Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Issa Ali Abbas Mangungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi kupata nafasi ya kuchangia taarifa hizi za Kamati mbili. Lakini, maji na chai peke yake havitoshi Wajumbe wa Kamati hii tunataka oversight ili tukaikague Serikali vizuri hasa Serikali za Mitaa. Lakini maji peke yake na hivi vitabu mama yangu Rwamlaza amesema pale vinatuzidi umri…
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo nitalifafanua mbele, lakini ningependa nianze kwa kushukuru kunipa fursa hii na mimi kuweza kuchangia. Na mimi moja kwa moja wenzangu wengi wamezungumza mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa. Wenzangu wengi wamezungumza kwa masikitiko makubwa jinsi gani Serikali yetu inavyoweza kuchangia kuzorotesha maendeleo katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hayo kwa sababu wengi wamezungumza, Serikali imekuwa ikichelewa sana kupeleka fedha za maendeleo katika Halmashauri hizi, lakini tunapouliza maofisa kutoka Hazina wanakuwa hawana maelezo na sababu za msingi. Kwa hiyo, ningeomba Waziri wa Fedha atujibu na atueleze tatizo ni la kibajeti au kuna uzembe na hao wazembe wanachukuliwa hatua gani kwa sababu watendaji wetu huko chini wanaumia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Halmashauri hasa za pembezoni, mfano Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kwa kipindi kirefu haikupelekewa fedha kabisa za maendeleo. Lakini kama walivyosema watangulizi wangu waliozungumza hapa, maagizo yanatoka, tujenge maabara, tufanye shughuli mbalimbali, mwenge na mambo mengine; kwa hiyo, Afisa Masuuli inabidi achambuechambue vifungu kuweza kukamilisha yale ambayo yameagizwa. Kama hizi fedha haziwezi kwenda kwa wakati ni kweli kabisa na usahihi tunaziua hizi Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini lengo la Serikali ni jema, inawezekana katikati hapa kuna vitu ambavyo vinasababisha hizi fedha zisiende. Kwa hiyo, Serikali iwe makini kupeleka hizi fedha za maendeleo kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile suala la hizi Kamati, tumeomba muda mrefu kwenda oversight ili tuweze kukagua, kwa sababu tunachoandikiwa kwenye vitabu sicho kile ambacho kiko katika site. Kwa hiyo, tumeambiwa kibali hakijatoka fungu halijaingia. Lakini kama mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Mheshimiwa Rais alisema tumsaidie kazi ili aweze kupambana na ufisadi katika nchi hii. Leo tunawekwa katika chumba kimoja tupewe maji au chai tunamsaidiaje kazi tukiwa ndani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Serikali ione haja ya kuziongezea bajeti hizi kamati ili twende kufanya oversight kukagua miradi ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nirudi moja kwa moja kwa Mkoa wangu wa Dar es Salaam, haswa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Kwa sisi watu wa Dar es Salaam Halmashauri ya Jiji kwetu ni tatizo. Na ningeomba Waziri uangalie muundo wa Jiji kama ikiwezekana basi tuvunje lile jiji kwa sababu sasa hivi tuna Halmashauri tano za Manispaa za Jiji la Dar es Salaam. Kwa sababu katika kitabu hiki cha LAAC ukurasa wa 28…
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilichokuwa naeleza East Africa Meat Company Limited, imezungumzwa hapa tatizo lake. Tumegawanya rasilimali katika hizi Halmashauri, lakini hili deni au hizi fedha ambazo Halmashauri zote hizi zilichangia kwenda Jiji hatujagawana wala hatujaambiwa na Serikali kwamba hizi fedha ziko wapi? Halmashauri ya Temeke, Ilala, Kinondoni zilitoa fedha kuchangia katika mradi huu, na ni pesa nyingi sana billions of money.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mpaka leo Jiji halijaelezwa kwamba hizi fedha ziko wapi, Halmashauri hizi zitafaidika na nini. Leo kwa Jiji kazi iliyobaki kwake ni sera, lakini sera iliyokuwepo pale kwa wengi wa Dar es Salaam tunaona ni kuongeza parking wasizozianda. Jiji pale kazi yao kubwa ni kukamata bodaboda kuwapa majembe na kampuni zingine hakuna kazi zinazofanywa na Jiji, zinaingilia mpaka maeneo ya Halmashauri zetu, ndio maana tunasema Jiji sasa hivi halina kazi. Lazima tuseme ukweli, tusifichane, jiji bora livunjwe ili Halmashauri ili zipate uwezo na Serikali ipunguze mzigo mkubwa wa kulilea Jiji ili Halmashauri mpya na zilizokuwepo za zamani. Huo ndio ushauri wangu kwa Serikali na ninaamini mtazingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie hii East African Meat kuna ardhi pale ambayo ipo. Ardhi ile sasa hivi imegeuka kichaka, haijaendelezwa bora Halmashauri ya Ilala ipewe lile eneo waweze kuendeleza au kujenga shule na shughuli zingine za maendeleo kuliko vile lilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba vilevile nizungumzie suala la watumishi katika maeneo ya pembezoni. Hivi leo kuna haja gani eneo kama la Kariakoo kuwa na Afisa Kilimo au Afisa Mifugo, au Upanga? Mfano