Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru Mungu kwa kuniruhusu kusimama hapa ili kuhitimisha mjadala wa Bunge lako Tukufu kuhusu Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 niliyoyawasilisha tarehe 8 Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nakupongeza sana kwa umahiri na weledi wa hali ya juu ulioonesha katika kusimamia Kanuni za Bunge wakati wote wa kikao hiki cha Bunge la Bajeti. Hakika viwango vyako ni vya kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa Mheshimiwa Kakunda, mwanafunzi wangu wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alichomekea sehemu fulani akidai kwamba mimi ni bahiri. Nadhani alimaanisha kwamba ni bahari wa kutoa maksi za upendeleo. Nataka niliambie Bunge lako Tukufu kwamba viwango vyako Mheshimiwa Naibu Spika ambavyo umevionyesha humu ndani hakika ningekuwa bado niko kule chuoni ningekupatia maksi za haki, asilimia 100 kama walivyofanya Maprofesa wako wa Sheria pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam lakini pia University of Cape town, hongera sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutambua michango iliyotolewa na Kamati ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini. Japokuwa ameingia mitini, napenda pia kutambua mchango wa Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, Naibu Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Wizara ya Fedha na Mipango lakini pia michango ya Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza au kwa maandishi hapa Bungeni, nawashukuru wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya Wabunge 171 wamechangia hoja niliyowasilisha. Kati ya hao, 146 wamechangia kwa kuzungumza na 25 kwa maandishi. Napenda kuwashukuru wote. Pia niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri tisa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliochangia asubuhi hii. Kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Dokta Ashatu Kachwamba Kijaji kwa kunisaidia kujibu hoja kwa umahiri mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na hatua ambazo zilipongezwa na Wabunge wengi wakati wa mjadala huu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017. Moja ambalo Waheshimiwa Wabunge mlilisema na kulipongeza ni Serikali kuthubutu kuweka lengo la bajeti ya shilingi trilioni 29.5 ikilinganishwa na shilingi trilioni 22.5 mwaka huu fedha tunaomalizia na kati ya hizo kutenga asilimia 40 ya bajeti yote kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo. Miradi hii ya maendeleo ni pamoja na uthubutu wa kuanza kujenga reli mpya ya kati kwa kiwango cha standard gauge, barabara, umeme, ununuzi wa meli mpya na ndege tatu za abiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Waheshimiwa Wabunge walipongeza sana uamuzi wa Serikali kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi na hadi sasa tumefikia wastani wa shilingi trilioni 1.2 kwa mwezi kwa kuziba mianya ya uvujaji wa mapato na kuimarisha matumizi ya vifaa vya kieletroniki (EFDs). Pia Waheshimiwa Wabunge walipongeza uamuzi wa Serikali wa kusimamia nidhamu ya matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza fedha hizo kwenye miradi ya maendeleo. Pamoja na mambo mengine Waheshimiwa Wabunge wamepongeza azma ya kufanya kazi na kurejesha nidhamu ya watumishi kazini kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo mengine mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge walipongeza. Napenda nimalizie tu na moja la mwisho ambalo ni azma ya Serikali kujielekeza kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015, ahadi za Viongozi Wakuu na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2020-2025 ili kutatua kero za wananchi hasa masikini.