Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Allan Joseph Kiula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia japo kidogo katika hotuba ya Waziri. Nianze kwa kupongeza bajeti imetengenezwa vizuri, mahesabu tumeyaona lakini tunayo kazi ya kujaribu kutoa michango yetu panapotakiwa kurekebishwa parekebishwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema wenzangu jambo la faraja ni kwamba pesa hizi zote tunazokusanya asilimia 40 zinaenda kwenye miradi ya maendeleo, hilo ni jambo la faraja. Kingine cha msingi zaidi, niliwahi kufanya kazi TRA, jambo kubwa ambalo sisi tunapungukiwa ni utayari au utamaduni wa kulipa kodi, lakini ukitaka kitu chochote kizuri lazima ukigharamie. Kwa hiyo, inatakiwa tufikie mahali Watanzania tuone umuhimu wa kulipa kodi ili tuweze kupata maji, barabara na huduma nyingine ambazo tunahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo ambalo napenda Wabunge pia walielewe na Waziri natumaini analifahamu, katika mwelekeo wa sasa hivi kodi za ndani zinatakiwa zichukue nafasi kubwa. Tumezoea hizi international taxes contribution yake percentage inakuwa kubwa, lakini ili tuweze kuendelea lazima kodi za ndani zikusanywe kikamilifu, tuone maeneo ambayo kodi zinaweza kupatikana kwa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni watu walikuwa wanasema meli hazionekani bandarini, kodi imeshuka, maana yake nini? Ingekuwa kodi za ndani zimeimarika jambo hilo tusingekuwa tunalizungumza. Kwa hiyo, ni jambo muhimu ambalo inabidi tulione na tuisaidie Wizara na tuisaidie Serikali kuweza kubaini maeneo ya kupanua wigo wa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuachane na mambo ya TRA na kadhalika nizungumzie kodi za majengo. Nimeshuhudia kulikuwa na mvutano wa jambo hili lakini nasema kama sisi ni Watanzania kabisa tusirudi nyuma, kodi za majengo zikusanywe na TRA. TRA wanazo resources za kutosha kwa maana wanao wafanyakazi wa kutosha, wanazo database, wanayo mifumo ambayo inaweza ika-support ukusanyaji wa kodi lakini pia itakusanywa kodi stahiki kwa maana kwamba kile ambacho kinatakiwa kukusanywa kitakusanywa. Wakati mwingine sisi huwa hatuambiani ukweli kwa sababu Halmashauri zetu zilishindwa hata kufanya valuation ya majengo ili kupanua wigo wa kodi. Sasa lazima tukitaka kodi ya majengo ipatikane tukubaliane valuation ifanyike, identification ya property ifanyike properly na tutapata pesa nyingi sana mpaka wenyewe mtashangaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukija kwenye vyanzo vingine vya mapato wamezungumza wenzangu suala la utalii. Nafikiri Mheshimiwa Waziri amelisikia, VAT kwenye utalii hiki kitakuwa ni kizungumkuti kwa sababu tunataka watalii waje, tunataka tuweke incentives mbalimbali na tunataka tuchukue opportunity ya usalama wa nchi yetu hii ili watalii waongezeke. Kwa hiyo, jambo hili inabidi liangaliwe kwa ukaribu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Tanzania ina wakulima wengi wanalima alizeti na pamba, suala la kutoza ushuru wa forodha wa asilimia kumi badala ya zero kwenye mafuta ghafi ya kula na lenyewe tuliunge mkono, libakie kama lilivyo ili tuweze kuwasaidia wakulima wetu waweze kupata masoko, viwanda vyetu vya ndani viweze na vyenyewe kusonga mbele. Kwa sababu ukiangalia sasa hivi mafuta ya alizeti hayana cholesterol, lakini hayauziki kwa sababu bei yake ni kubwa. Kwa kufanya hivyo, nafikiri tutapiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo naomba tutafakari pamoja hapa na Mheshimiwa Waziri. Jambo lenyewe la kutafakari ni kwamba karibu kila Mtanzania ana simu, ukichukua population ya Watanzania, Mheshimiwa Zungu amezungumza hapa, lakini kodi za kwenye simu hazionekani. Ukienda hapa jirani Kenya (Safari Com) kila siku ya mlipa kodi Safari Com wapo, mchango wao ni mkubwa, kiwango kinachotolewa kinaonekana, Tanzania kuna tatizo gani? Hizi kampuni za simu zinakwepa vipi kulipa au zinaficha vipi mahesabu yao? Mimi naamini TRA wako wataalam lakini naamini utaalam huo unatolewa sisi hatuuchukui, ingekuwa tunachukua utaalamu huo tungekuwa tumeshapiga hatua kubwa mpaka ikiwepo kuishauri TCRA ku-track zile simu na kujua gharama iliyotumia, hilo ni jambo muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata humu Tanzania tunaambiwa kwamba kuna watu wana pesa za kutosha (mabilionea) lakini mbona mchango wao hauonekani, mahesabu yao wanatengenezaje? Jambo hilo na lenyewe linatakiwa liangaliwe kwa karibu ili kuwe na equal share katika ulipaji wa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa 84 na 85 nimpongeze Waziri kwa kufuta baadhi ya kodi kwenye bodi, ni jambo muhimu, tulilitegemea na tunategemea twende zaidi. Suala la industrial sugar (asilimia 10), maana yake sukari hiyo ikiingia inaingia kwenye soko la walaji. Suala hilo pamoja na kwamba sasa tunabadilisha mwelekeo tuangalie usimamizi wake. Iagizwe sukari ambayo itaweza kwenda huko kwenye viwanda lakini huku kwingine tulinde viwanda vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la misamaha ya kodi. Nashauri lisimamiwe kwa ukaribu kwa sababu tunaaamini kabisa iko misamaha yenye tija ambayo inabidi iendelee kutolewa. Hata hivyo, sheria zetu na TIC ziwe aligned, nafikiri mgogoro unakuja hapa kwenye TIC, utafika pale unaambiwa kuna strategic investor sijui kuna nani, maelezo chungu mzima, hayo maelezo yanakinzana na sheria nzima ya ukusanyaji wa kodi. Jambo hili liangaliwe na liwekwe wazi ili isionekane kwamba kuna mtu anaweka sheria zake anazofikiria yeye mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 99 kuna suala limezungumziwa kuhusu kudhibiti misamaha ya kodi, kwamba watu walipe baadaye wadai refund lakini tumeshuhudia watu wanakaa kwenye queue kusubiri hiyo refund, pesa haziendi kwa lugha rahisi. Hiyo na yenyewe ina create image mbaya, lakini pia inafunga mitaji ya watu. Kwa sababu mtu anapolipa kodi anategemea refund ili aendelee kufanya biashara yake na mtaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lipo jambo lingine ambalo pia inabidi tuliangalie kwa pamoja nalo ni usajili wa bodaboda kuongezewa muda. Ni sawa umeongezewa muda lakini zamani kulikuwa na biashara ya taxi na ilikuwa ni formal business. Biashara ya taxi imekufa, waliochukua nafasi hiyo ni bodaboda, lazima sasa tujue contribution ya bodaboda katika kufidia pengo ambalo taxi imeliacha maana tulikuwa tunakusanya pesa kule. Kwa hiyo, ni jambo ambalo na lenyewe inabidi tutafakari kwa pamoja. Tunatambua kwamba bodaboda tume-create ajira ya kutosha, ni kitu kizuri lakini tuangalie basi mchango wake ukoje. Maana haya mambo tunayozungumza ya maji, umeme wote tutakuja kufaidi kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema tutakopa mikopo ya nje, kuna mikopo ya kibiashara na yenyewe tuiangalie. Kwenye michango Wabunge walisema kwamba tuangalie hii Private Partnership, wawekezaji wanaweza kuja kugharamia baadhi ya miradi ili tuondokane na suala la kukopa kwa wingi mikopo kutoka nje kwa sababu madhara ya mikopo tumeyaona na deni la Taifa linazidi kuwa kubwa. Kwa hiyo, tukisimamia vizuri suala hili tutapiga hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mapendekezo yalitolewa na ni rahisi tu ambayo yangeweza kutusaidia. Tuna wafugaji wetu wa kuku waliomba VAT iondolewe kwenye mashudu ya kutengenezea chakula, lakini naona suala hilo haliangaliwi kabisa lakini nyumbani tumeacha kuku kule wanafugwa. Tulisema suala la kuleta mapinduzi ya uvuvi, tukasema baadhi ya vifaa viondolewe kodi, mfano mafuta yanayotumika kuendeshea boti za uvuvi. Kwenye migodi wanasamehewa kodi kwa nini kwenye uvuvi wasiweze kusamehewa kodi kwenye vifaa vya kuvua samaki kielektroniki? Hayo ni baadhi ya maeneo kama tukiyaangalia kwa uzuri tunaweza tukapiga hatua kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa naamini kabisa kwamba sheria za kodi ni nzuri tu, lakini hazijasimamiwa vya kutosha. Ninaposema hazijasimamiwa vya kutosha nadiriki kusema kwamba mambo ya kisiasa ndiyo yanafanya zisisimamiwe kwa sababu TRA uwezo wa kukusanya kodi na kusimamia wanao, tatizo tukishaanza kuingiza mambo ya siasa wanashindwa kukusanya na kufikia malengo. Ndiyo maana ukifanya trend analysis miaka mitatu, minne iliyopita kuna miaka tumeshindwa kufikia malengo. Kwa nini tumeshindwa kufikia hayo malengo? Ukiwauliza watu wa TRA watakupa sababu na Waziri mhusika akienda kuongea nao watampa sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusisitiza ni nini hapa? Najua TRA wamejipanga vizuri lakini sasa nao wasaidiwe na kusaidiwa kwao ni rahisi zaidi kama sisi tutasimamia sheria. Kama sisi tunavunja sheria nao watashindwa kufikia malengo na baadaye tutawalaumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, nafikiri mchango huo utamsaidia Waziri, naunga mkono hoja.