kwenye Halmashauri yangu ya Temeke pale Afisa Kilimo hakuwa na bajeti amekaa mwaka mzima analipwa mshahara wa Serikali. Lakini Kalambo kule tuliona Afisa Mipango Miji ndio ana kaimu kuwa Afisa Kilimo, watu wako Dar es Salaam kule hawafanyi kazi, wanalipwa mishahara, maeneo ya pembezoni watu wa kufanya kazi hizi hawapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasikia Wabunge wenzetu wa pembezoni wanalalamika kuwa Maafisa Ugani hawapo, lakini Dar es Salaam wapo. Sio hilo tu, Wabunge wengi hapa wamezungumzia na wamelalamika suala la kukaimu watu ukuu wa idara. Lakini katika Halmashauri zetu za Dar es Salaam unaweza ukakuta idara moja ina maofisa zaidi ya sita, hawana shughuli ya kufanya zaidi ya kusubiri semina. Kwa nini wanakaa Dar es Salaam kule, waende maeneo mengine wakalitumikie hili Taifa! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo wa rasilimaliwatu lazima uzingatiwe. Wataalam waende kwenye maeneo yenye mahitaji ili waweze kutusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba sana suala la mradi wa mabasi yaendayo kasi ambayo unasimamiwa na DART, mara nyingi nikipita pale TAZARA huwa nashangaa kidogo, ule mchoro unavyoonesha kwa sababu DART Phase II, utagusa eneo la Gongo la Mboto kupita TAZARA mpaka Kariakoo. Lakini ule mchoro wa interchange pale hauoneshi kama zimetengwa tayari, eneo la barabara za mwendo kasi. Kwa hiyo tunategemea mwakakni tukianza kutekeleza huu mradi, tuvunje tena. Kwa hiyo, naomba Serikali itupe majibu je, pale wana mpango gani au huu mradi tena umeshakufa umeishia pale ulipo?.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa eneo la Mbagala, Mheshimiwa Mwijage anasema kila siku hapa tunataka kuimarisha viwanda, tunataka kufufua viwanda. Eneo ambalo DART wameamua ku-plan kwa ajili ya kulipa fidia zaidi ya bilioni 186 ni eneo la viwanda ambavyo vingine vinazalisha. Lakini ukitoka kilometa sita kutoka pale Mbagala Rangi Tatu kwenda mpaka Kongowe kuna msitu mkubwa umejaa pale hauna kazi yeyote, kwa nini wasi-extend mpaka kufikisha pale vikindu ule msitu, hauna kazi yoyote zaidi ya kuwa maficho ya majambazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mheshimiwa Waziri Maghembe ametoa heka pale ambazo zile zingesaidia ile DART wangei-extend ili Serikali isipoteze fedha nyingi ya fidia ikiwa eneo lipo. Ningeomba sana Mheshimiwa Simbachawene watu wa DART walitizame hili kuliko kupoteza fedha pasipokuwa na sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wengi wamezungumza kuhusu CAG, ni kweli CAG anafanya kazi katika mazingiara magumu sana. Naomba Serikali hii ya Awamu ya Tano yenye nia njema ya kumkomboa Mtanzania wamuwezeshe CAG aweze kufanya kazi. Bila kufanya kazi CAG Kamati hizi zinakuwa hazina macho kabisa na zinakuwa hazina uwezo wa kutekeleza majukumu yake. Lakini nimuombe Waziri wa Fedha, nina taarifa Halmashauri zetu Dar es Salaam bado hazijapata gawio la property tax. Na hata hao TRA wenyewe wanasema ndiyo kwanza wanaanza kujipanga na kutoa semina ili waanze kukusanya mapato. Ndugu zetu mmetuchukulia chanzo hiki kikubwa kwa Halmashauri za Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo Serikali inashindwa kuleta hizi fedha mnategemea tutekeleze vipi miradi ya maendeleo, mnategemea tujiendeshe vipi? Kama jukumu hili mmelishindwa naomba mrudi nyuma, mjisahihishe mtuachie Halmashauri tukusanye property tax ili tuweze kutekeleza miradi yeti ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, Sheria ya Manunuzi ya Umma (Public Procurement Act) ni tatizo katika Halmashauri zetu, zinachukua muda mrefu procedure hizi mpaka kuweza kutangaza mzabuni. Lakini huyo mzabuni anayepatikana, anapatikana kwa gharama kubwa, naomba sana Serikali ifanye marekebisho ya sheria ili sheria hii iweze kutusaidia, isiwe kikwazo katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna kero kubwa ya uhakiki wa madeni ya walimu, hasa waliosahihisha mitihani ya darasa la saba na darasa la nne. Walimu hawa hawajalipwa muda mrefu, wamekuwa wakilalamika na kila wakija Wakurugenzi wanasema fedha hazijatoka kutoka Hazina hazijaletwa kutoka Serikali Kuu. Naomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma walimu hawa ambao wanatusaidia kuboresha elimu ya watoto wetu na wao ni watumishi wanastahili kupewa haki, kwa wakati ili waweze kuwa na moyo na morali wa kuweza kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo lingine ningependa kulizungumzia na nitatolea mfano Halmashauri ya Jiji au Mji wa Iringa. Walikuwa na mpango na mwekezaji wa kuwekeza katika eneo la machinjio na kituo cha mabasi, lakini wamepeleka Wizarani karibu miaka minne sasa hivi hawajapata majibu na sisi Temeke pia tumepeleka Wizarani project zetu, lakini mpaka leo hatujapa kibali cha Waziri husika na ushauri wa CAG. Kwa hiyo, ile miradi baadaye inakuja ina-collapse Halmashauri zinashindwa kuwekeza.
