Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii mimi yangu ni machache, ninakuja kuwaeleza kwamba tunakwenda kwenye kujenga uchumi wa viwanda na nakuja kuwahakikishia kwamba uwezo wa kujenga uchumi wa viwanda tunao, na sekta itakayoongoza ujenzi wa uchumi wa viwanda mhimili wetu ni sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda mbele nichukue fursa hii kwako wewe binafsi, Waheshimiwa Wabunge niwakaribishe kwenye maeneo ya 40 kwenye Saba Saba Mwalimu Nyerere Dar es Salaam International Trade Fair ya 40 itafanyika kuanzia tarehe 1; karibuni nyote mtaingia na VIP pass. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie pale alipoishia Mheshimiwa Makamba. Dhamana niliyopewa ni kuhakikisha kwamba kunakuwepo wepesi wa kufanya shughuli, ni wepesi wa kufanya biashara jambo ambalo ninalisimamia mimi litakalowawezesha wawekezaji kuja hapa, mengine yote yatafuata baadaye. Ikitokea hakuna wepesi wa kufanya biashara mimi nitalaumiwa lakini mimi ndiyo mdogo nitawakumbusha Mawaziri wote kwamba wawekezaji wote tuwape wepesi wa kufanya biashara, mengine ya kodi yanafuata baadaye, kinachotangulia ni wepesi wa kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la mitumba ambalo mama yangu alilizungumza, hatuna dhamira ya kuwafanya Watanzania watembee uchi, tunajenga uchumi wa viwanda, viwanda vyangu vya nguo ambavyo vinazalisha 40% viende kwenye 100% na tunatengeneza nguo kusudi watu wavae na tunaanza kuwavika watoto wa nyumbani kabla ya kuuza nje. Kwa hiyo, kama tunawavika watoto wa nyumbani hawawezi kuvaa mitumba msiwaombee Watanzania kuvaa mitumba, kwa nini tumeongeza tozo kwenye mitumba, tumeongeza tozo kwenye mitumba tunawa-beep wenye viwanda kwamba sasa tunawalinda, zalisha nguo nzuri, watu wetu wavae na mitumba itapigwa marufuku yenyewe katika miaka mitatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie mafuta ya kula. Sekta ya mafuta ya kula (the edible oil), mbegu zinazotengeneza mafuta ya kula ukianzia migaze, ukaja karanga, alizeti zinaajiri watu milioni 1.5 lakini Tanzania tunahitaji laki nne mafuta ya kula, sasa mafuta yanalimwa nchini hayafiki 70,000, kiburi chetu ni kwamba tujenge ujasiri wazalishe kiasi hiki kama 70,000, zinatengeneza ajira milioni 1.5 laki nne itatengeneza kiasi gani ndipo mimi nitakpopata ajira ya Watanzania, wenye viwanda vya mafuta Tanzania msikate tamaa, najua wasiwasi wenu ni kwamba mafuta kutoka Kenya na Uganda yatakuwa na advantage kwa sababu kwao yanaingia kwa sifuri, ngoja niwaeleze.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu tarehe 1 Julai, mafuta yatakayoingia Tanzania ambayo hayakupitia kwenye viwanda vya Watanzania wale watatu yatalipishwa asilimia 25 na asilimia 18 nimemwambia Waziri wa Fedha kwamba tuhakikishe mafuta yanayotoka Kenya na Uganda kuingia Tanzania yanalipishwa zaidi kusudi viwanda vya Tanzania viweze kupata advantage. Wenye viwanda nitawalinda, leteni habari kwangu niweze kuwapa wepesi wa kufanya shughuli. Lakini siwafichi nichukue fursa hii kuwapongeza Wabunge wa Kigoma kwa mara ya nne mkiweza kuzalisha migaze kwenye hekari laki moja tutaweza kuzalisha mafuta ya kuweza kutosheleza mafuta yetu. Tunapojenga standard gauge rail kwenda Kigoma maana yake ni nini, treni ikipanda na mizigo ya Congo irudi na mawese kwenye viwanda vya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, limekuwepo swali tata watu wanasema Mwijage umepewa shilingi bilioni 40 utajengaje uchumi wa viwanda? Nitaujenga hivi Jimbo la Jiangsu juzi walikuja kumuona tajiri namba moja, wameahidi kwamba wataleta dola trilioni tano kujenga viwanda, ndiyo maana nachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji ameandamana kuja kwangu na nimemwambia anipe hekta 15,000 nitamletea mtengenezaji wa kiwanda cha sukari kuzalisha tani 150,000. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Makamba, ngoja nikueleze muingie kwenye benzi hii, muingie kwenye treni hii tunaondoka atakayekataa kujiunga na sisi atajuta na kusaga meno. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba bajeti hii ipite, nichukue fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Simbachawene ametoa maelekezo kwenye Wilaya yote na Mikoa kutenga maeneo ya uwekezaji natoa mimi maelekezo kwa wale walio chini yangu SIDO ndiyo itakuwa gateway, na Serikali ya China sisi tuna marafiki zetu bwana, Serikali ya China watatoa dola milioni 100 kusaidia viwanda vidogo zinakuja kwangu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge SIDO ndiyo itakuwa gateway, tutatafuta mbinu zote kuhakikisha tunaweka mazingira wezeshi kusudi Watanzania wote waweze kwenda vizuri.
Niwaeleze moja, pacha yangu amekwenda Mambo ya Ndani, tumedhamiria kwamba kiwanda cha Karanga Prison, tutawapatia vifaa kutoka Wizarani kwangu kupitia TIB watengeneze sole za viatu ili ngozi zinazotengenezwa Tanzania zitengeneze viatu tuanze kuvaa viatu na kabla Bunge lako halijaisha watu wa Karanga Prison, watu wa Imo Tannaries watakuja kuonyesha viatu vinavyozalishwa, viatu vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa uchumi wa viwanda ni lazima tukubali sisi wenyewe kuvaa bidhaa zetu, ukipende chako kabla wenzako hawajakipenda na kama nilivyowaeleza ujenzi wa uchumi wa viwanda ni vita hakuna anayecheka kwenye vita wote tunune tujenga uchumi wa viwanda, tuongeze GDP. Kama alivyosema Profesa Muhongo, GDB ikikua ukigawanya kwa watu wetu unapata dola 3000 kwa kila mtu, ifikapo 2025 Tanzania inakuwa uchumi wa kati, uchumi ambao mambo ya umaskini na ujinga itakuwa ni historia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja.