Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha majadiliano kwa ufanisi kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitambue michango mizuri iliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini na Makamu Mwenyekiti wake Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatambua pia mchango wa Waziri Kivuli na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe. Aidha, ninawashukuru kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia mjadala huu ambapo kwa kuzungumza walichangia Wabunge 70 na kwa maandishi wamechangia Wabunge 48 wakiwemo Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Naibu Mawaziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla mjadala ulikuwa mzuri na baadhi ya maoni yalitolewa kwa hisia kali na mimi ninaamini kwamba, kwa kuzingatia umuhimu wa uchumi katika nchi yetu ni jambo jema tukawa tunachambua, tukabishana na hatimaye turidhiane juu ya vipaumbele, mikakati na hatua stahiki za kukuza uchumi wa Taifa kwa namna ambayo ni endelevu zitakazo wezesha nchi yetu kufikia malengo ya dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia kuwa tumepokea michango na hoja nyingi tena sana kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge naomba niahidi hapa kuwa nitawasilisha Bungeni taarifa ya maandishi inayofafanua hoja zote zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema yako maoni na ushauri mwingi uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge, ninaomba nisiseme kwa kifupi yale yaliyosemwa ni mengi sana, nilitamani walau niseme hata kumi tu kwa msisitizo ili mjue kwamba tunasikia, lakini kwa ajili ya muda naomba nijielekeze zaidi kufafanua hoja chache hasa zile ambazo nadhani ni muhimu tukaelewana vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni hoja kubwa ambayo toka mwanzo mpaka mwisho imesemwa kwamba uchumi unahali mbaya, uchumi umedorora na kwamba kuna manung’uniko ya wananchi mtaani.
Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wa Taifa unapimwa kwa vigezo vingi, haupimwi kwa kigezo kimoja wala viwili, nitasema baadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, viko vigezo vya ujumla, ukuaji wa Pato la Taifa. Uchumi wa Taifa kwa kipindi cha Januari mpaka Juni, 2016 kwa wastani umekuwa kwa asilimia 6.7 ukilinganisha na asilimia 5.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2015. Asilimia 6.7 ni kasi kubwa ya ukuaji wa uchumi. Ngoja niwapeni mfano, wastani wa ukuaji wa uchumi kwa Sub-Saharan Africa kwa mwaka 2016 ni asilimia 1.4 tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya wanakuwa kwa asilimia 6, Uganda asilimia 4.7, Mozambique asilimia 6.5, Tanzania quarter hii iliyokwisha asilimia 7.2 jamani tujitendee haki. Sekta zilizokuwa zaidi hapa kwetu ni uchukuzi na uhifadhi wa mizigo, uchimbaji wa madini, mawasiliano, sekta ya fedha na bima, na hizi zimekuwa kati ya asilimia 17.4 mpaka asilimia 15. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumuko wa bei. Januari, 2016 tulikuwa asilimia 6.5, Juni, 2016 asilimia 5.5, Septemba, 2016 asilimia 4.5, hicho ni kigezo kimojawapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, akiba ya fedha za kigeni, Ni dola za Kimarekani bilioni 4.1 mwezi Septemba, 2016 ambayo inatuwezesha kununua bidhaa na huduma kwa kipindi cha miezi minne. Urari wa biashara (current accaount deficit), imepungua kutoka dola milioni 1,207 katika quarter ya Julai mpaka Septemba, 2015, imerudi dola milioni 601.8 Julai mpaka Septemba, 2016. Jamani vigezo vyote hivi vinatuonesha tuko vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwenendo wa sekta ya kibenki. Sekta hii imeendelea kukua na ina mitaji na ukwasi wa kutosha. Mitaji ukilinganisha na mali iliyowekezwa, nilisema wakati natoa hoja