Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kidogo tu Wizara hii ya Maji. Nina mambo matatu tu ya kuchangia leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni mradi wa umwagiliaji wa Delta ya Lwiche ambapo jana nilizungumza na Waziri. Maana yake nilikuwa naitazama kwenye randama ya Fungu Na. 5, sijaiona vizuri; na baada ya Mheshimiwa Waziri kunihakikishia kwamba ipo, lakini bado sijaiona. Pili, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, pia sijaiona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ni mradi mkubwa kwa ajili ya kulima mpunga katika Manispaa ya Kigoma Ujiji. Ni mradi ambao utawezesha umwagiliaji kwenye hekta 3,000 na kuweza kuzalisha tani 15,680 za mpunga. Kwa hiyo, ni mradi mkubwa ambao unaweza ukaisaidia nchi kuondokana na tatizo la chakula lakini ni mradi ambao unaweza kwa kiasi kikubwa kupunguza umaskini na kuleta ajira ya kutosha kwa watu wa Manispaa ya Kigoma na Vijiji ambavyo vinazunguka Manispaa ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waziri katika majibu yake, katika maelezo yake na katika ufuatiliaji wake aweze kuona ni kwa nini mradi huu hauonekani waziwazi licha ya ukubwa wake, katika vitabu vyake vya Wizara, kwa sababu bajeti nzima ya umwagiliaji mwaka huu ni shilingi bilioni 30.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu peke yake una thamani ya Dola za Kimarekani milioni 15. Kwa hiyo, ni zaidi ya bajeti nzima ya umwagiliaji katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kwa hiyo, naomba jambo hili Mheshimiwa Waziri aweze kulifuatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni mradi ambao utafadhiliwa na Serikali ya Kuwait kupitia Kuwait Fund na tayari Wizara ya Mambo ya Nje imeshakubaliana na Serikali ya Kuwait na nadhani kutakuwa na tatizo la kimawasiliano kati ya Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Fedha na Wizara ya Maji. Naomba Mheshimiwa Waziri alifuatilie jambo hili ili mradi huu uweze kuanza haraka iwezekanavyo. Watu wa Wizara ya Kilimo tayari wameshamaliza kutengeneza feasibility study na ninaweza nikampatia Mheshimiwa Waziri pia aweze kuiona kwa sababu ninayo hapa. Naomba tu aweze kwenda kuifuatilia vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nililokuwa napenda kufahamu, ni kuhusiana na mradi wa maji katika Manispaa ya Kigoma. Katika kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 53 ibara ya 123, ameelezea kwa kina kuhusu mradi huu. Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba mradi huu ulikuwa uishe toka mwezi Machi, 2015. Mpaka sasa kwa mujibu wa taarifa ya Waziri, mradi huu umefikia asilimia 50. Kwa mujibu wa mkataba, mradi ulipaswa kwisha mwezi Machi, 2015. Waziri anasema mradi sasa utakamilika mwezi Oktoba, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tuna tatizo! Tuna tatizo la Wakandarasi wanaopewa miradi ya maji; siyo Kigoma peke yake. Sehemu nyingi ya nchi, Wakandarasi katika Wizara ya maji ni watu ambao wamekuwa wakichelewesha kumaliza miradi. Mfano, mzuri ni Mkandarasi ambaye amepewa mradi huu wa maji wa Kigoma SPENCON.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaelezwa kwamba Mkandarasi huyu alitumia fedha za mradi wa maji Kigoma kwenda kulipa madeni aliyokopa kwenye miradi aliyokuwa nayo nchi ambazo ni tofauti na Tanzania, lakini katika hotuba ya Waziri, sioni uwajibikaji ambao unafanywa kwa huyu Mkandarasi, kwa sababu wananchi wamehangaika, hawana maji, Mkandarasi alipaswa awe amemaliza mradi huu, lakini mpaka sasa hivi mradi huu haujakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, pamoja na maelezo haya kwamba mradi utakamilika mwezi Oktoba lakini mradi huu umechelewa, tunapaswa kupata maelezo, ni hatua gani zimechukuliwa dhidi ya Mkandarasi ambaye alipewa mradi huu? Kwa sababu tusipochukua hatua kwa