Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza kabisa nichukue nafasi hii nikushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti yetu hii, ya mwaka 2016/2017 nikitambua wazi kwamba ni bajeti ya kwanza kabisa ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa, na ndugu yetu, kamanda wetu, Rais John Pombe Magufuli, Hapa Kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia nikupe pole kwa haya unayoyapita sasa, lakini ndiyo maisha yenyewe, tatizo huwa ni uelewa na ufahamu ilivyo kila sehemu kunapokuwa na jamii fulani lazima kuwe na sheria na kanuni zinazowaongoza. Bila kuwa na sheria na kanuni inakuwa vurugu mechi. Sisi kama Wabunge tunapaswa kwa hakika kuonesha dhahiri kwamba Wananchi hawakukosea kutuchagua kutuleta hapa tuoneshe kwamba tunatakiwa kwenda kwa sheria na kanuni mbalimbali za maeneo tunayokuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napata shida ninapoona humu ndani tunakuwa viongozi wa kutokufuata hizo sheria na kanuni. Lakini ni jambo nalo lisilokwepeka kunapokuwa na jamii tuko wa aina mbalimbali tuwasamehe tu, lakini naamini sisi humu ndani tunaifanya kazi ya watu waliotutuma hata kwa niaba yao kuhakikisha kwamba nchi hii inasimama na Serikali ya Awamu ya Tano inakwenda kutekeleza bajeti yake ambayo imelala sana katika kuwatetea wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia nimshukuru sana Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri na timu yake yote, kwa hotuba yao nzuri waliyotuletea hapa ambayo sasa tunaijadili inayohusiana na bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017. Nawapongeza kwa sababu ninatambua nchi yoyote itajiendesha kwa wananchi wake kulipa kodi, na hata misaada mbalimbali ambayo Serikali yetu inapata kutoka nchi za wenzetu ni kodi za wenzetu, kwa hiyo na sisi tunapaswa tulipe kodi tuendeshe nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa zaidi na bajeti hii pale nilipoona imeweka asilimia 40, imelenga kumsaidia Mtanzania. Nasema kumsaidia Mtanzania kwa sababu imepelekwa kwenye maendeleo. Tatizo letu limekuwa kubwa, wananchi wetu wanapiga kelele sana na hata wenzetu upande wa pili wamekuwa wakilibeba sana. Hawaoni maendeleo ya haraka kwa sababu fungu hili lilikuwa linatengwa dogo sana. Kwa sasa kwa kuweka asilimia 40 nina amini tutakwenda na tutaona mabadiliko makubwa au maendeleo ya haraka kwa maendeleo ya wananchi kutokana na fungu hili kuongezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, wengi wamechangia na wamechangia kwa umahiri wao, naomba nizungumze suala hili tu kidogo kwa mfano ulipaji wa kodi na maendeleo ya nchi kwa ujumla. Naamini tunapozungumzia kulipa kodi, kuna kodi mbalimbali, kuna kodi za mazao ya shamba, mazao ya viwanda, za biashara na kadhalika. Katika mzunguko huu wa hizi kodi ndipo tunapotengeneza maendeleo ya nchi na tunapoona ushiriki wa kila mmoja wetu katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. Nichukue mfano wa mkulima wa pamba; analima pamba kama yeye anaipeleka kiwandani, kiwandani itatengenezwa nyuzi, itapelekwa kwenye kiwanda itatengenezwa nguo, itapelekwa dukani itauziwa watu mbalimbali na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue mfano huu nijikite kwenda kutetea hoja moja ya kwamba TRA sasa ikusanye mapato ya property tax badala ya Halmashauri. Majengo tunayoyaona mijini sehemu kubwa ni ya biashara, ni viwanda na ofisi. Wanahudumia akina nani? Wanahudumiwa wananchi wa Tanzania, wako wapi? Asilimia 70 ya Watanzania wako vijijini, ina maana gani? Ina maana kwamba hayo majengo, hizo biashara za mjini na ofisi za mjini zinaendeshwa pia na watu wa vijijini kwa kiasi kikubwa, kama ni vyakula vikitengenezwa vitakwenda mpaka kijijini kwenye asilimia 70, kama ni nguo zitakwenda mpaka vijiji kwenye asilimia 70 ya wananchi.
Tukiangalia Halmashauri za vijijini mapato yao ni kidogo, kwa sababu maendeleo makubwa yako mijini, Halmashauri za mijini zina mapato makubwa kwa sababu zinabebwa na Halmashauri za vijijini. Kwa hiyo, unapoacha wa mjini anafaidi wakijijini hafaidi, kwa kiasi fulani tunakuwa hatuwatendei haki, lakini naamini sasa kwa kusema TRA ikusanye itaweka ratios ambazo zitaisaidia kwamba hata Halmashauri za vijijini zipewe fungu na makusanyo hayo. Sawa mjini watapata fungu lao kubwa, lakini vijijini na wao hawataachwa watapewa fungu ili kwa pamoja tuweze kuangalia namna gani tunasukuma maendelo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache nichukue nafasi hii niseme tu kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia 100 asante sana.