Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Salma Mohamed Mwassa

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SALMA M. MWASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai, lakini vilevile naomba nichangie Wizara hii muhimu ambayo inagusa maisha ya Watanzania kwa kiasi kikubwa hasa wanawake na watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichangie kuhusu upungufu wa maji Jijini Dar es Salaam. Pamoja na jitihada za Serikali za kupanua Mtambo wa Ruvu chini na Ruvu juu lakini bado Jiji la Dar es Salaam lina uhaba mkubwa wa maji. Ninyi wenyewe Waheshimiwa Wabunge asilimia 90 ni Wakazi wa Dar es Salaam; nafikiri ninapoongea hilo, mnanielewa vizuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna uhaba mkubwa wa maji na maji kuwa bidhaa adimu hasa katika maeneo ya pembezoni kama maeneo ya Makabe, Maramba Mawili, Msigani, Kiluvya, Kibamba, Msakuzi, Mabwepande, Bunju na mengineyo ya pembezoni. Yaani maji katika maeneo hayo ni bidhaa adimu mno! Lita 1,000 zinauzwa kati ya 20,000 mpaka 30,000 kwa ujazo wa tank la lita 1,000. Sasa mwananchi huyo ukipiga hesabu kwa mwezi anatumia kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie huu mradi ambao alisema kwenye hotuba yake katika ukurasa wa 69 kwamba utagharimu Dola za Marekani milioni 32; atuambie utaanza lini na utakamilika lini? Kwa sababu Wananchi wa Dar es Salaam jamani wanateseka kwa kiasi kikubwa. Hivi mkoa mkubwa kama ule, maana yake unapoongelea Tanzania unaongelea Dar es Salaam; mpaka leo miaka 54 ya Uhuru kuongelea uhaba wa maji, kwa kweli ni tatizo kubwa na siyo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niongelee kuhusu upotevu wa maji. Upotevu wa maji katika Jiji la Dar es Salaam ni mkubwa mno kutokana na uchakavu wa miundombinu. Mabomba mengi yamechakaa, sasa Mheshimiwa Waziri anaposema upanuzi wa huu mtambo wa Ruvu Chini na Juu, obvious utaleta maji mengi sana Dar es Salaam lakini hujatuambia ukarabati mkubwa utakuwaje nao, kwa sababu siku ambayo ni ya maji Dar es Salaam, ni mafuriko. Barabara zote zinaharibika kutokana na uvujaji wa haya mabomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa huu ukarabati wa miundombinu ufanyike kwa haraka. Vile vile ni wazi kwamba, ongezeko la maji safi kutokana na mradi huu mkubwa wa maji utaendana kabisa na wingi wa maji taka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie miundombinu ya majitaka, kwa sababu majitaka ni tatizo Dar es Salaam. Yaani kila unapopita ni mafuriko hasa katika maeneo ya Tandale, Hananasifu, Kinondoni, Tandika, huko ni hatari! Ndiyo inasababisha mlipuko wa magonjwa kama kipindupindu mara kwa mara. Mfumo wa Majitaka kwa kweli Dar es Salaam ni tatizo, naomba aliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nijikite kwenye suala la maji mashuleni. Uhaba wa maji mashuleni katika Mkoa wa Dar es Salaam pia ni tatizo. Wanafunzi wetu wanahangaika mno, hasa shule za msingi, hawana maji kabisa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie kama kuna uwezekano wa kuwatengenezea mfumo wa maji ya mvua kabla ya hii miradi ya kusambaza maji haijafika mashuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, haya maeneo ya pembezoni niliyotaja hapo mwanzo, mashuleni watoto hata maji ya kunywa hawana. Kwa hiyo, naomba kabla ya kuangalia hiyo miradi mikubwa ya kusambaza maji, lakini Mheshimiwa Waziri angeangalia mradi mbadala wa kuvuna yale maji ya mvua waweze kujengewa ma-tank, watoto waweze kunywa maji, wawe kwenye mazingira yaliyo sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nikiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, kuna Taasisi za Serikali kuwa wadaiwa sugu. Wanadaiwa karibu shilingi bilioni 29, hili ni tatizo. Ukiangalia, siyo wananchi tu ambao hawalipi; hizi Taasisi za Serikali ndiyo zilitakiwa zioneshe mfano mzuri. Sasa Mheshimiwa Waziri wanamwangusha, kwa sababu kama anawapelekea maji halafu hawapili, yeye atafanyaje kazi? Naomba hii iwe mfano kabisa kwamba sisi kwanza tulipe, hizi Taasisi za Serikali ziwe mfano wa kulipa maji ili tunapokwenda kwa mwananchi, tunapomwambia kwamba lazima ulipe maji, sasa na yeye asiwe na mfano kwamba mbona Taasisi za Serikali hazilipi maji? Itakuwaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kabisa Mheshimiwa Waziri afuatilie, waweze kumlipa, la sivyo watamwangusha na ataitwa mzigo, kumbe wao wenyewe ndio wanaomwangusha. Ahakikishe madeni yao yote yamelipwa vizuri. Wasipolipa, aweke zile mita zake kama za Luku; lipa maji kadri utumiavyo. Kwa nini wamwangushe, anawapa tu maji mpaka wanamaliza, bado yeye hajalipwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niongelee tena kuhusu upungufu wa hawa wataalam wa maji. Kwa kweli wataalam wa maji ni wachache na ndiyo maana hata elimu ya maji mbadala inakuwa ngumu. Kwa hiyo, naomba kabisa, Wizara hii iajiri wataalam wa maji kwa kiasi kikubwa. Wataalam wa maji wangeweza kwenda kule maeneo ya pembezoni wakawafundisha hata jinsi ya kuchimba visima, wakaelimisha watu njia mbadala za kupata maji kabla pale ambapo yale maji ya Serikali bado hayajafika. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri aangalie kabisa ni kiasi gani atapata hiiā€¦
MWENYEKITI: Ahsante.