Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami nichangie katika mjadala huu wa bajeti ya Serikali. Nikupongeze sana wewe, kama walivyokupongeza wajumbe wenzangu wa Baraza hili la Kutunga Sheria kwa maana ya Bunge, kwa ujasiri wako na weledi mkubwa wa kuliongoza Bunge hili Tukufu kwa kufuata Kanuni ambazo Bunge hili limejitungia ili kujiendesha. Kwa mwanamke kijana kama wewe umeonesha umahiri mkubwa na ni mfano mzuri wa kuigwa kwa viongozi waandamizi wa nchi hii, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri wa Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Mpango kuanzia kuteuliwa kwake na Mheshimiwa Rais kuwa Mbunge lakini kuwa Waziri wa Wizara nyeti, Wizara ambayo ndiyo mhimili wa Serikali. Pia nimpongeze mdogo wangu Mheshimiwa Dokta Kijaji naye kwa kupata fursa hii adhimu ya kulitumikia Taifa hili kwa nafasi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze pia Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa utendaji mzuri. Mheshimiwa Rais amekuwa akifanya kazi nzuri sana pamoja na changamoto za hapa na pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nianze kwa kuchangia kuhusu Wizara yenyewe ya fedha, lakini bajeti nzima ya Serikali. Waziri amekuja na mpango mzuri sana hapa, suala la kutokupandisha bei katika tozo za mafuta, niipongeze sana Serikali kwa kuliona hili kwa sababu impact yake huwa ni kubwa na inapelekea mfumuko mkubwa wa bei. Kwa kufanya hivi, maana yake sasa tutabaki katika mpango ule ule, kwa hiyo tutakuwa na changamoto chache.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nikumbushe Waziri au Serikali iangalie sana maduhuli ambayo yanakusanywa na Serikali hii kupitia maeneo mbalimbali (mapato yasiyokuwa ya kodi). Kuna eneo ambalo tukiliangalia kwa makini sana linaweza likachangia sana, eneo la misitu ya asili lakini eneo hili la misitu ya kupandwa na Serikali. Kuna mashamba makubwa ya Serikali, utaratibu mzuri ukitumika na kuhakikisha wazawa wananufaika na mashamba yale, basi yana mchango mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka mitano iliyopita miongoni mwa maeneo ambayo yalichangia katika Wizara ya Maliasili ni pamoja na sekta hii ya misitu. Mashamba ya Lunguza, Mashamba ya Mtibwa lakini misitu ya asili kama itavunwa kwa utaratibu mzuri bila uharibifu wa mazingira, Serikali ina chanzo kizuri sana cha mapato. Niiombe sasa Serikali napo hapo ipaangalie kwa macho mawili, ipatendee haki ili Serikali inufaike na rasilimali zake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika huduma za jamii Serikali imekuwa ikifanya vyema sana. Katika afya kuna mpango wa kujenga zahanati kila kijiji, lakini kuna kujenga kituo cha afya kwa kila kata, mpango huu umekuwepo kinadharia sana. Wakati umefika na wakati muafaka, kwa sababu ahadi yetu sisi Wabunge, Mheshimiwa Rais wetu wa Chama cha Mapinduzi tulikuwa tukimuunga mkono kwa kuwaambia wananchi kwamba sasa Serikali inayokuja itakuwa na mpango wa kujenga zahanati kila kijiji lakini kila kata kitajengewa kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji tuone hapa na Serikali ije itueleze sisi Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwamba inajipangaje kuhusu kutekeleza ahadi hizi ambazo humu katika makabrasha ya bajeti haionekani vizuri, sijui wana mpango gani. Tusije tukaenda kwa mpango ule tulikuwa na dhamira ya kujenga maabara kila shule ya sekondari matokeo yake zile nguvu zikasukumwa kwa wananchi moja kwa moja. Ni jambo la hatari na mpaka leo kuna baadhi ya maabara hazijakwisha kwa sababu kulikuwa hakuna mafungu isipokuwa mkoa mmoja tu wa Dar es Salaam ambapo Serikali ilitenga bajeti na ika-facilitate ule mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye elimu, tumeliona hili la elimu bure. Niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji wa jambo hili ambalo maswali kwetu sisi kama wawakilishi wa wananchi yamepungua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana katika suala hili la huduma za jamii ikiwemo maji. Wabunge wengi wamezungumzia maji ni tatizo katika maeneo yao lakini na mimi niseme wazi kwamba miongoni mwa majimbo ambayo maji ni tatizo Jimbo langu la Manyoni Magharibi maji ni tatizo kubwa. Ile mita 400 kule kwetu hata ukifanya mkutano ukiwaambia mita 400 watakushangaa sana labda useme angalau tupunguze kutoka kilomita saba, nane zilizopo sasa kufuata maji mpaka angalau kilomita mbili, sasa tunafanyaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri sasa Serikali ikajipanga isaidie Wabunge ambao majimbo yao ni magumu, tuongeze mafungu pale ili maji yaweze kupatikana na tutakapofika katika chaguzi zingine tuweze kuwa na kauli nzuri na kuhakikisha chama hiki ambacho ndiyo chenye Serikali kinarudi na Wabunge wengi zaidi kuliko tuliopo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa mikoa maskini ni Mkoa wetu wa Singida. Mkoa wa Singida na mikoa ya katikati kwa ujumla, Mkoa wa Dodoma na mikoa mingine ambayo tunapakana nayo watu wake ni hodari sana katika kilimo lakini tumekuwa na changamoto ya kilimo hiki cha kutegemea mvua. Niiombe sasa Serikali ifike mahali tuwe na mpango madhubuti, tutoke katika kilimo hiki cha kutegemea mvua ili tuweze kutengeneza miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, water table ya maji ipo karibu tukiyachimba na kuyapandisha yale maji kwa miundombinu safi na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji, haya majanga yanayotukabili watu wa mikoa ya katikati likiwemo baa la njaa yataondoka kabisa. Niiombe sasa Serikali ije na mpango wa kuondokana na kilimo hiki cha mvua tuweze kutegemea kilimo cha umwagiliaji ambacho kitakuwa na tija kwa nchi yetu na jamii yetu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali yangu pia kwa kuondoa mageti haya ambayo yalikuwa yana shida kwa wakulima wetu. Pia nizungumzie hili pia la ujenzi wa reli ya kati pamoja na matawi yake. Jambo hili ni jema na likienda na mpango huu kwa hakika uchumi utaendelea kwa sababu miundombinu ikiwa mizuri basi uchumi unakuwa ni rahisi na unakuwa mwepesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wamezungumzia sana kuunganisha RAHCO na TRL, RAHCO ni mmiliki wa miundombinu, TRL aendeshe reli. Ikiwa mwendesha reli akamiliki miundombinu ni hatari sana. Tuendelee kubaki na utaratibu tulionao leo, RAHCO aendelee kumiliki miundombinu kwa niaba ya Serikali, lakini TRL libaki kama shirika linaloendesha miundombinu ambayo ni mali ya Serikali. Ni jambo la hatari kama tutafika mahali tutabinafsisha Shirika la Reli na miundombinu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.