Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo na mimi niwe miongoni mwa wachangiaji katika hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa hapa Bungeni tarehe 20 Novemba, 2015 hapa Bungeni. Awali ya yote, naomba
kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya; na niwaombe sana Watanzania wote tumwombee na tumtakie heri aweze kutimiza malengo yake kwa faida ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana wananchi wa Mvomero kwa kunikumbuka tena kwenye ufalme wao, hatimaye nimerudi tena mjengoni. Nawashukuru sana na ninawaahidi sitawaangusha. Nawaahidi wananchi wa Mvomero sitawaangusha, ujinga ni pa kwenda siyo pa kurudi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana nichangie hotuba ya Mheshimiwa Rais katika maeneo mbalimbali na pia nimpongeze kwa juhudi kubwa aliyoianza katika kuboresha uchumi wa Taifa, katika kupambana na mafisadi, katika kuboresha mapato ya nchi yetu. Bado tuna
mianya mingi, bado tuna kazi kubwa ya kumshauri na kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu. Yapo majipu mengine yeye hayajui, sisi tunaoishi na wananchi, tunaokaa kwenye Halmashauri tunayafahamu, ni wajibu wetu tumsaidie ili sasa turudi kwenye mstari. Taifa hili lina kila aina ya
neema, ni nchi ambayo ina baraka kubwa za Mwenyezi Mungu. Tuna maziwa, tuna madini, tuna bahari, tuna ardhi kubwa, ni nchi ambayo inatakiwa isonge mbele kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na suala la wakulima na wafugaji. Katika Taifa letu lipo tatizo kubwa la wakulima na wafugaji hasa katika Wilaya yangu ya Mvomero. Eneo hili linahitaji kazi ya ziada. Nami napenda kuishauri Serikali kupitia kwa Wizara ya Ardhi, Wizara ya
TAMISEMI, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Mifugo na Kilimo na Wizara ya Maliasili zishirikiane kwa pamoja. Hawa wote ni wadau wakubwa katika eneo hili la kuondoa tatizo la wakulima na wafugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna tatizo kubwa kwenye maeneo yetu lakini bado tuna maeneo ambayo ni hifadhi. Hifadhi zile zinabaki kuwa hifadhi, lakini baadhi ya maeneo ya wakulima wanahangaika, wafugaji wanahangaika, hifadhi nyingine hazina tija kwa Taifa letu. Namwomba sana Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kama Waziri wa Kilimo, aliangalie hili, ashirikiane na wadau wenzake, tuwapatie maeneo wafugaji, tuwapatie maeneo ya ziada wakulima na tuweke sheria thabiti kuondoa maafa, kuondoa machafuko kati ya wakulima na wafugaji. Tukiweka utaratibu huo mzuri, nasi kwenye Halmashauri zetu tukatengeneza sheria za kuwadhibiti tutaleta maendeleo ndani ya kilimo, ndani ya ufugaji. Kwa kuwa muda ni mdogo, naomba niende haraka haraka.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niingie kwenye suala la uchumi. Naiomba sana Serikali ifanye kazi ya ziada kwa kuhakikisha kwamba tunaweka sera nzuri za kuendelea kuwatambua wafanyabiashara, kwa maana ya sekta binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna nchi yoyote duniani ambayo imesonga mbele kiuchumi bila sekta binafsi. Sekta binafsi ni mhimili mkuu wa Taifa. Sekta binafsi inaweza ikaongeza pato la nchi yetu, lakini katika sekta binafsi wapo wafanyabiashara wana upungufu.
Ni vyema sasa tukaweka utaratibu mzuri, tushirikiane na sekta hii kukuza viwanda na uchumi wetu. Yapo mambo mengi kwenye sekta binafsi yanatakiwa yashughulikiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kwamba Mheshimiwa Rais ana ndoto kubwa ya viwanda katika Taifa letu. Tatizo lililopo katika suala zima la viwanda ni sera za nchi yetu. Yapo maeneo sera zinatubana. Ni vyema tukakaa tukarekebisha sera zetu, tukaangalia
wapi tulikosea, wapi tupo na mabadiliko ya dunia ya leo yanasemaje. Tukibadilika katika utaratibu huo, sasa tunarudi kwenye kuanzisha na kusimamia viwanda. Hapo tutasonga mbele kwa hatua kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa waaminifu. Naomba wanaohusika na masuala ya bajeti, wanaohusika na masuala ya uchumi, mfanyabiashara mwenye kiwanda cha mafuta ana-declare analeta crude oil kumbe anadanganya analeta semi. Hawa ndio ambao wanadunisha, viwanda haviendelei, tunarudi nyuma, wao wananufaika. Wanacheza na Kamati ya Bajeti, wanacheza na wahusika, wanaingiza mambo yao kwenye bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nina imani na wewe, najua uzoefu wako, anza kupambana na mambo haya katika bajeti ya mwaka huu. Usiruhusu wenye viwanda vya ndani walete udanganyifu. Tunachotaka, uchumi ukue tupate maendeleo.
Mvomero tunahitaji barabara ya lami ikamilike, Mvomero tunahitaji umeme ufike vijiji vyote, Mvomero tunahitaji leo maji yafike maeneo yote. Lakini maji yale hayatafika kama uchumi utalegalega. Tutaisaidia Serikali, tutakaa na Mawaziri, dakika kumi hazitoshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la umeme. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri mhusika, lakini ushauri wangu katika suala la umeme tuongeze nguvu zetu katika kuzalisha umeme wa maji na umeme wa gesi badala ya kutegemea umeme wa mafuta
ambao unawanufaisha wafanyabiashara na Taifa tunabaki nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono juhudi zote, umeme wa maji, umeme wa gesi na umeme wa mafuta haufai, haufai, haufai! Umeme wa mafuta ni biashara ya wakubwa. Wamejiandaa, wana mambo yao, wanafanya kazi zao. Sisi tuongeze nguvu kwenye gesi, maji
na kwenye umeme wa upepo. Najua bado dakika zinaniruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la vocha za mbolea. Kuna tatizo kubwa sana vijijini, kuna watendaji ndani ya Serikali ndani ya Halmashauri zetu sio waaminifu. Baadhi yao vocha hizi wananufaika wao badala ya kumnufaisha mkulima wa kijijini.
Mheshimiwa Mwigulu nakuaminia sana, umefanya kazi nzuri na unaendelea kufanya. Tuendelee kukusaidia kama Wabunge ili uboreshe eneo hili kwa faida ya nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uchaguzi wa Zanzibar ni suala la kisheria. Tuwatakie Wazanzibar uchaguzi mwema. Wanaopiga kelele, waendelee kupiga kelele, uchaguzi umetangazwa unarudiwa. Mheshimiwa Rais hawezi kuingilia tena. Tume ya Uchaguzi Zanzibar
imetangaza uchaguzi urudiwe, tuwatakie uchaguzi mwema tarehe 20 Machi. Tutampata ambaye atachaguliwa kwa haki. Mizengwe mizengwe iliyokuwepo nyuma ndiyo imesababisha uchaguzi ule umefutwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwe wa kweli. Sasa hivi tumtakie mema Rais wetu afanye mambo mengine makubwa, tusimchanganye. Tumepata Rais ambaye anaweza kutuvusha hapa tulipo, haogopi, ni mkweli, ni mwaminifu kwa Taifa lake. Ana ndoto nyingi ambazo
anahitaji kuzitimiza kwa Taifa lake. Tumpe ushirikiano, tuache maneno maneno, tusonge mbele. Kama mlikuwa mna uchungu, mngemsikiliza Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja mia kwa mia. Nawatakia kila la heri Watanzania wote. Ahsante sana. (Makofi)