Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru pia na mimi kwa kupata nafasi hii ya kuchangia. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa maandalizi ya bajeti waliyotuletea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kupongeza, nimeona katika bajeti kuna suala la kuanzisha industrial clusters, nashauri hapa Halmashauri zipewe kama agizo kutenga maeneo hayo, lakini pia katika hotuba nimeona kuna suala la kufanya tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa. Hii ni muhimu kwa sababu itatusaidia kuonyesha jinsi gani ya kwenda mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati tunafanya tathmini hii nimuombe Mheshimiwa Waziri pia afanye tathmini ya mashirika ambayo tunaambiwa kwamba yalikuwa ni ya Serikali lakini kwa namna za ajabu ajabu yameangukia mikononi mwa watu binafsi. Mfano wa shirika hili ni kama PRIDE. (Makofi)
Katika pongezi zangu pia nipongeze kwa kuwepo ushuru kwenye bidhaa za samani kwa maana ya furniture. Nasema hivi kwa sababu mimi natoka Mufindi (Mafinga) tuna viwanda kule vya mazao ya misitu naona itakuwa ni chachu ya kuvisaidia kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia mimi binafsi nipongeze kwa kuongeza ushuru kwenye industrial sugar. Suala hili litasaidia wawekezaji wa ndani kupanua viwanda vyao na hivyo wakulima wetu wa miwa hasa wale wakulima wa nje (out growers) watahamasika kuendelea kulima, wao watapata mapato, lakini pia na Serikali itaendelea kupata mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi sasa nije kwenye maoni. Nimehangaika sana na nimebahatisha nimepata ile ripoti ya timu ya Mheshimiwa Chenge (Chenge One) ambayo ilikuwa inaainisha maeneo mbalimbali ya kuboresha mapato. Nashangaa sana labda ni kukosa ufahamu au uzoefu. Hao wenzetu wa TCRA kuanzia tarehe 16 watazima simu fake maana yake ni kwamba wana mitambo ya kuweza kung’amua simu fake. Mimi najiuliza, wanawezaje kukosa kuwa na mitambo ya ku-track mapato na makusanyo yatokanayo na makampuni ya simu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuwe wa kweli, makampuni ya simu sisi hatuja-exhaust ipasavyo mapato kutoka kwenye hayo makampuni na ndiyo maana hata Waheshimiwa Wabunge wanapolia kwenye gratuity na kuelekeza vyanzo vitizamwe maeneo mengine mojawapo ni kwenye makampuni ya simu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata competition iliyopo na mwenendo mzima wa haya makampuni ya simu yaani kuna unfairness kubwa sana. Ukiweka vocha ukilala ukiamka balance imeliwa. Ukinunua bando kwa mfano ni mkataba kwamba unanua bando mpaka itakapoisha ununue nyingine, lakini ikiisha unachajiwa direct kwenye ile pesa yako ya kuzungumza, yaani ni madude mengi sana yanafanyika kwenye makampuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mapato yatokanayo na makampuni ya simu Mheshimiwa Waziri anapowasilisha hotuba yake ya watu wa mawasiliano alisema tuna around simcard milioni 40; je, kweli sisi Serikali kupitia TCRA wakishirikiana na TRA tumepata makusanyo ya kutosha kutoka kwenye makampuni ya simu?
Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho, hebu jaribu kutueleza Serikali ina mikakati gani katika kuhakikisha kwamba tunapata mapato ipasavyo kutoka kwenye makampuni ya simu kama ambavyo mnakusudia kupata mapato kutoka kwenye maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu misamaha ya kodi kwa taasisi za dini na watumishi wa umma. Mheshimiwa Dkt. Kafumu ameeleza pale kuhusu haja ya kuwapa watumishi wa umma morali.
Mheshimiwa Waziri hata hawa watumishi tunasema kwamba ikiwa mtumishi anataka kununua gari itabidi ule msamaha wake wa kodi aliokuwa anapewa kwanza alipie halafu baadaye aje a-claim. Mheshimiwa Waziri watumishi wa nchi hii hali zao ni duni sana, haka ni ka-privilege kadogo walikonako. Hebu mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri kwenye hili tuwaache. Kama mtu anadunduliza anataka apate kausafiri tafadhali tumtie moyo kwenye suala hili la msamaha wa vyombo vya usafiri kwa watumishi. Namuomba Mheshimiwa Waziri kwa kweli tusiwawaguse, haka ni ka-privilege, ni sehemu ya kupandisha morali yao. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri amesema jambo hili pia litagusa hata mashirika ya dini, mashirika ya dini katika nchi hii yana-supplement sehemu kubwa sana huduma mbalimbali za elimu na afya. Sasa tunasema kwamba kama watakuwa wananunua bidhaa au masuala yoyote itabidi kwanza walipe kodi halafu baadaye waje wa-claim, vitu vingine Mheshimiwa Waziri ni misaada.
