Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Subhana Wataala kwa kunijalia uzima na afya na kuniwezesha kuchangia taarifa hizi mbili muhimu, ile ya LAAC ambayo imetolewa na Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale Mwiru, mtoto wa Kingunge, hongera sana kwa kazi nzuri na Mheshimiwa Kaboyoka, taarifa zao ni za kina kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za CAG ndizo ambazo wenzetu hawa wanazifanyia kazi. Taarifa zote hizi mbili ni nzuri, lakini tatizo la kutopatikana kwa fedha kwa viongozi wa Kamati hizi mbili kwenda katika maeneo mbalimbali kujionea uhalisia wa miradi ya maendeleo, kuangalia value for money, jinsi gani fedha zilivyotumika, limekuwa ni kubwa kweli. Kazi ambayo wameifanya Wenyeviti hawa wawili ni kubwa lakini kama hawapewi fedha za kwenda katika maeneo mbalimbali kuangilia uhalisia na kile kitu kinachoitwa value for money ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi nimpongeze Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, naye vilevile nimwonee huruma kidogo baada ya kumpongeza, kama alihitaji shilingi bilioni 62, Serikali imekwenda kumpa shilingi bilioni 18 atafanya kazi vipi? Huu ni upungufu mkubwa sana! Kila mtu aliyepewa dhamana na Serikali atengewe fedha ya kutosha ili atakapotoa mapendekezo yake basi yawe ni kweli. Kama Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaomba shilingi bilioni 62 anaenda kupewa shilingi bilioni 18 kuna jambo, tatizo kubwa. Kwa mara nyingine naishauri Serikali iandae mpango madhubuti, mpango makakati, ulio mzuri na mahsusi wa kuweza kutoa fedha hizi kwa wahusika hawa. Hiyo ili kuwa ni chombeza ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, wachangiaji wenzetu waliopita walisema kwamba moja ya tatizo kubwa hapa ni Hazina kuchelewesha kutoa fedha za maendeleo katika Halmashauri au kutopeleka kabisa. Utekelezaji wa miradi ambayo tumepanga sisi Waheshimiwa Wabunge na ikumbukwe kwamba asilimia 70 ya fedha za maendeleo zinakwenda kwenye Halmashauri, kama Serikali haitaki kutoa fedha kwa wakati, inachelewesha au haitoi kabisa ina maana sisi Wabunge ni kama danganya toto tu. Tatizo ni nini kwa Serikali? Ni lazima Serikali ikumbuke kwamba sisi Wabunge tunapopiga kelele na kuandaa mazingira mazuri basi hizi fedha waweze kuzitoa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya upungufu mkubwa unaonekana ni suala zima la Wakurugenzi wengi katika Halmashuri kutokuwa na sifa na ndiyo maana miradi mingi ya maendeleo huwa inakwama. Wenyeviti wetu na Kamati kwa ujumla waliwaita baadhi ya Wakurugenzi kuja kutoa taarifa, unaona jinsi wanavyojikanyaga kanyaga, hawana sifa. Wakurugenzi hawa wanachukuliwa kwenye NGOs, ni vyema Wakurugenzi hawa watoke katika utumishi na wajulikane wana sifa fulani lakini wapi, tatizo nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mikakati ya kuziboresha hizi Halmashauri zetu ni kwamba yale makusanyo ya ardhi ambapo fedha hizi zinakwenda moja kwa moja Serikalini inatakiwa asilimia 30 zirudi kwenye Halmashauri lakini hawapewi. Kwa hiyo, Halmashuri zinadhulumiwa, zinanyanyaswa, zimekuwa maskini na Serikali imekaa tu, tutafika kweli? Sijui. Niiombe sana Serikali iandae mpango mkakati na mzuri kabisa ili Halmashauri iweze kupata hizi asilimia 30 kutoka Serikali Kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende sasa katika lile la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambaye katika taarifa hizi ni jicho la kuona. Nitaanza na taarifa moja moja na naomba niende kwenye ukurasa wa 141 ambapo kuna ubadhirifu wa fedha ambao umefanywa. Kwa mujibu wa ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha unaoishia 30 Juni, 2005 kuna suala zima la Kivuko cha Kigamboni ambacho kinatoka Kigamboni kwenda Dar es Salaam. Kivuko hicho kilifanyiwa majaribio ni kibovu na kwa mujibu wa ripoti kilinunuliwa kwa dola za Kimarekani 4,980,000 karibu shilingi bilioni 10 lakini hakikufanya kazi, ni tatizo kweli, ina maana hapa Serikali imeingia hasara wakati tuliambiwa kivuko hiki ni kizuri, ni bora lakini hapa pametokea matumizi mabaya ya fedha za umma.
