Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijaanza kuchangia nianze kuweka rekodi sawa sawa. Hapa ndani kwa sababu kuna Wabunge wenzangu wakati mwingine wanasema kwamba Mawaziri waache siasa. Nataka niongee tu jambo hili; kwanza siasa ni taaluma; na sisi tuliopo wote hapa tumeingizwa kwenye siasa. Siasa ni ngumu sana, lakini ni nzuri sana, tatizo ni tunavyoitumia tu kama wenzetu wanavyoitumia vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kupata Ubunge ni kazi kweli kweli na suala la kupata Urasi ni kazi kweli kweli! Sisi ambao tumepita kwenye mchakato huu tunajua joto lake. Kwa hiyo, hata wote tunapokuwa humu tumebeba mizigo; wa kuteuliwa, sijui wa kutoka group gani, inategemea mizigo hiyo ina uzito gani; lakini uzito wa Jimbo ni uzito kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba duniani kote hakuna mtu anayehitaji kulipa kodi. Hata vitabu vya dini vimezungumza sana suala la kulipa kodi na aliyekuwa akitoza kodi wakati wa Yesu alikuwa ni mtu ambaye anachukiwa na Umma wote. Kwa hiyo, Serikali kukusanya kodi isiogope, ni jambo la kawaida, ndiyo uhai wa Serikali. Naiomba sana Serikali hii isirudi nyuma, ihakikishe inakusanya kodi ili wananchi waweze kupata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la maji. Suala la shilingi 50 kuongezwa kwenye dizeli na petroli ili iende kugharamia maji, ninasikitika sana, kwamba Serikali imeona kwamba ikiongeza shilingi 50 italeta mfumuko wa bei. Nataka kuuliza au mmeshatuuliza? Sisi Wabunge humu ndio watumiaji wa mafuta. Tumeshakataa kuongezwa hii shilingi 50? Sisi tumeshakubali tuongezwe shilingi 50 kwenye petroli pamoja na dizeli ili kugharamia Mfuko wa Maji Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu inasema mita 400 wananchi waweze kupata maji. Kwa namna hii tunayokwenda, hatutaweza kuifikia hiyo sera na mwaka 2020 tutapata taabu kweli kweli kurudi humu Bungeni, kwa sababu wakina mama wanateseka kila asubuhi, kila saa kumi na moja wanakwenda kuteka maji. Tuwahurumie! Wanapoteseka akina mama na sisi akina baba tunateseka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja nimewahi kusema asali ni tamu sana lakini wako watu hawaitumii asali, lakini kila mmoja anaguswa na maji; awe mtumia gari, anaguswa na maji aoshee gari lake. Kwa hiyo, naishauri Serikali hii ya Awamu ya Tano, Serikali ya kazi; kwa sababu unaweza kuwa na Serikali sikivu, ikawa inasikia tu, isifanye kazi. Sasa hii ni Serikali ya kazi, ifanye kazi kuongeza shilingi 50 ili akina mama waweze kupata maji ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongea haya kwa sababu nimetoka Jimboni, hali ni mbaya, akina mama wanasumbuka na mimi nina hali mbaya! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ungenionea huruma ukanipatia chupa ya maji hapa ili niweze kuongea vizuri huku nakunywa maji. Naomba hili, wala halipaswi kujadiliwa, iongezwe shilingi 50 kwenye mafuta, wala tusijadili hili; kama haitaongezwa, kama kuna kushika shilingi, mimi nitashika shilingi kwa sababu ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia kwenye fedha za ujenzi wa zahanati. Ilani yetu inazungumza kwamba kila Kijiji kiwe na zahanati; kila Kata iwe na vituo vya afya. Humu tuliomo ndani humu na wengine tunachagua mahali pa kwenda kupata matibabu, lakini mwananchi wa kawaida, maskini, hana hata mahali pa kwenda kupata matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati ni jambo la muhimu sana kujenga ili kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma hii. Sasa kama Ilani yetu inazungumza kwamba tuwe na zahanati kila kijiji, tuwe na kituo cha afya, wananchi wameshaandaa maboma ya kutosha, wanasubiri fedha za Serikali ili Serikali iwaunge mkono; tupelekeeni fedha hizo ili kupunguza matatizo ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali imekuja na mpango wa kupunguza kodi kwenye mazao, lakini nimeangalia kwenye zao la pamba; kilichoondolewa kile siyo tija kwa wananchi. Umeondoa mwenge, umeondoa kikao ambacho ni fedha ambazo zinalipwa na jina, ni hela kidogo sana hizo. Tunazungumzia shilingi 400,000 kwa jina; hiyo inaongeza nini kwenye bei ya pamba?
