti wa Serikali katika kukabiliana na tatizo hili kama walivyofanya kwa ugonjwa wa malaria kwa akinamama wajawazito.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni masikitiko yangu kuona Serikali ikinunua ndege ambazo zinawanufaisha tabaka la watu wachache tu huku hakuna uwekezaji wa kutosha katika sekta ya afya ambayo inamgusa kila mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia kusema, pasipo mashauri, Tanzania itapotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la utawala bora; hakuna maendeleo kama hakuna utawala bora. Ndani ya Serikali hii, washauri mbalimbali na watalaam wamekuwa wazito katika kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Rais katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo. Tatizo kubwa linaloitafuna Serikali hii ya Awamu ya Tano ni kutokuzingatia misingi ya utawala bora, kufuata sheria, Kanuni pamoja na kuruhusu mawazo huru kwa kila Mtanzania. Utawala bora ni pamoja na kukaribisha mawazo kutoka katika maeneo mbalimbali bila kujali itikadi za vyama. Ni pamoja na kuwa na kifua cha kupokea changamoto ikiwa ni pamoja na kukosoa na kukosolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni masikitiko yangu pale ninapoona Vyama vya Upinzani ambavyo ni jicho la pili la Serikali, ni jicho linaloweza kuona pale Serikali isipoweza kuona, ni mdomo wa kuwasemea wadau mbalimbali ikiwemo ninyi Wabunge wa Chama Tawala na Mawaziri pale ambapo mna mambo ambayo hamuwezi kuyasema waziwazi kwa Serikali kwa sababu ya hofu za nafasi au maslahi binafsi. Upinzani ni msaada kwa kuwa, ndiyo Serikali mbadala (Alternative Government). Tunapoona Mawaziri au Wabunge wakichukia Upinzani au kuwa na mawazo potofu kuwa, upinzani ni kupinga inashangaza sana!
Ni vema Waheshimiwa Wabunge wakapewa elimu ili kujua upinzani ni kitu gani ili linapokuja suala la kujadili mambo ya msingi ya kimaendeleo kwa faida ya nchi yetu waweze kuwa-change kwa kupokea, kuyachambua yale yanayofaa hasa katika kujadili Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi ya maendeleo inakwama kutokana na sanaa katika mambo ya msingi. Mfano, Mkurugenzi anatumbuliwa tena kwa barua kutoka Ikulu halafu anapelekwa nje ya nchi kuwa Balozi; tunakwenda wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi imekuwa na msururu wa kodi kwa wafanyabiashara wazawa tena wale wenye mitaji midogo. Maliasili kuna kilio kikubwa cha kodi hizo mfano, kodi ya kulipia magari, leseni, mageti na kadhalika. Hii ikiwa ni jumla ya kodi 32 katika biashara ya sekta ya utalii. Yaani inaweza kuchukuwa takribani miezi miwili mpaka mitatu katika kulipia kodi. Hii ni aibu kubwa kwa Serikali, ambayo inashindwa kuleta tija katika kuwasaidia watu wake ambao tayari wengi wao wanapambana na ukuta mkubwa wa maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, kuna baadhi ya viongozi wanabeza na kusema, eti Watanzania ni wavivu! Kwa wingi huu wa kodi ambao unawafanya wafanyabiashara kushindwa kuendelea kumudu biashara zao, Serikali haioni kuwa tunazalisha wimbi la majambazi na vibaka tena kwa bidii?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni rai yangu kuwa, Serikali iangalie upya namna ya kukusanya kodi. Iangalie ni aina gani za biashara za kukusanya kodi na kwa kiasi gani ili kupunguza mzigo mkubwa uliowaelemea wafanyabiashara wadogo au wachuuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri Watendaji wa Serikali na wanasiasa wakaheshimu kazi kubwa inayofanywa na upinzani. Mheshimiwa Rais aheshimu Sheria na Katiba ya nchi ambayo kimsingi inawaruhusu wanasiasa kufanya mikutano yao kwa uhuru na amani. Rais awe ni mfano wa kusimamia Sheria na Katiba ya nchi. Kila Kiongozi ataweza kutekeleza shughuli za maendeleo na kuleta tija katika Taifa endapo kuna uhuru na haki katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho; niombe Waziri wa Fedha aweze kupitia tena vipaumbele hivi vya mpango na kuangalia ni namna gani sekta ya utalii inaweza kuchangia zaidi. Kwa kuwa, awali sekta hii ndiyo ilikuwa inachangia pato kubwa la Taifa takirbani asilimia 27.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.