Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utazidi kuwashawishi Waheshimiwa Wabunge kwamba kuna umuhimu wa kuunga mkono bajeti hii kwa sababu inaanza safari ambayo tulikuwa hatuna. Michango ya Wabunge wengine wamesema kwamba mjusi arudishwe, mjusi wetu, naomba niwapatie ufafanuzi kidogo kuhusu huyo mjusi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mjusi huyu dinosaur ameanza kupatikana kwenye dunia yetu miaka milioni 231.4 iliyopita na yeye ndiye aliyekuwa kiumbe muhimu kwa zaidi ya miaka 135 iliyofuata. Mjusi huyu ana uzito wa kilo kati ya tani 50 na tani 70, urefu wake unatofautiana, lakini anaweza kuwa na urefu ambao unalingana na ghorofa sita. Mjusi wetu yuko Humboldt Museum ambayo zamani ilikuwa Ujerumani ya Mashariki, mimi nilikuwa naishi Berlin ya Magharibi yaani Ujerumani Magharibi. Nimeenda pale mara nyingi, nadhani zaidi ya mara mia moja.
Waheshimiwa Wabunge, nataka kuwaeleza ukweli ni kwamba hatuna uwezo wa kumrudisha na hatuna uwezo wa kumtunza, huo ndiyo ukweli kabisa. Tunachopaswa kufanya ni kujadiliana namna ya kupata yale mapato tugawane na Serikali ya Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri wengine ambao tunafahamu yote hayo, siyo kwamba majadiliano hayajaanza, majadiliano tumeyafanya nadhani hata miezi miwili nyuma, nilikuwa najadiliana na Balozi wa Ujerumani na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani namna ya kuweza kupata hilo pato. Ndugu zangu ukitaka kujua kwamba hatuwezi siyo kwamba tunahitaji muda kufikia hiyo ngazi hiyo, ukienda kwenye museum yetu Nyumba ya Makumbusho hii ukiangalia na kuangalia museum zingine duniani, utaona kuna tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huyu mjusi tunafahamu na hawa mijusi (dinosaurs) wako familia zaidi ya 15, hawapatikani kwetu tu wanapatikana dunia nzima ndiyo maana kuna Jurassic Park. Kwa hiyo, tumuombe Mheshimiwa Waziri na wengine ambao tuna-connections huko tuendelee na mjadala wa kugawana yale mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mgogoro wa wakulima na wafugaji. Ndugu zangu tulioongea hapa tumeona kuna mwingine anavutia wafugaji, mwingine anavutia upande wa wakulima, vitu hivi lazima tuvikubali. Miaka 50 ijayo watakaokuwa kwenye hili Bunge, tuliyoyajadili hawatayajadili kwa namna hiyo, kwa sababu tuna imani watakuwa na kilimo bora, watakuwa na ufugaji bora, hawatakuwa watu wanajadili ukubwa wa maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sayansi inakokwenda inataka eneo linalolingana na hili Bunge letu liweze likalisha Mkoa mzima kwa mwaka mzima, ndiko huko tunakokwenda sayansi inatupeleka huko, maana yake kuna C4 plants na C3 ambayo inatumia carbon dioxide nyingi, mimea inakua kwa haraka sana, mtu anavuna mara tatu, mara nne, mara tano. Sasa suala siyo eneo, hapa ugomvi wetu kwa wakulima na wafugaji tatizo siyo eneo, tatizo ni matumizi madogo sana ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Watanzania mwaka 1950 tulikuwa watu milioni 7.7, mwaka jana tumefika milioni 53.5, mwaka 2050 tutakuwa watu karibu milioni 138 eneo ni lilelile la ukubwa wa 0.97 square kilometers million. Sasa tatizo hapa siyo maeneo, tatizo ni deployment of science, innovation na technologies ndiyo tatizo. Kwa hiyo, bajeti ya Mheshimiwa Profesa Maghembe tuipitishe tujipange kutumia sayansi na ubunifu zaidi kuliko kugombania ukubwa wa maeneo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia takwimu zinavyoonesha, kilimo chetu cha pamba hekta moja Tanzania tunatoa kilo 147, Malawi kilo 269, China kilo 1,524, Brazil kilo 1,530 hapa tatizo siyo eneo. Kwa hekta moja mwingine anazalisha zaidi. Mahindi juzi Namibia ambayo ni jangwa wamefikisha tani 11 kwa hekta moja, Tanzania bado tuko chini kabisa. Mihogo nchi ya Niger ni nchi jangwa kabisa, Niger wao wanazalisha tani 22 za muhogo kwa hekta moja, Tanzania tuko chini ya tani 10. Hivyo, Waheshimiwa Wabunge tatizo hapa siyo maeneo tusimalizane, tatizo hapa ni utumizi mdogo wa sayansi, teknolojia na ubunifu, kwa hiyo Mheshimiwa Maghembe bajeti yake tuipitishe tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maziwa, hawa ng‟ombe tunaowapigania wafugaji hatuna ng‟ombe wazuri. Nimechukua aina mbili tu za ng‟ombe wanaojulikana duniani kwa kutoa maziwa mengi. Mmoja anaitwa holstein yeye anatoa lita 11,428 kwa mwaka, wa kwetu hapa mzee sijui lita ngapi, Mheshimiwa Nsanzugwanko wewe ndio unafahamu mfugaji.
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata tatizo kwa wafugaji hapa siyo eneo, tatizo ni sayansi, technology na ubunifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu nyama hapa, tatizo siyo kumtengea mtu pori la kuwinda, mnyama wa kileo hii yaani tukichukua ng‟ombe, unapaswa kumfuga afikishe kilo zaidi ya 500, nyama anayoweza kuitoa bila mfupa, bila makongoro, bila nini ni kilo kati ya 340 na kilo 360. Kwa hiyo, ndugu zangu hii Wizara tuipatie bajeti, sisi wenyewe tujue kwamba matumizi yetu ya sayansi ni madogo, ndiyo maana tunagombania maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.