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Waheshimiwa Wabunge walitoa ushauri katika maeneo mbalimbali, nitazungumzia machache. Moja, Waheshimiwa Wabunge wameshauri kuongeza tozo ya mafuta ili mapato hayo yatumike kupanua huduma za maji na kukamilisha vituo vya afya na zahanati vijiji. Pia walishauri kwamba mfumo wa kodi uboreshwe ikiwa ni pamoja na kufuta kodi zaidi, ushuru na tozo za kero kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara hasa wadogo. Pia kutoa ahueni ya kodi kwenye taulo za akina mama na vifaa vya watu wenye ulemavu, vifaa vya michezo, zana za uvuvi na kulinda viwanda vya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge walishauri kwamba ni muhimu kuimarisha elimu na kuhakikisha inaendana na mahitaji na wataalam wa Tanzania ya leo na kesho. Walishauri Serikali ichukue hatua za ziada kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na hususan kuongeza kilimo cha umwagiliaji, pembejeo, ugani, utafiti, mnyororo wa thamani, masoko, ruzuku, mikopo na bajeti ya kilimo. Waheshimiwa Wabunge waliishauri Serikali ipanue wigo wa kodi hasa katika sekta ambazo zina mapato makubwa kama mawasiliano, madini, maliasili na ardhi na sekta zenye fursa kama uvuvi na biashara kwenda nchi jirani lakini pia e-commerce, gawio kutoka kwenye mashirika ya umma na kuhakikisha kila mwananachi analipa kodi stahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri uliotolewa ni mwingi sana na mzuri na Serikali itauzingatia katika bajeti hii na bajeti zinazokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nianze kufafanua baadhi ya hoja na kama nilivyosema michango ilikuwa mingi haitakuwa rahisi kujibu hoja zote pamoja na zile zilizojibiwa na Waheshimiwa Mawaziri, nitajibu chache tu. Najua hoja hizi nyingine zilielezwa kwa hisia kali na wengine walinikaribisha Bungeni wakisema Waziri wa Fedha na Mipango amewa-beep Waheshimiwa Wabunge na wengine walisema Waziri wa Fedha hana jimbo ndiyo maana haoni machungu. Mimi nadhani walikuwa wananikaribisha tu Bungeni, kazi ya Waziri wa Fedha ina changamoto nyingi, inanilazimu niwe mtu ambaye hana maneno matamu tu lakini matupu, inanilazimu niwe mkweli na kuwaeleza kile ambacho kinawezekana na kile kisichowezekana ili kujenga nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja moja ambayo ilisemwa sana ni pendekezo la kuongeza tozo ya Sh.50 kwenye mafuta kwa ajili ya kutunisha Mfuko wa Maji na kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vijijini. Niseme tu kwamba hili ni pendekezo ambalo lina lengo zuri na Serikali inalipokea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ni vyema kutambua kwamba kufuatia kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia gharama ya mafuta yote ambayo tumeagiza kama taifa kutoka nje imepungua kwa takribani asilimia 20 na imechangia kushuka kwa mfumuko wa bei na sasa mfumuko wa bei uko asilimia 5.2 na mwenendo huu umeleta ahueni kwa maisha ya wananchi wetu walio wengi. Hata hivyo, Serikali imeamua kwamba kwa wakati huu hatutaongeza tozo kwenye mafuta ili wananchi waendelee kunufaika na huo unafuu wa bei ya mafuta. Ni wazi kwamba ongezeko la tozo katika mafuta ya petroli na dizeli litasababisha kupanda kwa bei ya mafuta jambo ambalo litaongeza gharama ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa chakula na bidhaa ikiwa ni pamoja na vifaa vya ujenzi na huduma nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwaambie Waheshimiwa Wabunge pia kwamba wataalam wa uchumi wanashauri kwamba katika kipindi ambacho kuna uwepo wa bei ndogo ya mafuta, ni wakati mzuri kwa nchi kuwekeza hususan katika miundombinu, viwanda ambavyo ni energy intensive na kuendeleza ujuzi na teknolojia. Kwa hiyo, ndiyo sababu Serikali inaona kwamba ni busara zaidi badala ya kuongeza tozo kwenye mafuta tujielekeze kuongeza bajeti ya kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya usafirishaji, nishati na elimu sambamba na kutumia pesa zilizopangwa kwa ufanisi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa huduma ya maji nchini ambayo pia ni Ilani ya CCM, tuliongeza bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Maji kutoka shilingi bilioni 373 hadi shilingi bilioni 690.16 kwa mwaka ujao wa fedha. Kwa hiyo, kama Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI alivyoeleza, Serikali inapenda itumie mwaka huu kujipanga na kujua majengo ya afya ambayo yamekwama kwa mwaka huu ili utekelezaji uanze ukiwa umepangwa vizuri mwaka 2017/2018. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni pendekezo la kuondoa msamaha wa kodi ya mapato kwenye kiinua mgongo cha Waheshimiwa Wabunge. Kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332, kodi ya mapato inatozwa kwenye vyanzo vyote vya mapato na kiinua mgongo ni chanzo kimojawapo cha mapato kinachotambuliwa na sheria na hutozwa kodi. Kupitia Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi ya Mapato kiinua mgongo kinacholipwa kwa Wabunge wakati wanapomaliza muhula wa miaka mitano kimesamehewa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, msamaha huu hauzingatii usawa wa utozwaji kodi kwani watu wengine wote wanaopata malipo ya kiinua mgongo, iwe ni sekta binafsi au utumishi wa umma wanatozwa kodi katika mapato hayo. Kwa hiyo, hatua niliyoitangaza tarehe 8 Juni, 2016 imechukuliwa ili kujenga msingi wa usawa na haki katika ulipaji wa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kufanya marekebisho hayo hivi sasa ni kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kisheria utakaotumika kukokotoa stahili za Mbunge endapo ukomo wa Mbunge yeyote utatokea katika kipindi cha kuanzia sasa (Julai 2016) na kuendelea. Pia mabadiliko haya yanafanyika sasa ili kuzingatia msingi wa utozaji kodi ambao unataka kodi iwe inatabirika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliarifu Bunge lako Tukufu na wananchi wa Tanzania kwamba siku nilipowasilisha pendekezo hili la kufuta msamaha wa kodi kwenye kiinua mgongo cha Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza alinishangaa akasema yeye ni Mtanzania na ni lazima Watanzania wote walipe kodi ili kuijenga nchi yetu. Kwa kuwa kiongozi lazima aongoze kwa mfano, Mheshimiwa Rais alielekeza kuwa yeye ni Mbunge wa Tanzania yote na anapenda awe wa kwanza kukatwa kodi stahiki kwenye mafao yake ya kustaafu. Naomba nirudie, alielekeza kuwa yeye ni Mbunge wa Tanzania nzima na anapenda awe wa kwanza kukatwa kodi yake stahiki kwenye mafao yake ya kustaafu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kufafanua kwamba marekebisho niliyowasilisha tarehe 8, Juni, 2016 maana yake ni kuwa kiinua mgongo cha viongozi wote wa kisiasa ambao wametajwa kusamehewa kodi chini ya Sheria ya Mafao ya Viongozi wa Kisiasa sasa kitakatwa kodi. Maana yake ni kwamba Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, kiinua mgongo chake kitakatwa kodi. Mheshimiwa Waziri Mkuu, yeye ni Mbunge wa Ruangwa, kiinua mgongo chake kitakatwa kodi. Mheshimiwa Naibu Spika na wewe kiinua mgongo chako kitakatwa kodi. Waheshimiwa Mawaziri, Naibu Mawaziri, sisi wote ni Wabunge, lazima tuongoze kwa mfano, kiinua mgongo chetu kitakatwa kodi. Vivyo hivyo kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya, kiinua mgongo chao kitakatwa kodi. Waheshimiwa Wabunge, hii ndiyo dhamana ya uongozi, we have to lead by example. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, palikuwepo hoja ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kwamba imetengewa fedha kidogo na haitaweza kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Wengine walizungumza kwa lugha kali kidogo kwamba Waziri wa Fedha na Mipango ana dhamira gani na CAG, je, CAG ni adui wa Serikali, la hasha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukomo wa bajeti ya OC ilitengwa kwa mafungu mbalimbali kwa kuzingatia maamuzi ya Serikali na mkakati wa kupunguza matumizi ya kawaida ili tuelekeze fedha nyingi zaidi kwenye miradi ya maendeleo. Katika kufikia ukomo wa matumizi mengine kwa Serikali nzima, uchambuzi wa kina ulifanyika ili kubaini mahitaji ya fedha ambayo siyo ya lazima kwa wakati huu na hayawezi kuathiri utendaji. Kwa hiyo, tulitazama yote hayo na fedha ambayo tumeweza kutenga kwa sasa ndiyo hiyo na tuna hakika kabisa kwamba Ofisi ya CAG itaendelea kufanya kazi yake ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua umuhimu wa majukumu ya msingi ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi na kama ilivyo kwa taasisi nyingine nyeti ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, mihimili mingine ya dola na uwezo wa kukabiliana na dharura, kama patajitokeza mahitaji ya lazima, napenda tena kusisitiza mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba tutahakikisha kwamba ofisi hiyo haikwami. Mahitaji hayo ya ziada yatazingatiwa wakati wa mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uhuru wa CAG katika kufanya kazi zake ni wa kikatiba na hautaingiliwa. Waziri wa Fedha na Mipango atakuwa mtu wa mwisho kukwamisha kazi za ofisi hiyo ambayo inamsaidia kufichua mchwa wa fedha za umma kwenye Wizara na halmashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya tathmini ya hali ya umaskini kimkoa. Naomba tu niseme kwamba viashiria vya kupima umaskini nchini huwa vinapatikana kwa kutumia utafiti wa mapato na matumizi ya kaya ambao unafanyika katika nchi yetu kila baada ya miaka mitano. Utafiti huo kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2011/2012. Utafiti huo ukichanganya na taarifa zinazotokana na sensa iliyofanyika mwaka 2012 ndiyo unatuwezesha kuweza kuchambua hali ya umaskini wa kila mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba sababu ambazo zinaeleza kwa nini kiwango cha umaskini katika Mikoa kama Mwanza, Kigoma, Singida, Geita na Kagera ni kikubwa ukilinganisha na Mikoa kama Lindi na Mtwara ni nyingi. Kwanza kwa ujumla umaskini wa kipato ni mkubwa zaidi pale ambapo kuna wananchi wengi zaidi wanaishi vijijini ukilinganisha na mijini. Kwa mfano ukiangalia Mkoa wa Mwanza, mwaka 2000/2001 wakati bado Geita iko humo kiwango cha umaskini kilikuwa ni asilimia 48. Umaskini wa kipato wa Geita kabla ya kugawanywa ulikuwa ni asilimia 62.3 lakini baada ya kutenganishwa kiwango cha umaskini wa kipato katika Mkoa wa Mwanza unateremka lakini kiwango cha umaskini katika Mkoa wa Geita kinaendelea kubakia juu na sababu kubwa ni kwamba wananchi wengi zaidi wa Geita wanaishi vijijini ambapo shughuli zao za uzalishaji mali hazikidhi kupunguza kiwango cha umaskini kwa kasi inayotarajiwa. Ukiangalia wilaya ambazo ziko karibu na miji, kiwango cha umaskini ni kidogo zaidi kuliko kiwango cha umaskini katika maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, umaskini pia ni lazima uende na hali ya kimaeneo. Kwa mfano, Mkoa wa Kigoma kwa kiasi kikubwa umaskini wa kipato katika mkoa huu unachangiwa na miundombinu hafifu ya usafirishaji ambayo inapunguza fursa ya kufikia masoko. Kigoma pia inabeba mzigo mkubwa sana wa wakimbizi na kusababisha ziada ambayo inazalishwa kutumika kulisha wakimbizi na kupunguza ustawi wa kaya katika mkoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama ni mkakati, cha kwanza ni kutambua kwamba kuna hilo tatizo na sababu zake lakini pia kujielekeza sasa kufungua fursa katika mikoa na wilaya husika. Pia kuja na interventions kama zile za TASAF ambazo zinalenga kusaidia kaya maskini kabisa lakini pia miradi ya afya na maji na pia specific interventions ambazo zinakwenda kushughulikia matatizo katika maeneo mahsusi kama vile tatizo la mnyauko wa migomba kule Kagera na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema tutawasilisha maelezo ya kina kwa maandishi kwa hoja zote ambazo Waheshimiwa Wabunge walizitoa. Naomba nieleze moja kabla ya kuhitimisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ililetwa hoja hapa kwamba dollarization imekuwa ni kero kubwa na inasababisha thamani ya shilingi kuteremka. Naomba tu niseme dollarization ni matumizi ya sarafu ya kigeni katika nchi husika sambamba na sarafu ya nchi hiyo. Dollarization kitaalam inachochewa na vitu kadhaa hususan mfumuko wa bei kama ni mkubwa lakini pia kama thamani ya sarafu ya nchi husika nayo inateremka lakini katika nchi ambazo hakuna usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Tanzania sababu kubwa ni kwamba tumekuwa na mapato kidogo ya fedha za kigeni lakini pia dola imeongezeka sana nguvu kutokana na kuongezeka kwa uchumi wa Marekani na kuchelewa kupata misaada ya general budget support. Kwa kawaida wananchi wanatumia hiyo sarafu ya kigeni ili kujikinga na athari za mfumuko wa bei yaani they hedge against the inflation risk. Mazingira mengine ambayo yanachochea dollarization kama nilivyosema ni kukosekana utulivu wa kisiasa ambayo sisi bahati nzuri hatuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa hili tatizo linahitaji muda na ukichukua hatua za kiamri, za kiutawala kusema tu sasa kuanzia leo watu wasitumie dola, uzoefu wa nchi mbalimbali ulimwenguni unaonesha kwamba hizo sera hazifanyi kazi. Utatia woga katika uchumi na watu wataanza kukimbiza fedha za kigeni na kuleta matokeo yasiyotarajiwa. Kwa hiyo, mkakati siyo kulazimisha au kudhibiti matumizi ya hizo dola, inatakiwa iende sambamba na sera za kisoko za kudhibiti tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa watu ambao wanapenda kusoma wanaweza wakatafuta jarida linapatikana kwenye internet „Dollarization in Sub-Saharan Africa: Experience and Lessons 2015‟, inawaonesha experience ya nchi nyingine na hatua ambazo walichukua hazikufanikiwa. Kwa hiyo, tunachukua kila tahadhari kuhakikisha tunaendelea kubakia na uchumi wetu tulivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwasihi Waheshimiwa Wabunge, kwamba bajeti niliyowasilisha inajielekeza kuanza kazi ngumu ya kuitoa Tanzania kutoka nchi inayotegemea kilimo duni kuwa nchi ya uchumi wa viwanda, nchi ambayo wananchi wake wameondoka kwenye lindi la umaskini ili twende mbele. Kwa hiyo, yote tunayopanga, katika mipango na bajeti ya Serikali, ni muhimu sana kutanguliza maslahi ya Taifa letu lakini pia maslahi ya Watanzania maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Bunge lako Tukufu kuikubali bajeti hii, utekelezaji wake utahitaji kujitoa. Mheshimiwa Makamba amesema tutahitaji sacrifice, tutahitaji selfless service to our country. Tunahitaji kuvuja jasho ili tuweze kuwainua maskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mambo mawili tunaweza kufanya, tunaweza tukaamua kuendelea na mazoea yaani business as usual ambayo siyo option kwetu lakini njia sahihi ni kuachana na mazoea. Ili kuachana na mazoea lazima tuanze sisi viongozi. Itatubidi tuachane na maslahi binafsi hata kama mara kadhaa inaonekana tunayavisha koti au kilemba cha maslahi ya wengi.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nilikuwa nasema tuna dhamana kubwa ya kuleta mabadiliko makubwa katika kuendesha shughuli zote za umma na matumizi ya rasilimali za Taifa ili tuweze kupiga hatua kubwa za kuitoa nchi yetu katika umaskini. Ni lazima kila mwananchi atambue wajibu wake wa kufanya kazi kwa bidii, kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika nyanja zote na uzalendo kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kuzielekeza Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuzingatia hatua za kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kusimamia matumizi ya Serikali na hatua za kupunguza gharama na kulipa na kuzuia ongezeko la madeni ya Serikali. Serikali ina dhamira ya dhati ya kuchukua hatua hizo na naomba Watanzania watambue kwamba ni lazima kujinyima, kujituma na kuvuja jasho ili kupata maendeleo na kupunguza utegemezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena, wajibu wa kwanza wa kuiendeleza nchi yetu ni ya sisi Watanzania wenyewe, tunazo akili za kutosha na rasilimali nyingi na fursa tele kuweza kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na ya uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Nawaomba tena Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono hatua zinazoongozwa na Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kuwa tunaimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, mapato ya kodi na yasiyo ya kodi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo yenye tija na hususani ujenzi wa viwanda kwa manufaa ya Watanzania wote.