hapa, total risk waited assets na off balance sheet exposures ni asilimia 19.08 ukilinganisha na kiwango cha chini ambacho ni asilimia 12 tu. Mali inayoweza kubadilishwa kuwa fedha taslimu ikilinganishwa na kiwango cha amana zinazoweza kuhitajika katika muda mfupi (liquid assets to demand liabilities) asilimia 34.18 wakati kiwango cha chini kinachohitajika ni asilimia 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli shida kubwa tunayoona pamekuwepo na mikopo chechefu. Septemba, 2015 ilikuwa ni asilimia 6.7 sasa imeongezeka kufikia asilimia 9.1, na ndiyo sababu tumeona mabenki ambayo yamepata hasara; CRDB kati ya Julai na Septemba wamepata hasara, TIB Development Bank wamepata hasara, na sababu ni hiyo ya mikopo chechefu. Twiga Bancorp nayo tumeiweka chini ya uangalizi wa Benki Kuu, lakini siyo kitu cha ajabu. Crane Bank Limited ya Uganda nayo imewekwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu yao mwezi uliopita. Imperial Bank ya Kenya nayo iliwekwa chini ya uangalizi Oktoba, 2015 na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya kibenki kwa ujumla ilipata faida, pato kwa rasilimali (retain on assets 2.53) na kadhalika, naweza nikaendelea kueleza lakini sisi tunavyotazama vigezo vingi vya uchumi vinatuonesha tuko sawa sawa. Nitakuja huko kwingine kwanini tunasikia maneno mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwango vya ubadilishanaji fedha (exchange rate) hatuko pabaya. Ule upungufu, wastani umekua shilingi 2,172 kwa dola moja mwezi Januari, 2016, Julai zikawa shilingi 2,180 na bado mapaka Septemba bado tuko 2,188, kwa hiyo, stability ya exchange rates siyo mbaya kama watu wanavyosema maneno.
Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa mwenendo wa bajeti, na hizi namba nitakazo sema ni preliminary. Mapato ya ndani kwa quarter iliyopita, mapato ya ndani ukijumlisha na fedha kutoka own sources za Halmashauri tulikuwa na shilingi bilioni 3,948.4 Mapato ya ndani ukitoa yale ya Halmashauri inakuwa ni shilingi bilioni 3,814.4, tulipata GBS grant kutoka EU shilingi bilioni 36.1 na kwa upande wa matumizi Waheshimiwa Wabunge tumekwenda vizuri. Matumizi ya kwaida katika quarter ya kwanza, fedha zilizotolewa kwa robo ya kwanza ni asilimia 26.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumetoa shilingi trilioni 4.5 wakati bajeti ya matumizi ya kwaida kwa mwaka huu mzima ni trilioni 17.7 lakini pia kwa upande wa matumizi ya maendeleo hapa tuna changamoto, tunazikiri lakini mwaka ndiyo umeanza quarter ya kwanza ina changamoto mwezi wa kwanza mapato yanakuwa kidogo, mwezi wa 9 ndipo mapato kidogo yana-pick up.
Mheshimiwa Naibu Spika, matumizi ya maendeleo. Tumesha kutoa shilingi bilioni 915 ambayo ni asilimia nane ya lengo ambalo tulikuwa tumekusudia. Kwa upande wa matumizi kutokana na fedha za nje, na hapa ndipo challenge ilipo, ni asilimia moja tu ambazo tumeweza kutoa, tulikuwa tumepata shilingi bilioni 45.9
Mheshimiwa Naibu Spika, ulipaji wa madeni ya ndani. Katika kipindi cha Julai mpaka Oktoba, 2016 tumelipa madeni mbalimbali ambayo yamehakikiwa na Mkaguzi wa Mkuu Ndani wa Serikali, tumelipa jumla ya shilingi bilioni 187.5 na haya yanajumuisha madeni ya wakandarasi wa barabara, maji, umeme, wazabuni mbalimbali na madeni ya watumishi wa umma na tunaendelea kulipa kupitia mafungu yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ulipaji wa deni la nje. Kuanzia Novemba, 2015 hadi Oktoba mwaka huu, Serikali imetumia jumla ya shilingi trilioni 1.19 kwa ajili ya kulipia madeni ya nje. Malipo ya mtaji ni shilingi bilioni 709, malipo ya riba shilingi bilioni 487.2.