Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Asha Abdullah Juma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii leo. Pia namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia uzima na afya leo nikapata fursa hii ya kuweza kuchangia katika hotuba hii ya bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya kipekee nasisitiza na nakupongeza na nakuombea dua Mheshimiwa Naibu Spika, Tulia Ackson. Mungu akupe nguvu uendelee kuhudumu katika Bunge hili kwa umahiri kama hivi unavyofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, umesimamia kanuni na taratibu bila kusita, hukubagua kama huyu mtu katoka chama gani wala nini. Mimi binafsi siku moja nilikatisha hapo ndivyo sivyo, ulivyomaliza kikao tu ukatoa mwongozo kwamba, siyo ruhusa kukatisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande mwingine nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wetu wa Fedha ambaye anapanga na anajua kupanga. Wizara hii amepewa kusudi kwa kuwa anajulikana anaimudu, uchumi wake unaonekana hapa na nimtie nguvu. Watu wengi humwita kaka yao, mdogo wao, sijui nani wao, mimi ni shemeji yangu na namwamini sana. Najua ataupeleka uchumi wetu kule tunakotaka kwenda kwenye uchumi wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa baada ya pongezi hizo na kutia nguvu huko, nianze kuzungumzia utaratibu wa kodi ya ongezeko la thamani. Hapa nataka kuhusisha ile section iliyozungumzia kuhusu bidhaa zitakazotoka kwenda pande mbili za nchi yetu za Muungano yaani Zanzibar na Tanzania Bara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijue tu, je, kodi hii itahusisha vyakula? Nauliza kwa sababu kwenye ukurasa wa 48 wa hotuba, kifungu 67 namba moja mpaka mbili kimeondoa kodi kwa baadhi ya vyakula. Hali halisi ni kwamba Zanzibar inaagiza vyakula na mboga mboga kwa kiasi kikubwa sana. Sasa naendelea kutaka kujua kwa ufafanuzi, vyakula ambavyo havikutajwa kodi yake itakuwaje? Kama kuna uwezekano iandaliwe orodha ya vyakula ambavyo havitatozwa kodi ili kuepusha migongano.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi mwingine juu ya kodi hii inayopendekezwa, kwamba je, pande hizi mbili zote zimeshirikishwa kupanga ili kuepuka kuwapa shida wananchi? Napendekeza pia kabla ya utaratibu huu yafanyike majadiliano ya kina kwa wadau wanaohusika na kwa kujua kiasi gani pande mbili hizi zimekutana na kutafakari mambo hayo ambayo kwa sehemu kubwa yasije yakasababisha kile kilichokuwa kinaitwa kero za muungano. Kwa sababu kwa spirit hiyo hiyo ya kuunganisha na kuboresha udugu wetu baina ya nchi yetu hii, kati yetu, basi ni lazima majadiliano ya kina yafanyike. Natambua kwamba Zanzibar ina bajeti yake na Bara ina bajeti yaken lakini ningeshauri hilo liwepo kwa spirit hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika sasa nataka kugusia uchumi wa viwanda ambalo ndilo tuliloambiwa na tulilotangaza kwenye ilani yetu na Mheshimiwa Rais wetu alisema kwamba Tanzania hii itakuwa kwenye uchumi wa viwanda na huko ndiko tutakopata manufaa. Naomba nijielekeze huko na naomba nilihusishe suala hilo na uwekezaji wa Kiwanda cha Sukari Bagamoyo ambacho kinajulikana kama Basic Bagamoyo Sugar Infrastructure and Sustainable Community Program. Hii ni program ambayo kwa bahati mbaya imepata mkwamo na imeanza siku nyingi sana, lakini ukichunguza kwa kina, mradi huu ni wa kipekee na unaendeshwa na mfadhili na Mwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mipango yote imepangwa. Mradi huu umeanza tangu 2005 na ungekuwa na faida kubwa kwa wananchi wetu kwa ujumla na hasa wananchi wa Bagamoyo. Wafadhili walikuwa tayari na washafanya study zao zote ni African Development Bank na IFAD na Mwekezaji ni ECO-ENERGY. ADB katika mradi huu ilivyojipanga ni kushughulikia miundombinu ya maji kuwafikia wakulima wadogo wadogo pamoja na barabara za mashambani. Pia kujenga bwawa la kuhifadhi maji litakalosaidia maji wakati wa kiangazi na kuzuia mafuriko.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwekezaji huu ambao umepatwa na vigingi vingi ungewasaidia sana. Kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha tani 150,000 za sukari na tunajua sukari ni tatizo na tunajua pia kwamba Kiwanda hiki kinge-take off, kingeweza kuwa na 140,000 CDM za Ethanol na 90,000 megawatts za surplus ya electricity. Kiwanda kitazalisha ajira, na ndicho tunachopigania kwamba vijana wetu wengi hawana ajira; hapa zingetegemewa kupatikana ajira 2,500 hadi 3,000 za moja kwa moja na karibu ajira 13,000. IFAD inasaidia wakulima wadogo wadogo wa miwa na kusaidia vijiji 27 vitakavyozunguka na pia wananchi karibu 91,444 watafaidika na kujiendeleza na ukulima wa kisasa (smart agriculture). Halikadhalika pia wafanyabiashara wadogo wadogo watafaidika.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana kwamba mpango wa awamu ya nne wa BRN ulikusudia kuanzisha viwanda 10 ndani ya maeneo ya corridor ya kusini lakini mpaka sasa bado. Wafadhili wako tayari, gharama, project study zote zimeshafanywa, kitu gani kinachozuia?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kidogo nigusie ile pesa ambazo tunaweza kuzikosa mradi huu ukitutoka. Ni USD milioni 450 kwa ajili ya maandalizi, preparedness, USD milioni 10 kwa uhifadhi wa mazingira za kingo za Mto Ruvu na Wami, USD 350 kwa ajili ya monitoring na evaluation. Sasa sisi tunafikwa na nini? Nafasi hizi na fursa hizi tunazipoteza, wenzetu kwa mfano kule Swaziland wamefadhiliwa na watu hawa hawa, African Development Bank na IFAD na sasa hivi wanazalisha sukari nyingi na wanapata faida kubwa, humo humo wamepata kumwagilia maji, wanapata mahindi ya kutosha, sisi tunakwazwa na nini? Kwa nini fursa tunachelewa kuzishika? Kila kitu bureaucracy.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri afikirie sana tija itakayopatikana katika mradi huu. Inawezekana kuna watu ambao hawataki kwahivyo tutazame kwa kina faida inayopatikana….
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.