Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri naomba anisikilize kwa makini ili nimshauri, ingawa tuko wachache huku lakini tuna ushauri mzuri kweli, huko usione wingi huo, hakuna kitu watakachokushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwenye hiki kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 112 ameelezea malengo ya Wizara yake. Kwenye lengo namba tatu, anasema kuendelea kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba, naishia hapo hapo kwa sababu nina dakika tano. Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana na wamesaini mikataba kwamba kila nchi itakuwa na Wizara maalumu inayoshughulikia Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kenya wana Waziri wa Mambo ya Afrika Mashariki na wana Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje; Uganda hali kadhalika; Rwanda hali kadhalika na sisi Rais Kikwete alikuwa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Waziri wa Afrika Mashariki. Ndiyo, Mheshimiwa Mwakyembe anasikitika nini, alikuwa Waziri wa Afrika Mashariki. Mwanasheria Mkuu wa Serikali hajui kama kuna mkataba wa Afrika Mashariki kwamba lazima kuwe na Waziri Maalum anayehusika na mambo ya Afrika Mashariki au huyu Mwanasheria anamshauri nini Rais sasa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba nilirejeshe kwa sababu Mheshimiwa Waziri ndiye anayehusika, suala la mabaki ya mjusi wa Tendegulu yaliyopo Ujerumani. Aibu! Watu wa Ethiopia walikuwa na mnara wao ulikaa Italia miaka 68, wameurejesha. Leo tuna mabaki ya mjusi yamechukuliwa Tanzania ninyi mnakaa hapa kuja kusifia tu, tani 70, sijui alikuwa na urefu wa mita 60, Tanzania tunanufaika na nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeandika barua nimewaletea kwenye Wizara hii, Makatibu Wakuu walichonijibu sikielewi, mara mpaka leo wanafanya calculation, hawajui Tanzania inanufaika na nini. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu hapa aje atuambie Tanzania inanufaika na nini na mabaki ya mjusi wa Tendegulu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani mjusi huyu mkubwa anaijengea historia Ujerumani, yuko pale Hamburg, watalii wanakwenda kuangalia wanaingiza pesa Ujerumani, leo alikotoka mjusi maji ya kunywa hawana, barabara hakuna, Wazungu wanakwenda pale Tendegulu tunawabeba mgongoni. Mheshimiwa naomba majibu na niliwaambia wananchi wangu na Mheshimiwa Magufuli alisema wakati wa kampeni alipokuwa Jimbo la Mchinga kwamba atashughulikia suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiona Waziri anashindwa kulishughulikia nitawachukua wananchi 112,000 wa Jimbo la Mchinga, nitampelekea Mheshimiwa Magufuli awajibu alichowaahidi wakati wa uchaguzi. Haiwezekani kama Taifa tunakaa tu, vitu vyetu viko nje vinawanufaisha watu wengine, sisi wenyewe tuko bwerere tunafurahifurahi tu hapa. Tunaomba majibu, mabaki ya mjusi wa Tendegulu tunayapata na kama hatuyapati tunanufaika na nini? Tunaomba majibu juu ya hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni suala la Chuo cha Diplomasia. Limezungumzwa sana. Hiki chuo wamekitelekeza au hiki chuo sasa hivi kazi yake ni nini? Miaka mitatu Chuo cha Diplomasia hawapeleki bajeti ya maendeleo na ni chuo ambacho kina-train wanadiplomasia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Waziri na nivishauri vyama, kuna umuhimu wagombea wa Urais waanze kupitia pale kwa sababu tunaingia kwenye matatizo ya kidiplomasia kwa sababu viongozi wetu wengine hawajui hata maana ya diplomasia ni nini. Ndiyo maana leo unakuta tunazuia hela za MCC shilingi trilioni moja, kiongozi mkubwa wa nchi anasema yeye haoni kama ni tatizo. Mheshimiwa Waziri nataka atakapokuja hapa atuambie tumewakosea nini, tatizo nini, diplomasia yetu imeyumba kwa kiasi gani mpaka pesa za MCC zimezuiwa, aje ajibu hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda tu, lakini nilitaka nimshauri mambo mengi. Nakushukuru.