Mimi kwa mfano juzi nimepata msaada wa ambulance sikuwa na bajeti hiyo ya kulipia. Sasa hawa watu vitu vingine wanaletewa kama misaada tukisema kwamba walipie halafu ndipo warejeshewe naona tutakuwa tunawavunja nguvu, ni jambo tunalopaswa tuliangalie mara mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuzungumzia suala la bodaboda, tumesema usajili utoke shilingi 45,000 mpaka shilingi 95,000, hii ni sehemu mojawapo ambayo watu na vijana wamejiajiri. Kama vijana wa bodaboda wamejiajiri na wanatusaidia sisi usafiri katika maeneo mengi maana yake ni kwamba kuwaongezea gharama ni kuongeza gharama kwa mtumiaji wa ule usafiri, napenda tuwatizame watu hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo napenda kuongelea suala la mitumba, mitumba mbali ya kuwa ni biashara kubwa hata mimi hapa nimevaa hii suti yangu hapa ni ahsante JK wakati ule nasafiri ndiyo nilinunua hii suti, lakini nina hakika nusu ya watu humu ndani tunavaa mitumba. Sasa tunapoongeza hiyo kodi kutoka 0.2 cent mpaka 0.4 cent ndugu zangu, tunawateketeza vijana waliojiajiri katika biashara hiyo. Kweli leo hii tunafuta mitumba baada ya miaka mitatu kulingana na makubaliano katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, je, viwanda vyetu viko tayari kweli kutuzalishia sisi nguo za kututosheleza humu au baadaye tunageuka kuwa soko la Wachina katika bidhaa zao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja na haraka haraka kwenye suala la VAT kwenye sekta ya utalii. Sisi wenyewe tunakiri kwamba sekta hii imechangia mapato ya fedha za kigeni kwa asilimia 25. Nilisema wakati nachangia Wizara ya Maliasili na Utalii hata fedha tunayoweka kwa ajili ya ku-promote utalii wetu bado ni ndogo. Sasa kama tunakusudia sekta itupe mapato ya kutosha kama ambavyo imekuwa inatupa hayo mapato kwa asilimia 25, tuna kila sababu ya kuendelea kuilea.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi leo promotion tu tunawekeza chini ya dola milioni mbili, wenzetu wa Kenya kwa mujibu wa takwimu nilizonazo karibu milioni 80 USD, Rwanda milioni 11 USD na Uganda milioni 8 ambayo tunadhani siyo washindani wetu. Badala ya kuielea hii sekta bado tunaiongezea mzigo wa VAT, wenzetu wamefuta VAT na ndiyo maana mimi nasema pamoja na hizi integration blocks katika uchumi wa dunia ya leo tuwe wanjanja. Maana Mheshimiwa Waziri ametuambia kwamba hilo wamekubaliana katika Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini wenzetu katika bajeti yao wameliondoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana kila siku nasema tuwe tunajiongeza na sisi tusikubaliane kila kitu kwa tu spirit ya East Africa, tukubaliane lakini na sisi turudi je, kwetu tumejipanga vipi kutumia hiyo fursa ipasavyo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba naomba misamaha ya kodi kwa mashirika ya dini na watumishi wa umma tafadhali Waziri atakapokuja kuhitimisha azungumzie hili, haka ndiko kadude pekee watumishi walikobaki nako kakurejesha morali yao, tuwatizame tuwaache kwa sababu mtu anaweza akalipa lakini marejesho kuyapata kwa kweli ikawa ni kazi sana.
Kwa hiyo, niombe kabisa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hayo ni baadhi ya mambo napenda ayasisitize namna gani tutahakikisha tunapata mapato kutoka kwenye makampuni ya simu, namna gani tutaweza kuona kwamba hii VAT tunaiondoa kuvutia utalii na kuunyanyua lakini pia kwa ujumla namna gani suala la mitumba tuliache kama lilivyokuwa tusubiri kwanza tujipange hapa ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nashukuru sana kwa nafasi pia.