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hivi; Serikali itaendelea kulipa kwa wakati mikopo yote iliyoiva kwa mujibu wa mikataba; kwa kuwa kama hatufanyi hivyo tutahatarisha mahusiano yaliyopo baina ya nchi zetu na wahisani na taasisi za fedha za kimataifa na mabenki ya nje. Aidha, nchi isipolipa kwa wakati inaweza kushitakiwa kwenye Mahakama za Kimataifa na kusababishia nchi yetu kupata hasara na pengine hata tukakosa kabisa mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutolipa kwa wakati kutaisababishia nchi yetu kulipa gharama kubwa za ziada (penalty) kulingana na makubaliano kwa hiyo ni lazima tulipe. Serikali imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha kwamba Deni la Taifa linadhibitiwa na linaendelea kuwa himilivu na linalipwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ruzuku ya pembejeo. Mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi bilioni 25 zilitengwa kwa ajili ya kununua Pembejeo. Hadi kufikia Oktoba tumekwisha kulipa shilingi bilioni 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, ununuzi wa chakula cha hifadhi. Mwaka huu wa fedha tulitenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kununua chakula cha hifadhi ya Taifa. Mpaka kufikia Oktoba mwaka huu tumekwishakutoa shilingi bilioni 9.
Mheshimiwa Naibu Spika, utoaji wa fedha za Mfuko wa Jimbo. Serikali ilitenga shilingi bilioni 10.4 kwa ajili ya mfuko wa kuchochea maendeleo jimboni. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni tisa ni kwa ajili ya Tanzania Bara na shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Serikali inatarajia kutoa fedha hizo mwezi huu wa Novemba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yamekuwepo kama nilivyosema manung’uniko mitaani lakini sisi tunavyoyatafsiri ni kwamba yametokana na jitihada na hatua zilizochukuliwa na Serikali kurudisha nchi kwenye utaratibu na nidhamu ya kazi katika utumishi wa umma, kurejesha nidhamu ya matumizi, kuondoa matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima, kupambana na wizi na ubadhirifu wa fedha na mali ya umma, kuhimiza ulipaji kodi na ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali inaamini kuwa hatua hizi ni kwa maslahi mapana ya Taifa letu, na maumivu ni ya kipindi cha mpito wakati tunaweka mambo sawa ili tuweze kurudisha mifumo kwenye utaratibu unaokubalika na ambao ni endelevu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, naomba nitumie usemi tena wa kiingereza; there is no gain without pain. Maendeleo hayatakuja hivi hivi, we have to sacrifice ndugu zangu. Lazima tu- sacrifice kama kweli tunataka vizazi vijavyo viweze ku-enjoy maisha in the future, lakini kama tunakula tu leo haiwezekani tutaendelea kubaki maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, upo utaratibu wa Serikali yenyewe, taasisi binafsi na mashirika ya kimataifa kufanya tathmini huru ya uchumi wa nchi na kutoa maoni juu yake kadri wanavyoona. IMF walikuwa hapa wiki moja iliyopita na wamekamilisha tathmini ya mwenendo wa uchumi wetu. Taarifa iko kwenye mtandao, someni. Wamesema wenyewe si maneno yangu wamesema kabisa wameridhika na hali ya uchumi wa Taifa letu lakini hii haina maana kwamba hatuna changamoto, haitawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kidogo kuhusu misingi ya mpango. Niliambiwa hapa kwamba tulivyoiweka hapa inajenga mazingira ya kushindwa tayari. Mimi nafikiri hapa tatizo lilikuwa dogo tu, neno misingi ambalo tulilitumia katika kitabu cha mapendekezo ya mpango kililenga kumaanisha assumptions. Hakika Serikali ya Awamu ya Tano tunafahamu vizuri hali halisi ya mazingira wezeshi kwa uwekezaji nchini kama ambavyo imetathminiwa na Benki ya Dunia katika Doing Business Report. Tunafahamu utabiri wa hali ya hewa na maoteo ya upungufu wa chakula katika nchi yetu, we are not naïve Waheshimiwa Wabunge, we are not naïve at all.
Mheshimiwa Naibu Spika, assumptions huwa tunazifanya na si lazima ziwe halisi, huwa tunazifanya ili kurahisisha uwekaji wa malengo kwa mwaka ujao wa fedha. Wachumi wanafahamu na ni utaratibu wa kwaida kabisa. Kwa mfano; unapotaka kuchambua biashara baina ya nchi mbalimbali ulimwenguni huwa unafanya assumtions unasema assume there only two trading nations, lakini kila mtu anajua nchi mbili duniani hazi-trade peke yake, kwa hiyo, nadhani hili lilikuwa ni suala la lugha tu, tafsiri yetu pengine assumptions haikuwa sahihi, lakini maana yetu ilikuwa ni assumptions na siyo hicho ambacho kilielezwa humu ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha kutopelekwa kwenye Halmashauri. Naomba niseme tu kwamba katika kipindi cha Julai mpaka Oktoba fedha zilizotolewa zinajumuisha mishahara shilingi trilioni 1.18 sawa na asilimia 33. Matumizi mengineyo shilingi bilioni 192.8 ambayo ni sawa na asilimia 32.2 na fedha za maendeleo shilingi bilioni 173.3 sawa na asilimia 14.3. Lakini mbali na fedha za ruzuku kutoka Serikali Kuu na makusanyo ya ndani ya halmashauri, kiasi cha shilingi bilioni 271 zilizotumika kutekeleza miradi ya maji vijijini ni shilingi bilioni 51.1, umeme vijijini shilingi bilioni 132.4, mfuko wa barabara shilingi bilioni 78.1 na utoaji wa pembejeo kwa wakulima shilingi bilioni 10 katika Halmashauri mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa taasisi za umma kuweka fedha zao kwenye revenue account Benki Kuu tulishauriwa hapa kwamba sasa zirejeshwe. Nafikiri limeelezwa vizuri, naomba niseme tu hivi; uamuzi wa Serikali wa kuzitaka taasisi za umma kufungua account za mapato Benki Kuu utaendelea kubaki kama ulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge tumepigwa sana, kwanini tuendelee kupigwa? Utaratibu ambao ulikuwa umejengeka ulizinufaisha benki chache na haukuwa na maslahi mapana kwa Taifa. Benki hizo zimekuwa zikipata faida kwa kutumia mgongo wa maskini na sasa basi. Naibu Waziri amesema hapa waende na vijijini wakafanye kazi huko ili turejeshe ushindani katika sekta ya benki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba TRA wanatumia vitisho, mabavu na mifumo kandamizi katika kukusanya kodi. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inaendelea na jitihada za kuhakikisha kila anayestahili kulipa kodi analipa kodi stahili na kwa wakati. TRA inatekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi kulingana na taratibu katika sheria na kanuni za kodi. Mlipa kodi anakadiriwa kulipa na kupewa muda wa kuilipa kodi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kodi hiyo itakuwa haijalipwa kwa muda uliyooneshwa kwenye taarifa ya madai, TRA huchukua jukumu la kumkumbusha mhusika anapewa reminder notice na kumtahadharisha hatua zitakazochukuliwa endapo kodi hiyo itaendelea kutolipwa mpaka tarehe iliyoonyeshwa kwenye reminder notice.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zinazochukuliwa kwa mlipa kodi anaekaidi ndizo hizo za kukamata mali na kuziuza kwa njia ya mnada na kuiagiza benki ya mlipa kodi kuhamisha fedha kutoka kwenye account yake kwenda TRA kulipia hilo deni. Hatua hizi zipo kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge. Hatua hizi si vitisho wala mabavu, wala mifumo kandamizi kwa wafanyabiashara. Ninawasihi sana ni vizuri walipa kodi wakazingatia sheria za kulipa kodi kwa hiari na kuepuka usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja hapa kwamba Serikali imeokoa fedha kuondoa watumishi hewa lakini wakati huo huo tarifa za Benki Kuu zinaonesha malipo ya mishahara yaliongezeka. Naomba niseme hivi Waheshimiwa Wabunge, Serikali imeendelea kuajiri watumishi kwa mahitaji muhimu. Kati ya mwezi Machi na Septemba, 2016 wameajiriwa watumishi 8,908 wakiwemo wa vyombo vya ulinzi na usalama, walimu wa vyuo vikuu, watumishi wa kada za afya kwa ajili ya hospitali mpya ya Mloganzila na watumishi wa kada nyingine ambao mishahara yao imeongeza wage bill kwa kiasi cha shilingi bilioni 5.08.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizi Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madeni ya watumishi. Kati ya mwezi Machi na Julai, 2016 shilingi bilioni 11.9 zililipwa kwa watumishi 13,544. Lakini pia Serikali iliamua kujumuisha mishahara yote iliyokuwa inalipwa nje ya pay roll kupitia bajeti ya matumizi (OC) kwenye wage bill ya kila mwezi na hivyo kupelekea ongezeko la shilingi bilioni 33.1 kwa mwezi kwenye wage bill kuanzia mwezi Februari. Kwa hiyo, kwa kweli hizi takwimu hizi zinahitaji tu maelezo lakini kila kitu kipo. Nimesikia kengele imeshalia na kama ambavyo nimekwisha kuahidi ziko hoja nyingi ambazo ningependa kuzitolea maelezo lakini inatosha tu niseme na nimalizie na mambo mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, vipaumbele vingi. Nimemsikia Mheshimiwa Silinde. Nafikiri tutakapoanza hilo zoezi la kupunguza vipaumbele tutaanza kupunguza na kuondoa miradi katika jimbo la Momba ili ibaki mitatu. Waheshimiwa Wabunge, kazi ya kupunguza vipaumbele katika Taifa letu ni ngumu sana kwa sababu moja; lengo ni kuielekeza sekta binafsi kwenye maeneo ya priority, kwahiyo si kwamba hizi priorities zote ni Serikali iende ikafanye. Lengo letu ni kuielekeza private sector iende kwente priority areas.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile vipaumbele lazima viwe vingi kwasababu fursa katika Taifa letu zinatofautiana sana, kwahiyo ni lazima miradi iwepo ambayo inazingatia fursa za maeneo husika ndiyo maana ni baadhi tu ya sababu kwanini vipengele ni vingi sana. Lakini kimsingi na umaskini wetu jamani niambieni niache nini, niache reli ya kati, niache miradi ya maji, niache Mchuchuma na Liganga, niache zahanati, niache umeme vijijini au niache barabara? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihitimishe na napenda kuwashukuru Wabunge wote waliochangia na kutupatia ushauri kuhusu vipaumbele na mambo muhimu ambayo sasa tunakwenda kuzingatia katika kazi inayofuata ya kuandaa mpango ujao wa maendeleo kwa mwaka 2017/2018. Napenda niliahidi Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itazingatia ushauri tulipokea kwa kadri inavyowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hakika haitawezekana kuzingatia kila kitu kinachosemwa hapa. Baadhi yataendelea kuzingatiwa katika mipango ya maendeleo itakayofuata. Na ili Bunge lione wazi kwamba Serikali inasikia na inathamini ushauri mzuri walioutoa ninakusudia kuweka bayana katika kitabu cha mpango wa maendeleo ujao utakapokamilika muhtasari wa ushauri uliozingatiwa na ule ambao tunaona unafaa uzingatiwe katika mipango inayofuata na mambo ambayo bado yanahitaji kuchambuliwa kwa kina kabla ya kuzingatiwa kwenye mipango. Kwa hiyo, ninawaahidi ili msiseme tunapuuza, tunazingatia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga Tanzania mpya ili kuwaondoa Watanzania kwenye lindi la umaskini kwa haraka. Uamuzi huu unahitaji kuachana na mazoea, unahitaji sacrifice, unahitaji tufanye kazi kwa bidii, unahitaji nidhamu na uadilifu. Tunataka uchumi ambao Wananchi wengi wananufaika nao. Nirudie tena, Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli inawajali wafanyabiashara, lakini hatuna budi wafanyabiashara wetu wazingatie sheria za nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.