Wakandarasi wa namna hii, tutapiga kelele hapa, tutapendekeza kuongezeka kwa tozo mbalimbali, fedha zitapatikana, lakini kwa Wakandarasi wa aina hii maana yake ni kwamba fedha zile tunakwenda kuzipoteza na wananchi wetu wala hawatapata maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nipate maelezo ya Mheshimiwa Waziri kwamba ni hatua gani zinazochukuliwa kwa Wakandarasi wa namna hii. Mtu ambaye amepewa Mkataba, hajautekeleza, kwa nini tuwabembeleze Wakandarasi wa namna hii na wananchi wetu wanazidi kuumia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba jambo hili Mheshimiwa Waziri alitolee ufafanuzi wa kutosha kabisa kwa sababu ni jambo ambalo linawaudhi sana watu wa Kigoma, mradi huu wameusubiri kwa muda mrefu sana. Viongozi walikuwa wanakuja Kigoma, wanapokelewa na ndoo za maji kwa sababu ya kero ya maji katika mji wa Kigoma na mradi huu ndiyo ulikuwa unakwenda kumaliza kabisa kero hii ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nipate maelezo ya kutosha kabisa na siyo maelezo tu ya kueleza kwamba, mradi umefikia asilimia ngapi; mradi ulikuwa uishe mwezi Machi, 2015, mpaka sasa hivi mradi haujakwisha, una asilimia 50. Ni hatua gani ambazo zimechukuliwa dhidi ya Mkandarasi na dhidi ya watu ambao walikuwa wanasimamia mkataba huu ili kuhakikisha kwamba jambo hili linaweza likaisha? Nakubali kwamba liishe mwezi Oktoba lakini ni lazima tuchukue hatua dhidi ya Mkandarasi ambaye amechelewesha mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo nataka kulizungumzia ni suala la Wakala wa Maji Vijijini. Hili ni jambo ambalo lina muafaka. Mheshimiwa Mwambalaswa amezungumza hapa; Serikali, Kamati na Kambi ya Upinzani Bungeni, vyote vimekubaliana na jambo hili, hakuna sababu ya kulichelewesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona faida kubwa ambayo tumeipata kwa kuwepo kwa REA na mafanikio makubwa ya REA yamepatikana baada ya Bunge hili kufanya maamuzi ya tozo ya mafuta ya taa kuielekeza REA. Ndiyo mafanikio ambayo tunayaona kwenye REA. Ni matunda ya kazi ya mapendekezo ya Wabunge katika Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Waheshimiwa Wabunge wanapendekeza tuwe na Wakala wa Maji Vijijini. Wakala huu uhangaike na maji tu. Tuupe fedha za kutosha, fedha ziwe ring fenced, uhangaike na maji tu. Kuendesha miradi ya maji kwa kutegemea Wizara peke yake, haitatusaidia sana. Tumeona muda wote huu tumefanya hivyo na hatujaona mafanikio makubwa. Kuna nyongeza imefanyika kwa watu kupata maji, lakini bado kasi yake haitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, tusimalize Mkutano huu wa Bajeti bila kutoka na Wakala wa Maji Vijijini. Wakala huu hauhitaji sheria, kwa sababu tuna mifano tayari. Unachukua tu templet ya uanzishwaji wa REA, unaiboresha, unatoa umeme, unaweka maji, unaweka utaratibu wa fedha zake kupatikana, tunaondoka hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuja kwenye Miswada ya kifedha itakayokuja baadaye, tuondoke na Wakala wa Maji Vijijini. Mheshimiwa Waziri ateue watu wazuri, awapeleke kule waendeshe Wakala huu tuondokane kabisa na kero ya maji kwa wananchi wetu. Ni aibu kubwa sana kwamba mpaka leo hii tunapozungumza, kuna baadhi ya wananchi wetu wanakunywa maji na mifugo katika sehemu nyingi za nchi yetu na sisi Waheshimiwa Wabunge tunajua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waheshimiwa Wabunge wote, kwa sababu tuna consensus kwenye jambo hili, tuondoke na Wakala wa Maji Vijijini. Wakati Bunge linaahirishwa hapa, Waziri Mkuu anafunga Bunge, tunaondoka na Wakala wa Maji Vijijini. Tutakuwa tumepiga hatua kubwa, tutakuwa tumewasaidia wananchi wetu na tutaingia kwenye historia kama tulivyoingia kwenye historia ya kuhusu REA na kodi ya mafuta ya taa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.