Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mfenesini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KAN. MST. MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru nafasi hii na mimi ya kuchangia mambo machache tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa maombi tu kwa Wizara hii ya Mambo ya Nje. Kwa kipindi kifupi ambacho tunaambiwa tunataka kujiunga na mtengamano wa Afrika ya Mashariki wasi wasi wangu mkubwa bado elimu hii haijafika kwa wananchi wa Tanzania. Na kama tukienda hivi itakuwa ni kama wale abiria tunaodandia gari lilishaondoka. Tumeona uzoefu, hasa kwetu hapa Tanzania na Zanzibar zaidi, sehemu nyingi za ajira wafanyakazi wengi wanatoka Kenya. Na tatizo si kwamba nafasi hizi Watanzania hawaombi, Watanzania wanaomba nafasi, sifa za kuajiriwa hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokwenda kwenye mtangamano huu wa Afrika ya Mashariki wasiwasi wangu tutakuja kukuta hapa sasa Wizara zote, sehemu zote za biashara na mambo mengine yamechukuliwa na wenzetu kwa sababu tayari walishajipanga. Ninaiomba sana Wizara hii ijitahidi, kwanza ifikishe elimu, tena tujipange sasa sisi wenyewe tunaingiaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko tunakokwenda ni kugumu kwa mawazo yangu nadhani tutakwenda kuanguka huko. Hatujajipanga, kama tuliodandia gari vile. Kwa hiyo, ninaomba sana Wizara ijitahidi kufanya uwezo wanaouweza wao walionao kuhakikisha vijana wetu nao wanakuwa na sifa; kwanza kwa kuajiriwa lakini pili tupunguze na sisi kununua bidhaa kutoka nchi za wenzetu, tujitahidi na sisi kuzalisha kupeleka kwa wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la kupeleka bidhaa nje ya nchi Serikali yetu ijitahidi kuondoa vikwazo, bado corruption ipo Tanzania. Wafanyabiashara wetu wanapata vikwazo vingi, wanapotaka kupeleka bidhaaa zao nje ya nchi wanapata vikwazo tofauti na wenzetu. Bidhaa zinazokuja tunapokea vizuri tu, lakini zetu sisi tukitaka kuzipeleka humo njiani mtu anakwama mpaka anaamua kuziuza njiani. Ninaomba sana Serikali hii ijitahidi na Wizara hii isimamie biashara na sisi tuwe tunanufaika na wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa ninataka kuzungumza kidogo. Tunapokuja hapa Bungeni kuna watu wanazungumza mambo mengi, wengine hatujasafiri, tumesafiri kidogo nje ya nchi. Sasa tunalinganisha wenzetu na sisi, lakini ninasema tulinganishe wenzetu na sisi katika baadhi ya mambo. Baadhi ya mambo Tanzania tuko mbele sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengine, kweli, wala tusikatae, ziko nchi kubwa zimetushinda lakini yako mambo sisi tuko mbele. Yule anayesema amekwenda Washington DC mimi pia nimeshafika huko, na si mara moja. Lakini ukisema maendeleo wanaangalia watu wanavyotembea mitaani, maendeleo wanayaona mitaani kwa zile sura za mitaa. Mimi nilishawahi kufika Washington DC nanikakuta barabara ina shimo, katikati ya barabara. Barabara yetu ya Kimara ni nzuri. Kwa hiyo, bado tuseme tu, yako mambo tumezidiwa, lakini yako mambo wenzetu bado wametushinda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kaka yangu, ndugu yangu mmoja hapa, Mheshimiwa Msigwa, sijui kama ni mchungaji maana hajawahi kuniambia na ni rafiki yangu sana lakini hajawahi kuniambia. Amesema, sitaki kulijibu lakini sijafanya kazi sana foreign, nilikuwa nayaona mambo mengine ambayo yanafuatwa, hasa suala la Mabalozi. Anapozungumza Mabalozi wanakatazwa, sijafahamu, labda atakuja kunifahamisha nikikutana naye nje. Nina vyofahamu mimi Balozi kama Balozi, hakatazwi kukutana na mtu, isipokuwa kuna taratibu lazima Balozi azifuate.
Mheshmiwa Mwenyekiti Balozi atakapo kwenda kwenye Taasisi au kuonana na mtu yoyote, lazima Ofisi ya Mambo ya Nchi za Nje ielewe. Lazima atoe taarifa na taarifa zifikishwe kule anakokwenda, sio kukutana naye tu halafu useme. Mimi sidhani kama Balozi anakatazwa kukutana na mtu, tunakutana na watu binafisi hiki kitakuwa chama?
Mheshimwa Mwenyekiti, utaratibu, tunachozungumza utaratibu ukifuatwa, sidhani kama Balozi anakatazwa kukutana na mtu. Naomba tu wanapotaka kukutana na watu kama hao, si wafuate utaratibu tu! Wasiogope kwa sababu utaratibu upo, umepangwa na wautekeleze, hakuna haja ya kuleta mambo mengine hapa ambayo kwa kweli ni kupotosha, si kweli! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema tunapokuja Bungeni, hasa Bunge letu la Tanzania hili, tukitaka liwe na heshima, sisi wote kwanza tuheshimiane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.