Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kiswaga Boniventura Destery

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Magu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Maji kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameiwasilisha. Kwa kweli imesheheni mambo mengi ambayo yakitekelezwa yatatatua kero za Watanzania na kidogo sana katika Jimbo la Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, Magu kwa ujumla ina shida ya maji, miaka yote tumekuwa na shida ya maji. Kilio kikubwa cha Wan-Magu ni maji, mpaka najiuliza kwamba Wilaya ya Magu imekosea nini, imeikosea nini hii nchi mpaka tupate matatizo makubwa ya maji kiasi hicho ambapo Wilaya ya Magu imezungukwa na maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Waziri nimeona mradi mkubwa wa maji Magu Mjini, ambao utasaidia wananchi wa Magu wapatao 36,000, lakini wananchi 340,000 hawatakuwa na huduma ya maji, ninasikitika sana na ukizingatia kwamba hata Wilaya ambazo zinanizunguka majirani zangu kwa maana ya Wilaya Bariadi ambako wewe uko, nayo haina maji, Wilaya ya Busega nayo haina maji, Wilaya ya Kwimba nayo haina maji. Kwa hiyo, najikuta niko katikati pale hata majirani hawawezi kunisaidia, wewe unajua kabisa kwamba bhuzengano bhutikubhwaga makira. Lakini huo uzengano hauna chochote napata taabu sana, yaani kwamba ujirani huwa haunyimani mambo mazuri manono. Kwa hiyo, napata taabu kwa sababu majirani zangu hawana maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa maji kwa kweli kama hotuba inavyosema kama kweli wakandarasi wameshapelekewa vitabu, kama kweli unaweza kuanza mwaka huu utarudisha imani kwa wananchi wa Magu kwamba sasa wanaanza kupata huduma ya maji. Lakini kama nilivyosema wananchi 340,000 bado wanakunywa maji ambayo wanachangia na ngo‟mbe, mbwa na fisi huko vijijini, wana shida kubwa ya maji. Ni vema katika Mji wa Kabila ambao wewe unaujua vizuri Mahaha, Ng‟haya, Nkhobola Serikali ikawa na mpango mzuri wa kuwafikishia maji wananchi hawa hata kama siyo bajeti hii kwa sababu naona bajeti hii imelenga kutekeleza miradi hii, bajeti ijayo nifikiriwe vizuri zaidi katika Wilaya ya Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kijiji cha Nyang‟hanga ambacho kimetoa Wabunge wa Nne tangu Magu ianze kupata Wabunge, wote wanatoka kijiji hiki cha Nyang‟hanga hakina maji. Kijiji hiki Mheshimiwa Dkt. Festus Bulugu Limbu alifanikiwa kuchimba visima virefu vya maji, vina maji mengi ya kutosha kwa ajili ya kusambaza katika kijiji hiki cha Buhumbi pamoja na kijiji cha Nyang‟hanga, lakini kila mwaka nina- declare interest kuwa nilikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri tulikuwa tukiomba maombi maalum ya shilingi milioni 700 ili mradi huu uweze kusambaza maji hatukupatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri anihurumie Jimbo la Magu, atuhurumie kijiji hiki atafute fedha mahali popote ili aweze kutusaidia shilingi milioni 700 tuweze kusambaza maji katika kijiji cha Nyang‟hanga na Buhumbi.
Tunao mradi ambao unaendelea wa Sola Bubinza, huu ni mradi ambao umeanza tu lakini umekosa fedha, Wizara inajua, Katibu Mkuu anajua na Mheshimiwa Waziri anajua. Ninamuomba sasa kwa sababu ni mradi ambao ulikuwa unaendelea kuliko kupoteza fedha nyingi za walipa kodi wa nchi hii, tupewe fedha kwenye bajeti hii ili mradi huu uweze kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika sana, mradi huu unaopeleka maji Magu chanzo chake kinatoka Kata ya Kahangala, kijiji cha Bugabu. Lakini Makao Makuu ya Kata ambayo ni kilometa nane tu kutoka pale chanzo kilipo au bomba litakapopita hakimo kwenye mpango wa kuwekewa maji, hii ni haki kweli? Niombe Waziri atafute kila linalowezekana ili Makao Makuu haya ya Tarafa ya Kahangala ambako maji yanatoka yaweze kupata maji ni hela kidogo tu. Naomba sana Mheshimiwa Waziri asaidie jambo hili. Tunayo Kata ya Mwamanga ambayo nayo ilikuwa na Mradi wa Matokeo Makubwa sasa wa awamu iliyopita. Kuna miradi ambayo ilianza lakini fedha zake hazijapatikana, niombe kwenye bajeti hii ni vizuri tukamaliza viporo ambavyo vilikuwa vimeanzishwa ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi wa Lugeye Kigangama, Mheshimiwa Waziri alifika kwenye mradi huu na Mheshimiwa Lubeleje pia alifika kwenye mradi huu. Unadaiwa shilingi milioni 94 tu ukamilike, chonde chonde naiomba Serikali yangu ya kazi, Serikali ya Awamu ya Tano itupe hizo shilingi milioni 94 ili mradi huu uweze kukamilika. Tuna kiangazi kikubwa sana, kwa kweli katika Wilaya ya Magu la sivyo tutapata taabu haingii akilini, kwamba shilingi milioni 94 zinakosekana ili mradi huu uweze kukamilika maji yameshavutwa yameshaletwa kwenye tank ni kusambaza tu kuunganisha koki mbalimbali, naomba nisaidiwe na Serikali hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Sanjo inazungukwa na maji lakini haina maji, na Tarafa ile inaongoza kwa kupata kipindupindu kwa sababu wanatumia maji ambayo hayajatibiwa, Tarafa ile ina Mji wa Kisesa, Mji wa Bujola bado una shida kubwa ya maji. Population ya pale inazidi hata Makao Makuu ya Wilaya ya Magu. Ninaomba angalau utafutwe mradi ambao unaweza kutokea Ilemela, Buswelu, Nyamongolo ulete maji katika Mji wa Kisesa, lakini hata Lutale, Kongolo pamoja na Chabula nao wanahitaji maji haya ya kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, ninajua kwamba fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya maji ni kidogo, lakini zitaleta impact sana kama miradi hii itatekelezwa. Tuombe mahala ambapo sisi hatujapata fedha tufikiriwe sana bajeti ijayo ili tuwemo kwenye utaratibu wa kusaidiwa miradi hii ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Ziwa imebaki kuwa jina tu, Wilaya zake zote hazina maji tunahangaikia Sengerema…
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Ahsante sana.