Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona. Kwanza kabisa naomba nitoe shukrani za dhati kabisa kwa Mungu wa mbinguni kwa ajili yangu na wengine wote tuliojaliwa kuingia mwaka 2016 na kuletwa humu na wananchi wetu. Zaidi sana nielekeze pia shukrani zangu za dhati kwa Chama cha Mapinduzi ambacho kimenipatia fursa hii ya kuwawakilisha wanawake wa Manyara. Vilevile niwapongeze wanawake wa Manyara kwa kunipatia nafasi hii ili nije niwawakilishe katika Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba nielekeze michango yangu moja kwa moja nikianza na elimu. Naomba ku-declare interest ya kwamba mimi ni mwekezaji wa ndani katika masuala ya elimu, kwa maana ya shule za binafsi. Nipende kuanza kumpongeza sana Mheshimiwa Profesa Ndalichako ambaye ameweza kusikiliza kilio cha Watanzania cha kuondoa GPA na kurudisha mfumo wa division. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichokuwa kinafanyika ni sawa na kuvalisha mtu mchafu gauni la gold. Kwa hiyo, niseme tu Mheshimiwa Profesa Ndalichako na timu yako hongereni sana maana mmedhamiria kuboresha elimu ya nchi yetu Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile hakuna nchi ambayo imewahi kuendelea duniani pasipo kuwekeza kwenye elimu, hata maneno matakatifu yanasema; “Mkamate sana elimu usimwache akaenda zake maana yeye ndio uzima wako.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu, kulingana na Mpango uliopo mbele yetu wa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli imeazimia kuwekeza sana kwenye elimu kwa kuanza kutoa elimu bure, basi nafikiri ni wakati muafaka kuangalia changamoto zinazokabili tasnia ya elimu nchini. Kwa hiyo kwanza kabisa, nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona ya kwamba, potelea mbali vyovyote inavyoitwa ya kwamba ni kupunguza makali kwenye elimu ama ni elimu bure, lakini iwavyo vyovyote ili mradi mtoto wa Kitanzania sasa anakwenda kupata elimu bila vikwazo vya aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwaambie tu ndugu zangu Wapinzani, msibeze kila kitu kinachofanywa na Serikali hii, Serikali inajitahidi sana ninyi si Mungu ama malaika ambapo mngepata nafasi hii kwamba mngeweza kuchange dunia in a day. Kila kitu kinakwenda taratibu, hatua kwa hatua, changamoto zilizopo kwenye elimu bure zinafanyiwa kazi na zinakwenda kwisha. Kwa hiyo, tambueni juhudi za Serikali kwenye hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye mchango wangu wa elimu. Naomba sasa pia Serikali ijitahidi sana kufanya kazi na sekta binafsi maana kuna wadau wengi sana wamewekeza kwenye elimu na ifike mahali watu hawa waonekane kama siyo competitors isipokuwa ni partners wanaoweza kusaidia kusomesha watoto wa Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu wawekezaji wa ndani katika suala la elimu wanakabiliwa na kodi zisizopungua 13, ndiyo maana inaonekana watu hawa wanatoa elimu kwa gharama ya juu sana mpaka mambo ya ada elekezi yanaingia humu. Shule za binafsi zinalipa property tax, income tax, service development levy, city levy, land rent, mabango ya shule yale yaliyo kwenye TANROADS tunalipa kwa dola. Sasa sijui mambo ya dola yanakujaje tena na halafu inaitwa TANROADS halafu tunalipa kwa dola, sasa si tuite tu USROADS. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kodi ya corporate tax, working permits kwa walimu ambao siyo Watanzania. Mwalimu mmoja mpaka uweze kumpata anatumia sio chini ya shilingi milioni saba ndipo aweze kupata working permits na residence permit. Wakati huo huo tuna upungufu wa walimu wasiopungua laki tisa, tulionao ni laki mbili thelathini na nane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna upungufu wa Walimu wa sayansi na hisabati wasiopungua elfu ishirini, Wizara ama nchi ina uwezo wa kutengeneza Walimu wasiozidi elfu mbili kwa mwaka. Kwa hiyo, tunachukua note less than ten years kutengeneza Walimu tunaowahitaji wa sayansi. Hii imekuwa pia changamoto kubwa kwa ajili ya maabara ambazo tumezijenga majuzi kati, tuna maabara kila mahali sasa, lakini changamoto kubwa imebaki kwa Walimu wa masomo ya sayansi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali sasa kama inawezekana Serikali ione umuhimu wa kupunguza gharama za kuwapata Walimu kutoka nchi jirani kwa gharama ndogo residence permit na working permit ili waweze kusaidia katika shule zetu.
MHE. WAITARA M. MWIKABWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kidogo suala la afya. Naomba katika suala la afya kwa sababu Serikali pia imeamua kuwekeza sasa kwenye afya ya wananchi wake. Nizungumzie kidogo hospitali ya Hydom, hospitali ya Hydom ipo katika Mkoa wa Manyara lakini ina-save Mikoa ya Singida na Mikoa ya Arusha kwa maana ya wenyeji wa Karatu na maeneo mengine hata ya Meatu. Kwa hiyo, ifike mahali sasa Serikali isaidiane kabisa kama ilivyoahidi kwenye mfumo huu wa PPP kusaidia hospitali ya Hydom kuendelea kutoa huduma njema na toshelevu kwa wananchi wake wa karibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tena kidogo suala la utalii, utalii wetu umekuwa na changamoto nyingi za kuandamwa na kodi nyingi, mfano wa TALA Licence ni dola 2000 kwa mwaka bila kujali anayelipa ni mzawa ama mageni. Nashauri Serikali ifike mahali wazawa wapewe first priority na kwa gharama rahisi kidogo ili wanapowekeza kwenye suala la utalii, basi vijana wengi wakapate ajira kupitia utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, magari mengi yamekuwa grounded, utalii umekuwa threatend na masuala haya ya Al-Shabab na hata Ebola. Wazungu kule nje hawajui umbali wa mahali Ebola ilipo na Al-Shabab ulipo, kwa hiyo, utalii umeshuka. Mimi naishi Arusha, kwa hiyo, niseme tu utalii umeshuka na imefika mahali hayo magari ya watalii sasa yamekaa tu yanafanya kazi za kubeba abiria wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto, nimesafiri mwenyewe Disemba mwaka uliopita, nimepita geti la Naabi pale wageni wanapoteza masaa yasiyopungua mawili mpaka matatu wakati wa kujiandikisha kuingia hifadhini. Sioni kwa nini hili liendelee wakati tupo kwenye dunia sasa ya sayansi na teknolojia. Muda mwingi mno unapotea foleni na jam inakuwa kubwa pale getini. Namwomba sana Mheshimiwa Jumanne Maghembe aweze kuangalia hilo ni kiikwazo. Mtu anayekwenda day trip kuingia pale chini crater na kurudi anapoteza masaa yasiyopungua matatu. Kwa hiyo, naomba hili nalo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.