Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hizi taarifa zilizowasilishwa mbele yetu, taarifa ya Kamati ya PAC na LAAC. Mchango wangu wa kwanza utajielekeza katika suala zima la Deni la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Juni, 2016 Deni la Taifa limeongezeka kwa asilimia 9.76 maana yake linakimbilia shilingi trilioni 40. Madeni haya kwa mujibu wa taarifa ya CAG ameeleza kabisa hakuna mkakati wa namna gani yanaweza kwenda kulipika. Kulikuwa kuna rasimu ya mkakati huu ya mwaka 2002, ikatengenezwa rasimu nyingine ya mwaka 2004, ikatengenezwa nyingine ya 2014 lakini zote ni rasimu bado haijakamilika kuwa mkakati wa kuona namna tuta-control Deni la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipoangalia, itafikia mahali fedha zote za makusanyo ya nchi hii zinaenda kulipa madeni. Kama ambavyo ilivyo leo kila kinachokusanywa karibu shilingi bilioni 900 inaenda kulipa madeni. Kwa hiyo, ni lazima Serikali ifike mahali iandee mkakati. Ripoti ya CAG imesema kabisa hii rasimu ambayo ipo tena imeandaliwa kizamani haiendani na hali halisi ya uchumi wa nchi. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaona umuhimu wa kuwa na mkakati huu ambao utaendana na hali halisi ya uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Tuna Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo kwa kiwango kikubwa fedha zake zinakopwa na zinaenda kuwekezwa katika miradi mikubwa. Hatukatai kufanyia shughuli hizo, lakini unapoenda kukopa halafu hurejeshi inakuwa ni tatizo. Mfuko mmojawapo tu kwa mujibu wa taarifa ya CAG ni PSPF una hali mbaya ambapo unakaribia kufilisika kabisa kwa sababu Serikali hairejeshi fedha ilizozikopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima ifike mahali muache kabisa kukopa hizi fedha za wanachama. Ni fedha za wanachama wanaweka kule wakijua wanajiwekea akiba lakini Serikali mnaenda kuzichukua na ku-invest kwenye miradi mikubwa ambayo tunaona kabisa siyo rahisi muweze kurudisha kwa sababu mmejaa madeni, mnadaiwa ndani na nje, mnakopa tena kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, mnadaiwa kila kona, mwisho wa siku mtaenda kuua hii akiba ya wafanyakazi ambao wanatarajia waipate siku wakistaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaongelea sana suala la kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, tumesema sana kwenye Bunge la Kumi. Leo mnajiita wazee wa hapa kazi tu, wazee wa kubana matumizi, si ndivyo mnavyojiita? Kama kweli mnataka kubana matumizi ni lazima muangalie suala la kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iko takribani tano au sita yote ina Wakurugenzi, ofisi, inaendeshwa kwa gharama na kwa fedha za wanachama. Kama mnasema mnabana matumizi muende muunganishe hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwepo na ama mifuko miwili au mitatu ili hicho mnachokiita cha kubana matumizi mkifanye kwa vitendo siyo mnatuambia tu halafu hakuna mnachokifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya mwisho nitajielekeza katika Serikali za Mitaa. Katika Awamu hii ya Tano mnaenda kuua kabisa Serikali za Mitaa. Mnaenda kuzimaliza wakati Serikali za Mitaa zipo kwa mjibu wa Katiba ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uteuzi tu mliofanya, Mheshimiwa Rais alifanya uteuzi wa hawa ma-DC, ma-DED, ma-DAS, kwa kweli ni watu ambao hawajapitia kwenye mifumo ya local government, wengine wametolewa mnakojua, wamepewa nafasi ambazo hawana experience hata nukta moja. Hivi wanaendaje kufanya kazi? Ma-DED wengine hawajui hata vote ni nini, anauliza vote ni nini? Wanauliza hawajui. Hivi mnategemea kutakuwa na ufanisi? Ndiyo maana tunawaambia mnaenda kuua Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali miaka yote imeonesha suala la Serikali Kuu kutokupeleka fedha za maendeleo katika Halmashauri za Wilaya. Hivi tunavyoongea leo, fedha zilizoenda katika local government ni fedha za mishahara tu. Mfano mzuri ni Halmashauri yangu ya Karatu. Fedha kidogo tu iliyoenda ni ya barabara shilingi milioni 50 lakini hakuna fedha za miradi ya maendeleo zilizoenda yaani mpaka leo tunaingia robo ya pili ya bajeti ya Serikali fedha hazijaenda katika Serikali za Mitaa. Mnatarajia nini si mnaenda kuziua Serikali za Mitaa.