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo kodi mbalimbali cess za Halmashauri, kuna CDTF, mfuko wa kuendeleza zao la pamba; hizi zote inapashwa Serikali ifidie ili mkulima aweze kupata bei nzuri. Tusipofanya hivyo, zao la pemba linakwenda kufa. Sasa mnapozungumzia viwanda, kwa mazao yapi? Mnapozungumzia viwanda, kwa sababu viwanda vinavyoongeza ajira ni viwanda ambavyo malighafi yake ni pamba. Hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie ili tuweze kuona ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia wakulima wa pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko kodi ambazo Mheshimiwa Rais alikuwa anasema ataziondoa; kodi zenye kero, lakini naona kama hatujaziondoa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wana shida, akina mama ntilie, sokoni wauza nyanya na michicha wana shida. Tungeangalia jambo hili kwa mapana yake, upo ushuru hauna tija, hata Halmashauri haiongezei kitu chochote. Naomba anakapokuja kumalizia hapa atuambie, hizi kodi ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi, ushuru wenye kero, utaondolewa kwa namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie tu kuongeza usajili wa bodaboda. Hili ni kundi ambalo ni maskini sana, lakini ni kundi ambalo linarahisisha usafiri wa wananchi wetu vijijini ambako gari hazifiki. Yapo maeneo barabara haziko; wanaotusaidia ni hawa watu wa bodaboda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunapoongeza usajili maana yake tunataka kuwapunguza hawa watu. Kama tungeacha kodi ilie ile, ingechochea kuingiza bodaboda nyingi zaidi, ikachochea hao bodaboda kununua mafuta mengi zaidi na kuongeza uchumi wa nchi hii. Naomba hili nalo liondolewe; halina sababu na halina tija sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamezungumza suala la CAG, na mimi naendelea kusema nilikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, chombo hiki ni muhimu sana; chombo hiki ni cha kitaalam. Mheshimiwa Profesa Muhongo anasema haya ni mambo ya kitaalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama haya ni mambo ya kitaalam halafu tunayapunguzia fedha, itakuwa ni aibu. Halmashauri zitakuwa na hali mbaya na Wizara zitakuwa na hali mbaya. Naomba fedha ziongezwe ili tuweze kuhakikisha udhibiti wa fedha hizi tunazozipeleka, zinakuwa na uhakika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo duniani huwa hayajadiliwi. Suala la mafao kwa Wabunge ni jambo ambalo duniani halijadiliwi. Ku-maintain Jimbo ni sawasawa na kujenga kiwanda cha kati. Wabunge hawa wabishe. Ku-maintain Jimbo ni sawa na kujenga kiwanda cha kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba hili liondolewe mara moja, halina mjadala, halina nafasi ili kuhakikisha kwamba Wabunge hawa sio pensionable. Mbunge hapa akienda kupigwa dafrao, unaweza kumshangaa, ni hali ngumu. Naomba hili kwa kweli lisiingizwe, wala lisijadiliwe na liondolewe mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naendelea sasa kuipongeza Serikali, kazeni buti kukusanya kodi ili huduma za wananchi zipatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.