Niishauri Serikali kwa kuwa aliyekuwa Waziri katika Wizara hii sasa ni Mtukufu mwenyewe wa heshima, kiongozi wetu, ni vema ashauriwe kwamba watu wote waliompelekea Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingia katika mkataba huu mbovu wa shilingi karibu bilioni 10 kununua kivuko kibovu ambacho ni cha kutoka Bagamoyo kuja Dar es Salaam na hakifanyi kazi, watu hawa Mheshimiwa Rais awatumbue. Yeye mwenyewe anawajua, yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais awatumbue watu hawa ambao walituingiza katika mkataba mbovu na Ujerumani kwa dola za Kimarekani 4,980,000 karibu shilingi bilioni 10 na kivuko hiki kikawa hakina sifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali ikasema kwamba hati ya makabidhiano haikutolewa. Kivuko kilikabidhiwa bila hati ya makabidhiano jambo ambalo ni baya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote sifa ya kiwango cha kutembea ni tatizo. Ukiangalia kivuko cha Bakhresa kinatoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar ambacho kimenunuliwa shilingi bilioni nne, kinatumia saa moja na nusu lakini kutoka Bagamoyo kuja Dar es Salaam saa tatu. Ni vema kwa kuwa kiongozi mkuu yeye mwenyewe alikuwa ndiyo wakati huo ana dhamana mumshauri wale wote waliotuingiza katika mkataba huu awatumbue alfajiri mapema ili wananchi wapate imani nao, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala zima la wastaafu. Mara nyingi kumekuwa na malalamiko, ripoti nyingi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zimekuwa zikizungumzia jinsi gani wastaafu wanavyoonewa, wanavyopunjwa na wanavyodhulumiwa. Ukiangalia ripoti zote za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, nianze na inayoishia mwaka 2015, kati ya majalada 4,683 ya wastaafu yaliyokaguliwa majalada 200 yalipunjwa jumla ya shilingi milioni tatu themanini na tano laki tatu na mia nne themani na moja. Utetezi wa Serikali na kinachoonekana tatizo ni kukokotoa, mnakokotoa jambo gani jamani? Majalada 200 wastaafu wamepunjwa, wamedhulumiwa na ndiyo maana wakawa maskini. Wastaafu hawa wakishakufa risala nzuri na mnatoa machozi, machozi ya nini wakati mliwaonea alfajiri mapema? Roho mbaya kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inakuwaje leo ripoti inayoishia 2014, majalada 4,764 ya wastaafu yaliyokaguliwa majalada 283 yamepunjwa shilingi 481,456,311, jamani! Kila siku wakati wa kustaafu hawataki kuwatendea haki wastaafu. Wastaafu hawa na wao walikuwa ni wafanyakazi wetu, wameshastaafu jambo gani kubwa la msingi mnashindwa kukokotoa mkawapa haki zao. Kila siku ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaonya kwamba wakati wa kukokotoa basi Serikali iwe makini au hakuna wataalam? Jamani, aibu si aibu, ni shida kweli. Kila mmoja ni mstaafu mtarajiwa kuna Wabunge wastaafu na watu wengine mbalimbali, lakini wastaafu hawa ni vema kwa vyovyote iwavyo waangaliwe kwa jicho la huruma ni jinsi gani wanavyodhulimiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye jambo lingine, nikuombe habari zifike kunakohusika, kwa sababu Serikali hapa ipo, inakuwaje sisi kila siku tunaingia kwenye mikataba mibovu? Tumeingia mkataba na Shirika la Ndege kipindi kile la South Africa na Shirika letu la Ndege la Tanzania (ATCL) tukakodi ndege (Airbus 320) na baadaye ndege hiyo ilikuwa ni mbovu, ikapelekwa Ufaransa kwa matengenezo, ikasuasua, ikaondolewa ikapelekwa Guinea, ikapakwa rangi, tumepata hasara ya shilingi bilioni 91 nani katumbuliwa? Mnatumbua maskini za Mungu waliokuwa hawana kitu, tumbueni hawa, hawa ndiyo wa kutumbuliwa. Wameiingizia hasara Serikali ya shilingi bilioni 91 mbona hawa hawatumbuliwi? Muwatumbue na hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali anapotoa maelezo yake kwamba kuna wizi, ubadhirifu na ufisadi mkubwa kama huu, Serikali lazima mtilie maanani, muone kwamba hili jambo ni la msingi sana vinginevyo ni shida kweli! Hata ukichangia kiasi gani, Serikali inasema ni sikivu, inasikia kilio chetu lakini usikivu uko wapi? Sisi wengine tunapata shida kweli Serikali ukiishauri haikubali. Kazi ya Bunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali lakini Serikali haikubali kusimamiwa ni shida na inavyoonekana Serikali haitaki kusimamiwa, wanataka watusimamie sisi tutakubali wapi, hatukubali. Tutachombeza hivi hivi kidogo kidogo kuna siku mambo yatawaingia vizuri muweze kutufanyia yale ya haki na hasa kwa wananchi. Haiwezekani shilingi bilioni 91 ziende, ndege mbovu, muiondoshe Ufaransa muipeleke Guinea muipake rangi, lakini hakuna aliyekamatwa, ni shida kweli, tutafika sisi kweli? Sijui, kwa sababu ameingia Trump inawezekana akatusaidia pengine anasikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, mimi sitaki nichombeze chombeze sana, naomba jicho hili la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mumpatie fedha aende katika maeneo mbalimbali. Haiwezekani anaomba shilingi bilioni 62 anapewa shilingi bilioni 18. Mheshimiwa Kaboyoka na Mheshimiwa Ngombale nao hawakupewa fedha za kutembelea maeneo mbalimbali kujionea wenyewe, value for money iko wapi, hamna kitu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumbe wao ripoti walitumiwa moja kwa moja kwenda site hakuna. Bunge ndiyo…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana nashukuru na naomba kuunga mkono hoja.