Kwa hiyo mimi ningeomba sana Serikali ibadilishe utaratibu, ili Halmashauri hizi zikiwa na plan ya kuwekeza basi uwekezaji ule ufanyike kwa haraka na wapate ridhaa ya Waziri na wahusika kwa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile suala la Mifuko ya Hifadhi za Jamii. Jamani wastaafu wetu wanateseka sana, hawapewi mafao yao kwa wakati, tangazo la nyongeza ya Serikali mpaka sasa hivi hakuna na majibu yanakuwa hakuna na hawa watu ni wastaafu, wanachotegemea ndicho hicho hicho kilichokuwepo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hapa nimesoma ripoti ya PAC Serikali inadaiwa pesa nyingi sana na Mifuko ya Hifhadhi za Jamii. Lazima tuseme ukweli kama hili ni tatizo basi Serikali ijipange, Mifuko ya Hifadhi za Jamii iwe inalipwa at least nusu ya madeni yao ili waweze kujiendesha na waweze kulipa madeni yao mbalimbali ikiwemo pamoja na kuwalipa wastaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, wastaafu wanahangaika sana, wastaafu wanapata shida sana. Mimi ningeshauri sana Serikali iwaangalie wastaafu kwa jicho la huruma.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile limezungumzwa hapa kwa upana sana suala la UDA. Ni kweli UDA ina kigugumizi na hatujapata majibu yake, lakini sisi tuombe Halmashauri zetu nazo zinatakiwa zipate zile unallotted share basi na sisi tuelekezwe jinsi gani ya kuzipata ili tuweze kumiliki. Lakini sio hilo tu kuna suala la pesa ambazo ziko mpaka sasa hivi benki, kama ni ndogo kaeni fanyeni negotiation na mwekezaji, ziongezeke au kama mwekezaji hatakiwi tupewe taarifa hizi ili zile pesa kama inawezekana basi zitumike kwenye miradi ya manendeleo katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hilo tu kuna suala la pesa ambazo ziko mpaka sasahivi benki. Kama ni ndogo kaeni fanyeni negotiation na mwekezaji ziongezeke au kama mwekezaji hatakiwi, tupewe taarifa ili zile pesa kama inawezekana basi zitumike kwenye miradi ya maendeleo katika Halmashauri zetu na Manispaa zetu, lakini kero hii naomba iishe na hili neno liwe lilefutika kwa sababu, linawezekana na kama kukiwa na nia njema na ukweli na uwazi katika jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ningeomba sana, wengi wamezungumza na ni kweli sasahivi kuna mkanganyiko maana sasahivi Mbunge ukishirikiana na wananchi unaambiwa mchochezi. Mkuu wa Wilaya anataka wewe uende pale umpigie salute. Ni vizuri mkawapa semina Wakuu wetu wa Wilaya, mkawapa semina viongozi wetu ili wajue mipaka ya majukumu yao, wajue heshima ya Mbunge ni ipi, heshima yake yeye ni ipi na vilevile mgawanyo wa madaraka yake na majukumu yake ni upi.
Mheshimiwa Naibu Spika, isifike mahali Mbunge unaalikwa uende kwenye mahafali na Mkuu wa Wilaya mnapishana na yeye anataka kwenda kwenye mahafali. Kila mtu ana majukumu yake na katika maeneo yake. Naomba sana semina elekezi kwa viongozi wetu zitolewe ili kusiwe na mgongano. (Makofi)
Lakini lingine kumekuwa sasa hivi, hasa kwa Madiwani, nilipata taarifa kwamba kuna baadhi ya Madiwani wamekamatwa, wamewekwa ndani kisa wanaambiwa ni wachochezi. Haya mambo yanaweza yakazungumzika katika maeneo yale na yakaweza kusawazishika. Si kila jambo lazima itumike nguvu, kuna mambo ambayo tunaweza tukawaelewesha, watu wakaelewa na wakatekeleza wajibu wao na nchi yetu ikabaki kuwa salama na tukawa wamoja kwa amani na utulivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme pale ambapo kuna maelewano, pale ambapo kuna maridhiano maendeleo yatapatikana. Pale ambapo kuna migongano maendeleo hayawezi kupatikana, tutumie busara katika…
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono.