Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwanza nimshukuru Mungu kwa namna pekee ametujalia mpaka muda huu tuna afya njema. Naomba tu niseme mimi ni mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na naanza kuchangia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza naomba Serikali iiangalie Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwanza kwa masuala ya bajeti. Tulisema na wenzangu wamesema basi ni wakati muafaka sasa kushughulikia suala hili. Waziri wa Fedha aliahidi mwezi Disemba ataangalia utekelezaji na ataongeza fedha kulingana na kazi zinavyoenda. Tunaomba ahadi hiyo ikifika Disemba wakati wa kupitia bajeti aliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Ofisi ya CAG kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanya, tumeona matunda yake kwani wameibua hoja nyingi, kwa hiyo tunawapongeza sana. Pamoja na pongezi hizi tunahitaji Ofisi ya CAG iboreshwe zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa vikao vya briefing vya kupitia hoja zao ambazo wamezikagua na wamezileta kwenye Kamati tuliweza kugundua upungufu mdogo mdogo aidha ni wa wafanyakazi au mfumo, hili tutaomba aliangalie. Kwa mfano, kuna wakati tuliwahi kuwauliza maofisa wanaotoka CAG, kwenye auditing kuna kitu kinaitwa analytical review, una-check movement, una-analyze kati ya mwaka wa fedha huu na mwaka wa fedha hata miwili, mitatu iliyopita. Hiyo ndiyo auditing ambayo inafanyika tukaona kwamba hii Ofisi ya CAG ni kama vile inafanya kazi kama internal auditor badala ya external auditor. Kwa sababu uki-check movement ya accounts mbalimbali hiyo ndiyo audit japokuwa utaenda kwenye item na ukapata zile schedule na utaangalia utajiridhisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunahitaji wa-improve maeneo mbalimbali kwenye audit procedures, audit technique na audit plan ili waweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika utendaji wa Ofisi ya CAG tunajua wanaangalia muhtasari wa vikao vya Kamati za Fedha za Halmashauri zetu, lakini inabidi waongeze juhudi kwa sababu kwenye Kamati hizi za Fedha na Mipango ndipo mahali ambapo maoni mengi yanatolewa kuhusiana na matumizi mbalimbali ya fedha za Halmashauri. Kwa hiyo, tunaomba waongeze sana juhudi kwenye kuangalia muhtasari wa vikao vya Kamati vya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukizihoji Halmashauri mbalimbali tuligundua kuna upungufu kwenye mfumo wa kihasibu kwa kutumia computer (EPICOR). Maoni yangu ni kwamba Serikali iangalie mfumo huu wa EPICOR tangu tumekuwa nao kwa miaka yote hii umetusaidia nini? Kama hauna msaada wowote ambao umeutoa kwa nini tusipate mfumo mwingine wa kihasibu kwa kutumia computer? Kwa sababu kumekuwa na upungufu mbalimbali, modules nyingi zimekuwa hazifanyi kazi na maeneo mengine kweli Halmashauri wanakuwa hawajawekewa mfumo huu, lakini ile link pamoja na platform zingine za kiuhasibu na za report zimekuwa hazifanyi kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ifanye upembuzi yakinifu kuangalia upungufu ulioko kwenye EPICOR. Dunia ya sasa hivi ina mifumo mingi ya accounting package ambayo inakuwa ni strong hata internal control yake inakuwa ni strong, huwezi uka-temper data. Kwa hiyo, tuhame kutoka kwenye EPICOR twende kwenye software zingine ambazo zitakuwa na msaada kwenye Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona maeneo mengi pia kama TAMISEMI haijaweza kukamilisha ufungaji wa EPICOR na wakati huo huo kwenye Halmashauri zetu kumekuwa na tatizo la mtu mmoja ndiyo anakuwa mtu wa EPICOR tu watu wengine wanakuwa hawajifunzi pale pale ndani. Kwa hiyo, hilo nalo Waziri wa TAMISEMI aangalie, kwenye Halmashauri isiwe anategemewa mtu mmoja kama atahama au atakufa au atakuwa anaumwa mambo mengine yatakuwa yamelala.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni upande wa Hazina, miradi mingi haijatekelezwa kwa sababu fedha zimekuwa hazipelekwi kwa wakati au zimepelekwa kiasi. Kwa hiyo, tumuombe Waziri wa Fedha akaangalie commitment ambazo zimefanywa na Halmashauri zetu, wengi walishatoa GPN wapelekewe fedha ili miradi ya maendeleo iweze kufanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni upande wa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa. Wakati wa vikao vyetu Katibu Tawala wa Mkoa wameji-commit kwenda kuhakikisha kwamba Halmashauri zinafanya kazi ipasavyo.
Kwa hiyo, tumuombe Waziri wa TAMISEMI akahakikishe kwamba anawakumbusha, maana Wakurugenzi wengi wameahidi kushughulikia ule upungufu ulioonekana na wengi wameahidi kwa maandishi. Tuombe Ofisi ya Katibu Tawala ya Mkoa kuhakikisha kwamba anazisimamia hizi Halmashauri ipasavyo ili hata masuala mengine CAG anakuwa anapunguziwa kazi kwa sababu wao wapo kila siku na wana watumishi katika ngazi ya Mkoa wenye fani mbalimbali na wanaweza kusimamia hizi Halmashauri ndani ya Mkoa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni deni la 10% ambapo Halmashauri zinatakiwa zitenge fedha kwa ajili ya kukopesha vijana na akina mama ili waweze kupata mikopo ambayo riba yake ni nafuu sana. Tatizo ambalo tumeligundua fedha hizi hazina akaunti maalum benki, kwa hiyo, zinakuwa kwenye pool moja na Halmashauri zetu pale OC zinapochelewa wanatumia fedha hizi. Kwa hiyo, niombe Waziri wa TAMISEMI alichukue hili, apeleke mwongozo waidhinishe Halmashauri ili ziweze kufungua account bank ziwe maalum kwa ajili ya kuweka hizi fedha za 10% baada ya kuwa wamezikusanya ili kuongeza udhibiti wa kutokutumia kwenye matumizi mengine. (Makofi)
Jambo lingine ni suala zima la Kamati za Bunge kuwa na ufinyu wa bajeti. Tunaelewa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 63, wajibu wa Bunge ni kutunga sheria na kuisimamia Serikali na kupitia hizi Kamati tunakuwa tunaisimamia Serikali lakini fedha zimetengwa kwa kiasi kidogo na hatukamilishi kazi. Kwa hiyo, tutakuwa tuna-save kumi lakini kwa usimamizi ambao hatuufanyi tunapoteza mia. Kwa hiyo, niiombe Serikali kwenye mapendekezo ya mpango tulichangia hivyo na Waziri wa Fedha ahakikishe kwamba bajeti ya Bunge isiwe chini ya 20% ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2015/2016. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuchangia ni kuhusu operesheni za Halmashauri zetu. Makusanyo ya ndani yana mgawanyo kwa mujibu wa kanuni na sheria, kuna 60% iende kwenye miradi ya maendeleo, 20% maeneo mengine na 10% kwa vijana na akina mama. Niombe Ofisi ya CAG ikasimamie sana mgawanyo wa hizi fedha wanazokusanya wenyewe (own source) kulingana na sheria ili tuhakikishe kwamba miradi ya maendeleo kwenye Halmashauri zetu na kwa wananchi wetu hasa maeneo ya afya, elimu na maji inafanyika kwa fedha za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kwa kuunga mkono ripoti ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa na niombe Serikali ikatekeleze mapendekezo yote ambayo yameonyeshwa mule ndani na sisi kama Kamati ihakikishe kwamba tunapata mrejesho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.