Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipatia fursa hii kuweza kuchangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2016/2017.
Awali ya yote, nachukua fursa hii ya kipekee kabisa kuwashukuru wananchi wa Tarime Mjini, kwa mara ya kwanza tangu dunia iumbwe kuweza kuchagua mwanamke tena kutokea Chama cha Upinzani. Wameudhihirishia ulimwengu kwamba wamechagua mtu ambaye atawasemea na kuwatumikia na siyo jinsia. (Makofi)
Vilevile nawashukuru wananchi wa Mkoa wa Mara kwa kuonesha kwamba wana imani kubwa na UKAWA; na CHADEMA wote mtakumbuka kwamba Bunge ililopita alikuwepo Mbunge mmoja tu wa kuchaguliwa, lakini sasa hivi tupo Wabunge wanne kutoka Mkoa wa Mara licha ya dhuluma nyingi nyingi, lakini nafikiri CCM mmeisoma namba kidogo kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuchangia na nianze na utawala bora. Kwenye utawala bora, wakati wa uchaguzi yalijitokeza mambo mengi sana. Cha kusikitisha, hata Mheshimiwa Rais Magufuli alisema uchaguzi umeisha na mambo yameisha; lakini mpaka leo wale ambao wanaonekana walikuwa washabiki wa vyama vya upinzani, wameendelea kunyanyasika, wanakamatwa na wanabambikiwa kesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea hili nikizungumzia Jimbo langu la Tarime Mjini. Kuna wananchi wamebambikiwa kesi, wengine wamepewa murder case ya binadamu ambaye anaishi na ameenda akasema kabisa huyu mtu sijawahi kukosana naye na wala sijafa na nipo hai. Huyu anaitwa Charles Kitela Chacha na amepewa mashitaka ya murder mwenye PI No. 37/2015. Utawala bora uko wapi? Mtu ambaye wanasema ni Marehemu ameuawa anaitwa Wambura Ryoba Gucha, yupo hai wa Kijiji cha Turugeti, Tarime. Tunaomba muwe na utawala bora ili haki itendeke; na kama tutaenda kwenye demokrasia na uchaguzi muweze kupata haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, Chama tawala kinasikitisha. Mnapoona wapinzani wameshinda, mnawawajibisha watendaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninavyoongea, Tarime, Watendaji wanawajibishwa, walimu wanasumbuliwa, RPC amehamishwa, OCD amekuwa demoted kisa Mheshimiwa John Heche kashinda Tarime, Mheshimiwa Esther Matiko ameshinda Tarime; Halmashauri ya Mji wa Tarime upo CHADEMA; Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, upo CHADEMA. Utawala bora upo wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata watu wakisimama hapa wakaongea yanayotokea upande wa pili, nami nikipata muda baadaye nitazungumzia, mnabaki mnaona kwamba wanaongea ndivyo sivyo mjichunguze, mwitendee haki Tanzania. Tunataka amani, tusiimbe amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine sasa nichangie kuhusu uchumi na viwanda. Tumekuwa tukishauri; Bunge lililopita nilikuwa Waziri Kivuli wa Mipango na kwa bahati nzuri sana ambaye ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mpango alikuwa akituletea. Atakuwa ni shuhuda na amekidhihirisha hiki ambacho naenda kuongea kwamba mnapanga vitu bila uhalisia. Hiki kitu ambacho tunasema uchumi na viwanda hakiwezi kufanikiwa kama tunapanga vitu bila uhalisia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Tunajua kabisa ili tuweze kuwa na uchumi na viwanda ni lazima tuwe na barabara ili hata wale wazalishaji, wakulima waweze kusafirisha mazao yao na kufikisha kwenye viwanda. Lazima tuwe na reli imara, lazima tuwe na umeme, maji na vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye barabara ukiangalia ukurasa wa 27 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 mnatuambia kipengele cha pili ujenzi mpya wa barabara zenye urefu wa kilometa 5,427 na kukarabati barabara zenye urefu wa kilometa 1,055 kwa kiwango cha lami. Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 mnaweza mkajenga kilometa 5,427 iwapo kwa miaka mitano mmetujengea kilometa 2,700.