Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kuipongeza hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na niseme tu Serikali makini ni ile inayokusanya kodi. Kwa hiyo, nampongeza sana Waziri, hakuna nchi yoyote iliyoendelea bila kukusanya kodi. Serikali ya Awamu ya Tano imekwenda mbali zaidi, imepanua wigo wa kukusanya kodi ili iweze kuhudumia wananchi wake, tunaipongeza sana Serikali kwa kupanua wigo na kupeleka huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi, Serikali imepeleka asilimia 40 ya mapato yake kwenye miradi ya maendeleo, imepeleka pesa za walipa kodi kwa wananchi moja kwa moja. Pesa hizi zitajenga zahanati, barabara, madaraja, shule na kadhalika. Naipongeza sana Serikali na imeonesha dhamira ya Mheshimiwa Rais Magufuli ambapo katika kila hotuba yake amekuwa akiongelea masuala ya wanyonge, leo kwenye bajeti yake ametuonesha dhamira yake kwamba amedhamiria kusaidia wanyonge kwa pesa za walipa kodi, tunamtia moyo kwamba aendelee kukusanya kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu CAG kama walivyoongelea wenzangu. Naomba pesa za CAG ziongezwe kwa sababu yeye ndiye Mkaguzi Mkuu wa vitabu vya Serikali, CAG ndiye anakagua kitaalamu. Tusidanganyane anaweza kuja mtu mwingine kukagua, akakagua juu juu tu asiingie in deep. Mhasibu anakaguliwa na Mhasibu? Mhasibu anakaguliwa na External Auditor ambaye ana uelewa wa kumkagua, ukimkagua juu juu akifika Mahakamani, wewe ni Mwanasheria, huwezi kumthibitisha kwa asilimia 100 atakukimbia tu na atashinda kesi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali impe hela CAG akatimize dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kutumbua majipu na kuhakikisha fedha za Serikali haziliwi hovyo. Kwa mfano, kwenye Halmashauri au system nzima ya Serikali sasa hivi wanatumia EPICAR System, walianza kutumia Platinum System wakatumia EPICAR 7, sasa hivi wanatumia EPICAR 9.5 ambayo External Auditor wamesomea. Huwezi kumpeleka PCCB akafungue EPICAR 9.5, hawezi kufungua na kuingia ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii External Auditor akienda kumkagua Mhasibu anapewa cash book nzima akiona kuna longo longo anamwambia Chief Accountant nipe password yako anaingia moja kwa moja kwenye system ya EPICAR 9.5 kwa sababu wamefundishwa. Hivi ni nani mwingine anaweza akaingia kwenye system ya EPICAR? Ni nani mwingine anayeweza kumkagua Mhasibu mtaalam anayeiba kwa kalamu, anayeiba kisomi zaidi ya External Auditor? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mnawapa pesa za mishahara na pesa za matumizi ya ofisi, watu hawa wanafanya kazi mpaka saa nane ya usiku kwa macho yangu nimeona. Unakuta kuna risiti feki, anaenda kuchukua vitabu vya revenue anahakikisha kitabu kwa kitabu kuona kwamba ni sawa, anachukua password ya Revenue Accountant anaingia kwenye system anakagua mpaka saa saba ya usiku, mnawavunja moyo watu hawa, hamuwatendei haki. Niiombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, mpeni CAG pesa afanye kazi ya kubana pesa za Watanzania zinazoliwa na watu wachache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ni vitu vya kitaalam jamani, vinakwenda kwa utaalamu. Haiwezekani mtu tu akaja akakagua mkasema eti huyu mtu Mahakamani mtamtia hatiani asilimia 100, siyo rahisi, ndiyo maana wanashinda kesi kila siku, niombe kabisa CAG akague. Leo ameokoa shilingi bilioni 20 kwa mwezi pesa za mishahara hewa angekuwa siyo CAG tungeokoa hizi shilingi bilioni 20 ambazo zimeenda kulipa watumishi hewa? Siyo CAG ndiye ametuletea shilingi bilioni 20 ambazo tumeziokoa? Naomba sana Serikali iangalie hili kwa makini, mpeni pesa aendelee kuwabana watumishi wasio waaminifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningeweza kuliongelea kwa upana ila muda wangu ni mchache niende moja kwa moja katika Mkoa wangu wa Tabora. Kitu kinachoumiza zaidi RC wa Mkoa wa Tabora hana gari, leo utamkuta kwenye Pick up, kesho utamkuta kwenye gari ya mradi, ukimkuta kwenye gari ya RC yupo njiani nimemuona kwa macho yangu anasukumwa gari imekufa. Naiomba Serikali, Mkoa wa Tabora ni mkubwa, jinsi ya kuutembelea kwa gari bovu hauwezi, anahangaika kuomba magari mpaka kwa Wakurugenzi, ni jambo la aibu sana. Naiomba Serikali impe Mkuu wa Mkoa gari. Mkuu wetu wa Mkoa mnamjua siyo jembe ni katapila, nani ambaye hamjui Mheshimiwa Mwanry hapa? Anafanya kazi sana mpeni gari afanye kazi aliyopewa na Rais. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije sasa kwenye suala zima la kodi, mimi sipingani na Serikali kulipa kodi, hakuna Serikali ambayo inaweza kuendelea bila kulipa kodi lakini boda boda wa Tabora wanalipaje sawa na boda boda wa Mwanza wakati population ya Mwanza ni kubwa, mzunguko wa pesa wa Mwanza ni mkubwa, unamwambia boda boda wa Tabora alipe kodi sawa na boda boda wa Mwanza! Jamani acheni watoto walipe kodi kwa haki zao na ili waweze kujikomboa na waendelee, msiwape kodi kubwa tofauti na uwezo wao wa kulipa. Naiomba sana Serikali iliangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliongea na kaka yangu Mheshimiwa Mavunde, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, nikamuambia aje Tabora tukae na boda boda wa Tabora tuone jinsi ya kuwasaidia kuwapa mikopo ili waweze kujikomboa kiuchumi. Mikoa yetu bado maskini sana, nimuombe kaka yangu Mheshimiwa Mavunde alitafutie siku maalumu aje Tabora nimuitie vijana wa boda boda akae nao ili tuweze kuona ni jinsi gani tutainua mikoa ile ya pembezoni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kuhusu suala la mkopo. Naibu Spika wewe ni mwanamke, wanawake wengi wanashindwa kwenda kukopa benki kwenye riba ndogo kwa sababu hawana hati za nyumba, hawana hati za magari, wanaenda Pride, Finca ambapo riba ni asilimia 30 kuendelea. Mikopo hii wanashindwa kulipa wananyang‟anywa makochi yao, mafriji, waume zao wanawageuka wanawafukuza hatimaye tunazalisha watoto wa mitaani kila siku, Serikali ipo tu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku hizi habari ya mjini imekuwa ni microfinance, kila mtu akipata pesa anafungua microfinance, ndiyo unatajirika kwa haraka kwa sababu wanatoza riba kubwa, Serikali imekaa kimya tu! Nani anatoa leseni za hizi riba, wanamkopesa mtu kwa riba mpaka ya thelathini na huyu mtu atatajirika saa ngapi, atatoaje huo umaskini? Niiombe sana Serikali, nimuombe Waziri anayeshughulika na wanawake, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, nilimsikia siku ya Sikukuu ya Wanawake akimwambia Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake kwamba anakopeshaje kwa riba ya asilimia 18 wakati anapewa ruzuku ya Serikali lakini benki hizi mikoani kwetu hazipo. Mimi sijui maana ya Benki ya Wanawake kwa sababu mkoani kwangu haipo! Wanawake wa Mkoa wa Tabora hawapati hiyo huduma ya Benki ya Wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sasa Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye tuna imani naye, ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi, aniambie lini atakuja Tabora kuongea na akina mama na awape ahadi lini atafungua deski la Benki ya Wanawake kwenye Mkoa wa Tabora. Wanawake hawa wamekuwa waaminifu kwa Serikali hii, lazima muwatendee haki na hii benki ni ya wanawake wote siyo benki ya wanawake wa Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya hata sisi kwetu kuna wanawake na wanahitaji huduma hii na ni haki yao wanastahili kwa sababu ni haki ya Serikali kuwapelekea huduma hii. Naomba sana Mheshimiwa Ummy aniambie atakuwa tayari lini kuja Tabora kuongea na wanawake wa Tabora awaahidi suala la hata deski tu kama siyo benki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la chuo cha manesi. Tabora tumejengewa chuo cha manesi na Serikali wakisaidiana na ADB. Chuo kile ujenzi umefikia asilimia 90 bado asilimia 10 tu kumalizia lakini miaka miwili hatujapata fedha ya kumalizia. Majengo yale yameanza kupasuka, majengo yale yameanza kushuka kwa maana value ya majengo yale imeanza kupotea. Kwa kuweka maji na umeme asilimia 10 tu tutakuwa tumekamilisha. Mradi huu pia ulikuwa unajumuisha jengo la operesheni ambalo na lenyewe limesimama, pesa ni ndogo sana. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie jinsi ya kutupa hii pesa ndogo iliyobakia kwa sababu ya jengo la manesi ambalo litazalisha manesi wengi, wataweza kusaidia wananchi wa Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.