Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Martha Jachi Umbulla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi nichangie Wizara ya hii ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yamezungumzwa na wazungumzaji wamenifilisi kidogo lakini niendelee kusisitiza kwamba kwanza naishukuru Serikali yangu kwa kuhakikisha kwamba bajeti ya mwaka asilimia 40 zinakwenda kwenye miradi ya maendeleo. Hii ni hatua ambayo imekuwepo kwa mara ya kwanza na kabla kabisa ya utekelezaji, kadri wenzangu walivyosisitiza tunaomba na kwa muda mrefu tumesisitiza kwamba Sheria ya Manunuzi iletwe haraka sana Bungeni tuweze kuifanyia marekebisho ili asilimia hiyo 40 iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo iweze kuwa na impact kwa bajeti hii ya mwaka 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kupanga matumizi ni jambo moja lakini kutekeleza yale yaliyokusudiwa ni jambo la pili na la muhimu zaidi. Nishauri Wizara kuhakikisha kuwa yale yote yaliyokusudiwa, yaliyopangiwa matumizi yaweze kutekelezwa jinsi ambavyo Bunge litapitisha na kuidhinisha matumizi hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hadi kufikia Machi 2016 fedha zile zilizokuwa zimepangwa kwa bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa mfano mafungu 62 yale yaliyoko chini ya Serikali Kuu ni mafungu 33 yaliweza kupewa fedha kwa asilimia 50. Kwa hiyo, ni wazi kwamba bajeti hiyo haitakidhi matarajio yale ama matumizi yale ambayo yamepangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria ya bajeti ambayo ni ya 2015 mwaka jana tu, tunatarajia kwamba sheria hiyo italeta impact kwa bajeti ya mwaka huu. Kwa kuwa kuna sheria, tuna imani kwamba matumizi ya fedha ambazo zimepangwa kufikishwa katika miradi yetu yatasimamiwa na sheria hiyo. Zaidi sana kwa kuwa tuna mid term review ya bajeti yetu, tunaamini kwamba Sheria ya Bajeti itaisimamia kikamilifu kuhakikisha kwamba jinsi Bunge litakavyoidhinisha fedha hizo zitaweza kufikishwa jinsi zilivyopangwa.
Mheshimiwa Naibu spika, nizungumzie na mimi mradi wa Village Empowerment maarufu kama shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Kwanza ni-declare interest kwamba mimi nina utaalamu kiasi fulani wa micro-finance na kwa hiyo, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wetu kwa kubuni mradi huu wa shilingi milioni 50 kila kijiji. Pia nieleze hofu yangu, sijajua vizuri kwamba hiyo shilingi milioni 50 ambazo zitatolewa kama mikopo kwa wajasiriamali ni pamoja na fedha zitakazotumika katika kuhamasisha wananchi ama zitakazotumika katika kuweka wataalamu watakaosimamia miradi hiyo ama ni fedha zitatengwa na bajeti nyingine ili kuweza kuhakikisha kwamba shilingi milioni 50 kwa kila kijiji inamfikia kila mwananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze wasiwasi wangu pia kwamba je, shilingi milioni 50 zinavyokwenda kwenye kijiji ni kwa jinsi gani kila mwanakijiji atafikiwa na fedha hizo? Kama hivyo ndivyo ilivyo na nadhani ndiyo matarajio ya Rais wetu kwamba kila mtu atapaswa kupata mkopo hasa wale waliolengwa wanawake na vijana. Kwa hiyo, ni lazima kuwe na mkakati madhubuti kuhakikisha kwamba hizi fedha zinawafikia walengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, fedha hizo zinawafikiaje? Mimi siamini utaratibu huu wa SACCOS, naamini zaidi utaratibu wa revolving loan fund ili fedha hizi zitakapotolewa kwa awamu ziweze kuzunguka zimfikie kila mwananchi. Kwa sababu tuna uzoefu tumeona kwamba katika mifuko mingine ambayo tumeahidiwa na viongozi wetu, kwa mfano mabilioni ya JK, bahati nzuri mimi nilikuwa mmoja wa walioteuliwa kati ya Wabunge saba kushauri katika ile National Executive Empowerment Council lakini tukaishia kupata barua na hatukuweza kuitwa hata siku moja na hatukujua hata yalikwendaje na yaliishia wapi. Kwa hiyo, tuna hofu kutokana na uzoefu wa kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba fedha hizi za sasa zikiwekewa utaratibu madhubuti, zikawekewa na riba kwa sababu riba ni suala muhimu sana katika kukopesha wananchi, unapoweka riba inazalisha zaidi na kupunguza uzito kwa Serikali kwa sababu ile riba inaweza ikatumika katika kuhakikisha kwamba kunakuwepo na wataalamu watakaolipwa ili wasimamie kwa kikamilifu utoaji wa mikopo na urejeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilishikwa na wasiwasi kama Wajumbe wengine wa Kamati yangu, ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, kwa shilingi milioni 50 zinapaswa ziende shilingi bilioni 980 na zitafikia jumla ya vijiji 19,600. Hata hivyo, tunaona kwamba zimetengwa tu shilingi bilioni 59.5 ambazo hazitoshi kabisa. Kwa hiyo, naishauri Serikali yangu iongeze bajeti hiyo ili azma ya kufikia kila kijiji kwa shilingi milioni 50 iweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile fedha hizi ziwekewe utaratibu ili zisiweze kupotea kama ambavyo tunaona utaratibu wa mikopo ya Halmashauri inavyopotoea kwa sababu haina ufuatiliaji, haina riba, haina hata namna yoyote ili ya kufuatilia nani kapewa, nani karejesha na kwa muda gani urejeshaji ufanyike. Mkopo ni fedha unayompa mtu kwa matarajio ya kurejesha kwa hivyo ni lazima uwe na utaratibu madhubuti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yamekwishasemwa lakini nashauri kwamba utaratibu huu wa revolving loan fund ni sawa unapompa mtu mwenye njaa samaki ukitarajia kwamba kesho atakuomba tena, lakini kumbe ni vizuri basi ukampa mtu vifaa vya kuvulia samaki ili aendelee kupata chakula badala ya kumpa samaki ambaye atakula leo tu na kesho atakuwa hana kitu. Kwa hivyo, mimi nashauri, revolving loan fund ndiyo utaratibu ambao utawezesha kila mwananchi kufikiwa ndani ya kijiji na hatimaye mradi utakuwa endelevu, hata Rais atakapokuwa amemaliza muda wake wa miaka kumi, atakuwa ameacha legacy ya mikopo hii inaendelea ndani ya nchi yetu, wananchi wanaendelea kukopeshana na hatimaye tunapunguza umaskini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na haya machache mengine yamezungumziwa sina sababu ya kurudia, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.