Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Charles John Tizeba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa na mimi naomba niseme moja kwa moja kwamba, naunga mkono hoja ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuunga mkono niseme tu kwamba Kilimo, Mifugo na Uvuvi karibu Wabunge zaidi ya 60 wamezungumzia mambo mbali mbali; na kwa manufaa ya muda, naomba nizungumzie tu machache katika hayo ambayo kwa wingi zaidi yamezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nizungumzie tu suala la sukari kwamba sukari ipo nchini. Sukari ipo nchini na inaendelea kuletwa, sasa hivi tunachokifanya ni kusimamia vizuri usambazaji wa hii sukari ili ifike maeneo yale ambayo tulihisi kwamba yanaanza kuwa na upungufu na tumewaomba Wakuu wa Mikoa wasimamie vizuri zoezi hili la upelekaji wa sukari hasa kwenye Wilaya ambazo ziko mbali na Makao Makuu ya Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lililozungumziwa sana kwa hisia na Waheshimiwa Wabunge, ni kodi nyingi zilizoko kwenye mazao ya kilimo, uvuvi, na ufugaji. Hizi kodi kwanza Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliwaahidi Watanzania kwamba zitafanyiwa kazi, na kwa kadri itakavyowezekana, zitapungunzwa au kuondolewa. Bajeti hii imekwishaanza, ziko aina za kodi ambazo Waziri wa Fedha katika hotuba yake alipendekeza ziondolewe; na sasa hizo hazitakuwapo kwenye pamba, kahawa, korosho, ziko kodi ambazo tayari zimekwisha ondolewa na kwenye tumbaku pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo hili jambo linaendelewa kufanyiwa kazi, Serikali imeunda Tume ya Makatibu Wakuu, nilikwisha sema kwenye kujibu maswali ya Wabunge hapa, kwamba Kamati hiyo inaendelea kuzipitia, na kodi zile ambazo zitaonekana hazina madhara katika bajeti hii na bajeti za Halmashauri, zitaondolewa mara moja kadri ya mapendekezo yanavyokuja; na zile ambazo zitakuwa na effect kwenye bajeti hii, basi tutasubiri tuziondoe muda muafaka kwenye bajeti ya mwaka kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumeanza msimu wa pamba. Pamba msimu utazinduliwa kesho huko Mkoa wa Geita, katika kijiji cha Nyang‟hwale, naomba sana kwanza bei elekezi nzuri ambayo itakuwa na manufaa kwa pande zote mbili, wanunuzi na wakulima wa pamba itatajwa kesho. Lakini niombe kutumia muda huu kuwaomba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wa maeneo inakozalishwa pamba, wasimamie vizuri masoko, wananchi wasipunjwe kwenye mizani, kwa sababu wako wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, wanabana mizani kuwaibia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niseme na upande mwingine, kwamba wako wakulima wasiokuwa waungwana, wanaochakachua pamba kwa maji na michanga ili wapate uzito zaidi na kwa kufanya hivyo wanaharibu ubora wa pamba yetu, kwa hivyo wanapunguza thamani yake katika soko la dunia. Wote hawa niwaombe sana Wakuu wa Mikoa, hakikisheni mnatumia uwezo wa kisheria mlionao kudhibiti vitendo vya namna hii pande zote mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao lingine linaloleta shida sana katika usimamizi na uendeshaji wake ni tumbaku. Tumbaku umekuwa wimbo, vyama vya msingi vinakufa na wafanyabiashara makampuni ya tumbaku yanaendelea kunufanika na kupata faida. Sasa bahati mbaya sana hapa katikati utaratibu ulilegezwa wakaingizwa na wakulima binafsi na associations katika tasnia hii ya tumbaku. Matokeo yake imekuwa ni vyama vingi vya ushirika kudorora au kufa kabisa, kwa sababu hawa independent farmers na associations hizi, zingine hazina mashamba lakini wana tumbaku wanauza sokoni. Sasa tutahakikisha hili jambo haliendelei tena, maelekezo yalikwisha kutolewa wasisajiliwe upya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naangalia uwezekano wa kupunguza madaraja ya tumbaku. Madaraja ya tumbaku yako 67, haiwezekani. Wakulima hawajui, tumbaku ikisindikwa haitoki na madaraja 67, kwa nini katika kuuza iwe na madaraja 67. Hili jambo tunalifanyia kazi na kwa kweli nadhani tutayapunguza ili yawe yale yanayotambulika kwa wananchi na wakulima; kwamba madaraja ni matano, basi yabaki kuwa matano. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya wafugaji na wakulima. Hili jambo ukilitazama na chimbuko lake ni ukosefu wa malisho na maji kwa wafugaji, kwa hivyo wanalazimika kuhama kwenda kuvamia maeneo ambayo hayakuwa yamelengwa kwa ajili ya ufugaji. Sasa tunachokifanya tutarajie kwamba kwanza tutapitia upya mgawanyo wa Ranchi zote za Taifa, ili kujua wale waliopewa kweli walikuwa wanastahili; na hicho walichopewa kukifanya huko kama wamekifanya, kwa sababu kilichobainika katika ziara za viongozi wetu, ni kwamba mtu alipewa kipande cha Ranchi, badala ya kufuga yeye mwenyewe anakitumia kuwakodisha wenyeji wa eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii haikuwa nia ya Serikali kwamba iwagawie watu maeneo haya kwa ajili ya kukodisha, kwa hivyo tunaangalia upya, yule aliyeshindwa kutimiza masharti aliyokuwa amepewa tutawanyanganya ili wananchi waweze kugawiwa maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa wameombwa waainishe maeneo mapya, yanayowezekana kufanyia malisho na ufugaji wa ng‟ombe, ili tuweze kupanua maeneo haya; kwa sababu yako maeneo hayatumiki vizuri, sasa haya yakibainika mkoa kwa mkoa tunaweza tukawathibiti wafugaji wetu katika maeneo ya Mikoa yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tena kusema naunga mkono hoja.