Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) ni miongoni mwa mashirika ya umma yenye kulisaidia Taifa kupata fedha nyingi za kigeni. Utalii nchini mwetu unachangia asilimia 18 ya GDP na sasa kiasi hiki kinaweza kuongezeka zaidi. Jambo la ajabu, TANAPA kwa miaka zaidi ya mitatu sasa haina Bodi ya Wakurugenzi. Mambo yote yamekuwa yakiamriwa na viongozi wa Wizara yaani Waziri na Katibu Wakuu waliopita na waliopo sasa. Hii ni hatari kwa shirika kama hili lenye fedha nyingi zinazohitaji utaratibu wa Bodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujangili unashamiri, idadi ya wanyamapori ni kubwa mno. Tembo wako hatarini kutoweka licha ya juhudi za Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama katika kukabiliana na hali hiyo. Majangili wana silaha hasa katika mapori kama ya Ugalla, Moyowosi, Loliondo na mengine mengi. Mbaya zaidi sheria haziruhusu walinzi wa kampuni zenye vitalu vya uwindaji katika mapori ya akiba na WMA kuwa na silaha. Hali hiyo imesababisha majangili watambe. Kwa nini Mheshimiwa Waziri asilete sheria Bungeni ili walinzi hao wapewe silaha na kwa hiyo, wasaidiane na wale wa TANAPA na wa wanyamapori kukabiliana na ujangili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, adhabu kwa majangili zisiwe faini, bali ziwe hukumu za kifungo cha maisha. Kenya wana sheria kali zinazosaidia sana kulinda wanyamapori wao. Kwa mfano, wao mtu akipatikana ndani ya hifadhi kinyume cha sheria, wanampiga risasi. Sisi tunaweza tusiwe na adhabu ya aina hiyo, lakini wakati umefika kwa Serikali kuleta hapa Bungeni mabadiliko ya sheria ili majangili wajue tumedhamiria kukomesha vitendo vyao. Serikali isiwe na kigugumizi cha kuwashughulikia viongozi wanaotajwa kuwa ni washiriki wakuu wa ujangili. Yapo maneno kuwa hata miongoni mwetu Waheshimiwa Wabunge kuna majangili. Kama kweli wapo, ni vizuri sheria zikatekelezwa badala ya kuendelea kuwaaminisha wananchi kwa maneno tu kuwa kuna Waheshimiwa Wabunge majangili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka kadhaa iliyopita kulitokea mvutano kuhusu ada wanazopaswa kulipa watu wenye hoteli (concessions fee). TANAPA walifungua kesi katika Mahakama Kuu na kushinda kesi hiyo. Ikaamuliwa wenye hoteli walipe, lakini utekelezaji wake ulipaswa uanze kwa Bodi kukaa na kupanga viwango vya ada hiyo. Sasa miaka zaidi ya mitano uamuzi huo haujatekelezwa na haujatekelezwa kwa sababu hakuna Bodi. Kwa kutoweka ada hizo, TANAPA wanapoteza wastani wa shilingi bilioni 10 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ahakikishe anamshawishi Mheshimiwa Rais mapema iwezekanavyo ili Bodi ya TANAPA iundwe; na kwa kufanya hivyo, iweke viwango vya ada na utekelezaji uanze mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo katika mapori ya akiba, mapori tengefu, WMA na Hifadhi za Taifa ni mingi sana. Mapori kama Maswa, Moyowosi, Kijeleshi, Ugalla yanaelekea kufa. Pori tengefu la Loliondo limevamiwa na malaki ya mifugo kutoka nchi jarani (Kenya). Loliondo ni kama imekufa. Shughuli za kibinadamu zikiwamo za kilimo ni kubwa mno. Wanyamapori wamekimbia, Loliondo hii ni buffer zone ya Serengeti na eneo ambalo ni mazalia ya nyumbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifugo imekuwa mingi sana kiasi cha kufikia hatua sasa ya kuona hatari siyo ujangili tu, ila mifugo katika mapori ya hifadhi. Pamoja na umhimu wa mifugo katika nchi yetu, Serikali isisite kutekeleza Operesheni Ondoa Mifugo ambayo imepangwa kuanza tarehe 15 Juni, 2016. Bila kufanya hivyo rasilimali wanyamapori itatoweka katika nchi yetu na hii itakuwa aibu kubwa kwa kizazi kijacho na ulimwengu kwa jumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuweke kando siasa na tujikite kwenye uhifadhi. Faida za uhifadhi ni kubwa; kwa mfano, nyati mmoja anayewindwa anaiingizia Serikali zaidi ya shilingi milioni tatu. Simba mmoja anaingiza zaidi ya shilingi milioni 10. Kwa hiyo, tusiifanye mifugo ikawa mbadala wa wanyamapori kwa sababu faida yake ni kwa wachache wenye kuimiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni Gazeti la Jamhuri lilitoa makala ikionesha vibanda vibovu kabisa vya kukusanya mapato kutoka kwa watalii katika maeneo ya Oldonyo Lengai na Engaruka. Ile ni aibu kubwa kwa sababu vibanda vyenyewe vimeshikiliwa na nguzo za miti visianguke. Hata watalii watatushangaa kuona dola zinakusanywa kwao na watu walio kwenye vibanda vibovu. Ingawa vibanda hivyo vipo chini ya Halmashauri za Longido na Monduli, bado Wizara ya Maliasili na Utalii inapaswa kuitazama aibu hii na kuiondoa kwa sababu watalii hawazijui Halmashauri hizo, isipokuwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya mkaa inashamiri sana. Misitu inamalizwa na sababu inayotolewa ni kuwa bei ya gesi au nishati mbadala ni kubwa. Ingawa suala hili la mkaa ni mtambuka Kiwizara, bado ukweli unabaki kuwa mkaa mwingi unatolewa katika mapori yanayohifadhiwa kisheria chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Mbaya zaidi, hata huo mkaa unaouzwa watu wengi hawalipi ushuru. Malori ambayo kisheria hayaruhusiwi kusafirisha mkaa, leo yanasafirisha hadi kwenye makontena nyakati za usiku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pale Dar es Salaam watumishi wa Wizara wakae kwenye maegesho pale kwa Msuguri ili kuyakamata malori yote yanayopakia na kusafirisha mkaa bila vibali wala kulipa ushuru. Watumishi wa Wakala wa Vipimo wapo hapo sasa wakidhibiti upakiaji wa lumbesa kwa mazao kutoka mikoani. Sioni kwa nini Wakala wa Misitu nao wasikae hapo kwa Msuguri ili kuyadhibiti malori haya yanayotumika kutenda makosa haya ya uhifadhi.