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uhalisia gani? Ndani ya mwaka mtajenga Kilometa 5,400! Let’s be realistic! Ndiyo maana leo tutapoteza nguvu nyingi kuwashauri hapa; tutapoteza fedha nyingi za Watanzania, mnachokiandika hakioneshi uhalisia. Kwa hiyo, naomba kabisa, tuwe tunaonesha uhalisia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmeainisha reli nyingi, nyingi! Mimi natokea Kanda ya Ziwa na ningependa kabisa reli ya kati iweze kukamilika ili tuweze kupunguza ajali. Siyo tu kukuza huu uchumi wa viwanda ambao mnasema; jana walisema hapa miundombinu ya barabara haichangii vifo, lakini kiuhalisia tunapoteza nguvu kazi ambazo tumezisomesha, wengine ni ndugu zetu ambao ni wajasiriamali wa kawaida, wanakufa barabarani kwa sababu ya barabara mbovu. Malori yanapita hapo hapo, ajali nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imarisheni reli ili tusafirishe kwa reli. Kwanza tunakuza uchumi lakini hatutapoteza Watanzania. Ninachokiona mmeainisha hapa, tutarudi hapa mwezi wa sita mwakani, mtaanza kusema hatukupata fedha na asilimia nyingi za maendeleo zilikuwa zinatoka kwa wahisani; na sijui sekta binafsi; tutaanza kuimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bora mwandike mtajenga kilometa 300 za lami tutawaelewa, kuliko kutuandikia 5,400 halafu tunakuja hapa mwakani hamjafanya chochote. Tunapenda sana Watanzania tuwe na hiyo mnayosema uchumi wa viwanda; tunapenda kuona Watanzania wengi wakiwa kwenye uchumi wa kati na siyo wachache wapo juu, wachache ni masikini wa kutupwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuwe na uchumi wa viwanda nimeshataja. Kuhusu kilimo chetu; zaidi ya 70% Watanzania tunajishughulisha na kilimo, lakini kilimo ambacho hakina tija. Ile kauli mbiu ya kilimo kwanza tumeiimba, tumeicheza hakuna mafanikio. Mkisoma ripoti zenu zenyewe kuhusu kilimo inaainisha dhahiri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni shida ingawa mmesema Mpango ulioisha umekamilisha kwa 68% vijijini na 95% mjini. Ndiyo maana nasema tuwe wakweli. Leo kule Tarime Mjini ukiyaona maji utafikiri ni ubuyu, tuje na uhalisia! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pensheni kwa wastaafu. Mwaka 2015 tulipitisha tukasema walipwe shilingi 100,000/=, lakini kuna watumishi tena Mapolisi ambao mnawatumia sana, wanalipwa shilingi 20,000/= mpaka leo. Sasa mlipokaa hapo mjiulize, hawa Watanzania wanaishi vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kampeni Mheshimiwa Magufuli alisema na hata kwenye Star TV mlikuwa mnarusha sana; ushuru wa kero kwa maana mboga mboga, matunda, mama ntilie na wengine wote mnaenda kuondoa. Leo Watanzania hawa wananyanyasika; na alisema pia mgambo watatafuta kazi nyingine. Mimi nasema mnisikilize na mwondoe wale mgambo kwenye Jimbo la Tarime Mjini. Watanzania wote, wamama, wababa, vijana wanaojitafutia wamachinga, mlisema ushuru mdogo mdogo mtaondoa. Tubuni vyanzo mbadala tusiwakamue hawa ambao wana kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure, mimi naomba mseme mmepunguza makali ya elimu, lakini siyo elimu bure.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu muda ni mchache, nimalizie kwa Zanzibar; ingawa watu walisimama hapa wakasema sisi wa Bara tusizungumzie ya Zanzibar. Kiukweli tujichunguze, kiuhalisia, tena nianze na Mheshimiwa King siku ile alisema kwamba maiti walipiga kura. Kama maiti walipiga kura, ajiulize na yeye huyo maiti alipiga kura tano. Yeye kama Mbunge wa Jamhuri amefuata nini hapa na yeye alipigiwa kura na maiti? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni sawa na kumwambia muislamu, umepika kitimoto, umechanganya na kuku, unamwambia achukue kuku, aache kitimoto, wakati ile supu yote imechanganyikana. Mmechambua kuku ambao ni wale Wabunge wa Jamhuri na Rais, mmeacha wale Wawakilishi kwamba ndio kitimoto. Jichunguzeni! Kama ni maiti alipiga kura, amepiga kote. Tutendee haki Watanzania wa Zanzibar, tusiingize nchi kwenye machafuko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi. Mmeainisha mtapima ardhi, tunaomba mfanye hivyo. Ardhi imepimwa kwa 10% tu, kule Tarime Mjini tunahitaji mpime ardhi ili tupate thamani tuweze kukopa na kujishughulisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Mheshimiwa Magufuli kwenye kampeni alisema atatoa shilingi milioni 50 kwa kila Kijiji na Mtaa. Sijaona mmeainisha; naomba mwainishe, wananchi wa Tarime mimi nina Mitaa 81, ili tuanze kuzipata hizo shilingi milioni 50 kuanzia mwaka huu wa fedha, tuweze kunufaika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.