Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Rose Kamili Sukum

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. ROSE K. SUKUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana nami kupata fursa hii ili niweze kuchangia taarifa ya Kamati kuhusu Hesabu Serikali za Mitaa pamoja na PAC. Kwanza kabisa niombe Wabunge wote tukubali kupokea maoni au mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ili kuweza kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya hii ya LAAC ina kazi ngumu sana. Wote tutambue kabisa kwamba Halmashauri zetu zote zinatakiwa zikaguliwe na Kamati ya LAAC. Kila Mbunge hapa ana Halmashauri yake, nadhani haya maoni yanamgusa kila mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuzungumzia suala la ugumu na usugu wa matatizo ambayo yako kwenye Halmashauri na yote yanatokana na kwamba sasa hivi Serikali yetu ambayo haitaki kusikia imesema ina ufinyu wa bajeti. Kama kuna ufinyu wa bajeti, umebana hizo fedha ili uweze kufanya jambo, kama hawakaguliwi si ndiyo wizi unaongezeka? Kama unaongezeka, nani anaweza kuwabana kama Kamati ya LAAC au PAC haitapewa mafungu ya fedha ili kwenda kutembelea miradi yote ambayo inafanyiwa kazi na Halmashauri zetu au na Wizara mbalimbali? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ucheleweshaji wa fedha katika Halmashauri zetu umesababisha baadhi ya miradi kutokamilika. Miradi hiyo haikamiliki kwa sababu fedha zinapochelewa kwa kuwa baadhi ya Maafisa Masuuli na Wakuu wa Idara waliopo kwa tamaa waliyonayo basi hutumia fedha zile halafu wanasubiri za mwaka unaofuata. Kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa ambalo lipo la Serikali kuchelewesha hizo fedha za maendeleo nao wanachangia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ifikie sasa mahali Serikali ikubali kwamba fedha zikitolewa zitolewe kwa wakati ili maendeleo ya watu yaweze kufanyika. Ndicho tulichokiona kwenye Kamati ya LAAC tulipokuwa tunaendelea kukagua kwamba ucheleweshaji ule unasababisha Maafisa Masuuli kula hizo fedha bila kutumia utaratibu unaofaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine maagizo kutoka ngazi ya juu yamesababisha ubadhirifu wa fedha au kutumia fedha ambazo haziko kwenye bajeti katika Halmashauri zetu. Utakuta Mkuu wa Mkoa anawaagiza wakatumie fedha kwenye mafungu ambayo yeye hausiki kupitisha hiyo bajeti, DC naye anaagiza, DAS anaagiza, RAS anaagiza na kuchukua fedha. Kwenye ukaguzi huo tumeona kwamba kuna RC alikuwa anaagiza fedha zitumike kwenye sehemu ambayo haipaswi kutumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huo ndiyo ubadhirifu mmojawapo ambao tumeugundua kwenye Kamati ya LAAC. Tunaomba haya maagizo yanayotoka juu basi wawe na mafungu yao ya fedha, mnataka kutengeneza madawati mtuambie fedha iko wapi ili wakatengeneze madawati. Siyo unaagiza watengeneze madawati halafu hakuna fedha kwenye bajeti, ni ngumu sana kufanya hiyo kazi kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine, sisi Kamati ya LAAC mmepata taarifa kwamba tumekagua Halmashauri 66. Sababu ya kukagua Halmashauri 66 ni ukosefu wa fedha tumeshindwa kwenda kukagua hata miradi ya maendeleo. Kati ya Halmashauri 164, ni Halmashauri 66 tu ndiyo zimekaguliwa, je, ubadhirifu unaoendelea kufanyika kwenye zile Halmashauri zilizobaki ni kiasi gani? CAG pia amekosa hizo fedha, je, kama CAG hajaenda kukagua ile miradi ya maendeleo ubadhirifu unafanyika kwa kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke suala value money, wanasema fedha zimekwenda kuchimba kisima, visima ni hewa, zimeenda kujenga sekondari, sekondari ni hewa, zimeenda kutengeneza barabara, barabara ni hewa na hakuna anayekwenda kukagua. Waziri wa TAMISEMI unafahamu kabisa wewe peke yako hutoshi kwenda kukagua hizo Halmashauri zote, lazima tusaidiane. Leo mnabana hizo fedha, je, tunafanyaje sasa na fedha zimetumika vibaya na hakuna miradi ya maendeleo iliyofanyika? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, udhaifu na udhibiti wa Mkaguzi wa Ndani. Mkaguzi wa Ndani yuko chini ya Internal Auditor General, lakini huyu Mkaguzi wa Ndani kwa masuala ya kiutawala yuko chini ya DED, hebu niambieni atawapeni taarifa iliyo sahihi kweli kama yuko chini ya DED? Matokeo yake yule Mkaguzi wa Ndani anashikwa anaambiwa ukitaka usafiri, ukitaka hela usitoe taarifa inabidi asizitoe. Je, tunafanya nini kuhusu huyu Mkaguzi wa Ndani?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri katika Halmashauri zetu Mkaguzi wa Ndani asiwe chini ya Mkurugenzi au Afisa Masuuli kwa sababu taarifa hazitolewi mpaka wagombane, wakishagombana na Mkurugenzi ndiyo unapewa taarifa kwamba kuna fedha imeliwa au kuna kitu fulani kimefanyika. Nashauri kwamba Mkaguzi wa Ndani awe chini ya Internal Auditor General na taarifa zake ziende pale na utaratibu wa shughuli zake zote utoke kule au awe chini ya CAG kuliko kuwa chini ya Mkurugenzi wa Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulizingumzia, kazi ya ufuatiliaji na usimamizi ni ngumu sana na kubana matumizi pia inahitajika lakini Kamati zote kutotembelea miradi hatufanikiwa. Kamati ya PAC na LAAC kama hazitatembelea miradi hatutaweza kufanikiwa kwa jambo lolote. Tumeona wote tuliokuwepo kwenye hizo Kamati kwamba kama hatukwenda kutembelea tunaangalia taarifa ya kwenye makaratasi hatutafanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Afisa Masuuli anaweza kuwa mjanja, suala la risiti zinaweza kuandikwa zikaletwa hapo na akawa na hati safi, lakini kumbe kule kwenye kazi hakuna kilichofanyika. Kwa hiyo, nadhani sasa suala la ufuatiliaji kama lipo tunatakiwa sisi kama Kamati ya LAAC, kama Kamati ya PAC au Wabunge wote kwa ujumla kutembelea miradi ili kuhakikisha kwamba miradi inafanywa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho kimeonekana zaidi ni kwamba wakati Bunge linaendelea na Halmashauri zinaendelea na vikao vyao. Hiyo imesababisha sehemu kubwa sana ya Wabunge kutokujua mapato na matumizi yanayofanyika kule. Hata Mfuko wa Jimbo imeonekana wazi kabisa Mbunge hajui fedha zake zimetumikaje na hata akiuliza anaambiwa hela zimeshatumika zimefanya kazi zingine. Kama Mfuko wa Jimbo unaweza kutumika, Wabunge mna kazi gani kama hamuwezi kudhibiti mapato na matumizi ya Halmashauri zetu au ya Serikali kwa ujumla? Kwa hiyo, tunatakiwa kupata hiyo fursa ili kuweza kufanya kazi ya usimamizi wa Halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokigundua zaidi kwenye Halmashauri zetu pamoja na kwamba tuna manunuzi yasiyozingatia sheria lakini pia kuna watu ambao wanatumia nafasi zao kuingiza mikono yao pale. Mkuu wa Mkoa anakwambia umtumie mkandarasi huyu, mimi ndiyo nawaagiza na mkandarasi hajatimiza wajibu wake. Je, hamuoni kwamba tunatumia fedha za umma vibaya? Tunawalalamikia sana Maafisa Masuuli kutofanya kazi yao vizuri lakini sehemu kubwa ni maagizo yale yanayotoka kwa sababu ni mkubwa anamuagiza Mkurugenzi, haya yametokea maeneo mengi kwenye Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi suala la Wakurugenzi ambao hawaelewi utaratibu wa Halmashauri imekuwa ni tatizo kubwa. Uteuzi wa juzi tu umefanyika Julai lakini kilichotokea kwenye Halmashauri ya Hanang mfano kuna watumishi wamekula fedha shilingi bilioni 1.2 na uchunguzi umefanywa na Mkuu wa Mkoa na imebainika fedha hiyo kuliwa, lakini kwa kuwa Mkurugenzi haelewi, maskini ya Mungu ametoka TFDA hajui masuala ya Halmashauri akapewa ushauri na wale waliotumia ile fedha kwamba hawa watumishi waliokuwa hiyo fedha tunashauri warudi kazini wateremshwe vyeo siyo wachukuliwe hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiona suala kama hilo ujue kwamba hawa Wakurugenzi wapya wanahitajika aidha wakapewe semina au waende shule ambayo itawasaidia kujua ni namna gani watakavyoweza kuendesha hizo Halmashauri. Kwa sababu kama unashauriwa na mtumishi wa chini yako uliyemkuta pale ambaye na yeye amehusika kwenye kutumia hizo fedha halafu na wewe unaishauri council kwamba hawa watumishi adhabu yao ni kuteremshwa cheo, wamekula shilingi bilioni 1.2. Hebu niambie kwa nini wale wa Kagera wameshtakiwa kwa Rais wakati yule wa Hanang aliyekula shilingi bilioni 1.2 anaambiwa aendelee na kazi? Kwa hiyo, kuna mambo ya kufanya ili kuweza kuisaidia Serikali hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.