Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Agnes Mathew Marwa

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kusimama katika Bunge hili Tukufu siku ya leo. Kwa umuhimu zaidi nawashukuru sana wapiga kura wangu, wanawake wa Mkoa wa Mara, walionipigia kura nyingi sana za kishindo hadi leo hii kuwepo hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashukuru kwa upekee mama yangu mzazi na baba yangu, pamoja na Mashirika ya Kikristo yaliyonifanyia maombi, pamoja na Mashekhe na wanamaombi wote na watu wote wa Mkoa wa Mara waliokuwa wanafurahia leo hii niwe Mbunge. Nawashukuru sana, nawaahidi sitawaangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kunukuu kidogo Hotuba ya Mheshimiwa Rais kwa sababu sikupata nafasi ya kuongea siku ile. Kwa ruhusa yako naomba ninukuu. Hotuba ya Mheshimiwa Rais iliwakumbusha watumishi wengi wa umma ambao wengi walijisahau wajibu wao, hivyo aliwakumbusha watumishi wengi kuwajibika kwa umma kwa taaluma na weledi kwa kuzingatia usawa bila upendeleo kwa watu wote, bila kujali itikadi ya vyama na dini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, nampongeza Mheshimiwa Rais Magufuli kwa hotuba yake ambayo imehimiza kuzingatia kanuni na maadili ya utumishi wa umma (integrity). Hivyo basi, kwa hotuba hiyo nzuri ya Mheshimiwa Rais tunatarajia kwamba kila mtumishi mahali pake pa kazi atimize wajibu wake ipasavyo na kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza ndoto na matarajio ya Watanzania walio wengi hasa wa kipato cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza moja kwa moja kwa kuongelea au kuchangia kwa suala la ujasiriamali. Wajasiriamali au ujasiriamali ni suala ambalo linatakiwa liangaliwe kwa macho ya ziada, kwa maana katika Mpango wa Taifa au Mpango wa Maendeleo, wajasiriamali ndio wanatoa mchango mkubwa sana kwa Taifa hili; na haswa naanzia na akina mama wa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akina mama wa Mkoa wa Mara ambao wanafanya biashara ndogo ndogo, ikiwemo wafanyabishara wa dagaa, ikiwemo wale wanaouza mboga mboga na wengine wa masokoni wananyanyasika sana kutokana na kutozwa ushuru usiokuwa na sababu. Kwa hiyo, naomba tuangalie sana hawa wajasiriamali kwa macho ya huruma, kwa maana na wao wanatoa mchango mkubwa sana katika Serikali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niende kwenye suala la maji. Suala la maji limekuwa ni ni kilio cha kudumu katika Taifa hili la Tanzania. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangazie sana macho yake na itoe kipaumbele katika suala la maji, kwa maana suala la maji limesababisha matatizo na majanga makubwa hasa kwa wanawake wetu wa Mkoa wa Mara, kwa kuvuruga au kuachanishwa kwa ndoa zao kutokana na umbali mrefu wanakwenda kutafuta maji. Vilevile limekuwa likiwasababishia ulemavu wa migongo, limekuwa pia likiwaletea shida sana katika uzazi. Kwa hiyo, kwa namna ya kipekee sana liangaliwe suala la maji na hasa Mkoa wa Mara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami pia naungana na Waheshimiwa walioongea jana, Mheshimiwa Zitto Kabwe pamoja na Mheshimiwa Lugola, kuhusiana na suala la reli. Ni kweli katika mazingira ya kawaida, utaratibu ambao unatakiwa katika kuunganishwa kwa reli ili nchi ya jirani au ndugu zetu wa jirani wapate unafuu, ni kitu ambacho siyo kizuri sana, kwa sababu kwanza itatupotezea sisi Pato la Taifa na wao kwa ujanja wao, wanachotaka kukifanya ni kwamba wataunganisha kule juu kwa juu nchi nyingine ili malipo haya yasije Tanzania. Kwa hiyo, hilo suala liangaliwe au lipewe kipaumbele, liwe kama lilivyoongelewa na Mheshimiwa Zitto au Mheshimiwa Lugola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie sana suala la polisi kuhusiana na makazi au vituo vya kazi. Vituo vya kazi na masuala ya makazi ya polisi wetu imekuwa ni shida sana. Hivyo, Serikali ingechukua taratibu za ziada ili iingie mkataba na Shirika la Nyumba la Taifa ili kuwajengea nyumba za kudumu hata baadaye watakapomaliza kuzilipa ziwe za kwao hata pale wanapokuwa hawapo kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba ndugu zangu wa upinzani, tumtie moyo Rais wetu Mheshimiwa Magufuli. Ameanza vizuri. Siyo kila kitu tunaongea maneno machafu, maneno ya kashfa, maneno ya dharau, kiasi kwamba hata wewe ukiombwa kitu huwezi ukakubali kama mtu ameongea maneno ya dharau. Hata Mwenyezi Mungu anatoa pale unapomsifia; ndiyo maana unasema; “Baba yetu uliye Mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, mapenzi yako yatimie, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni,” ukimaliza unampiga kibao Mungu, halafu ndiyo unamwomba, “utupe riziki yetu ya kila siku.” Siyo ninyi kila siku mnatoa matusi tu. Kesho msipofanyiwa maendeleo mnalalamika.
Ndugu zangu Wapinzani nawaomba sana; mmefanyiwa mambo mengi sana kwenye Majimbo yenu kuliko hata sisi wa CCM. Mfano ni Arusha au Mkoa wa Kilimanjaro, uko wazi kabisa, mmefanyiwa mambo mengi mazuri, hata barabara mlizonazo ni kama barabara za Kimataifa, mikoani kwetu, hatuna. Mnatakiwa muwe na Shukurani, lakini pia mnatakiwa mkubali kwamba aliyeshinda, kashinda, ninyi mmeshindwa. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Muda wako umekwisha.