Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ahmed Ally Salum

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Solwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Kwanza kabisa, naunga hoja mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza kuongea kuhusu suala zima la bajeti hii na hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nilikuwa nataka kusema kwamba katika Kata yangu ya Makitorio, kuna tatizo kubwa sana la wachimbaji wadogo wadogo ambao sasa imefikia wakati vurugu inataka kutokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mwekezaji anaitwa Barricks ambaye naye katika utafiti wake kafika mahala naye akaliuza, yaani kapewa eneo akaona halifai naye akaenda akaliuza. Sasa katika kuliuza kuna mwekezaji mmoja amenunua, imeleta mkanganyiko mkubwa sana kwenye kata ile, tunashindwa kuendeleza, tunashindwa kufanya kazi. Kwa hiyo, naomba Serikali isimamie na hasa Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Muhongo, nafikiri nitakuja ofisini kwako ili tuone namna ya kutatua tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Hospitali ya Wilaya, Rais aliyemaliza muda wake aliahidi mara mbili; kaja Waziri Mkuu, Mheshimiwa Pinda aliyemaliza muda wake, akaahidi; akaja Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ameahidi. Sasa mimi sina majibu katika suala hili na katika bajeti hii sikupangiwa fedha.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri hili ulichukue, sisi tuliomba shilingi bilioni tatu, angalau tupate shilingi bilioni moja na nusu, twende, kwa sababu ina miaka sita. Sisi kama Halmashauri kwa miaka sita tumejenga Hospitali ya Wilaya tumeshindwa kumaliza na sina namna nyingine yoyote. Naomba Mheshimiwa Waziri alisimamie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna maji ya World Bank; nimeuliza swali langu hapa asubuhi. Huu ni mwaka wa pili, mradi umefikia nusu. Mwaka wa pili hatujapata fedha za kuwalipa wakandarasi kumaliza kazi zao na hakuna maji; miradi kumi, tunasubiri zaidi ya two billion na mpaka leo mkienda kule maswali ni mengi; ufinyu wa bajeti. Majibu hayo ya ufinyu wa bajeti kwa kweli inafika mahali yanakuwa hayaridhishi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina fedha nyingi. Katika mambo ambayo kama kweli tunataka tujikite vizuri kwenye suala zima la viwanda, sijaona bajeti ya research and development. Hakuna nchi duniani inaweza ikaendelea bila kuwa na bajeti ya research and development. Hapa tunafanya kazi kwa matukio tu, kikitokea kitu hivi, basi au itokee makampuni fulani yameweza kuomba halafu Wizara ya Viwanda na Biashara ithibitishe iite vikao, task force mpaka ije Wizara ya Fedha, ndiyo mwone. Hayo ni mambo tu ya matukio.
Mheshimiwa naibu Spika, sasa mkiweka bajeti ya research and development ikafanya kazi kwa maana ya kwamba tukatambua mfano, eneo lote hili la viwanda, ni vitu gani ambavyo vinatufanya Watanzania tuweze kuendelea haraka? Ukishayatambua yale yakakaa juu ya meza, ni mara moja mno kutatua, kama kubadilisha sheria, sera na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vikwazo ni vingi katika uwekezaji ndani ya Tanzania hii. Nchi yetu ina amani, hakuna kitu kikubwa duniani kama amani, ndiyo advantage kubwa; na wawekezaji wa nje hawa wanaokuja hapa, kitu kikubwa kabisa wanachokifuata hapa ni amani na masoko, lakini ukiingia ndani ya uwekezaji, vikwazo ni vingi sana. Ukitaka raha ya ngoma ingia ucheze tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vikwazo ni vingi sana. Nilichangia wakati ule katika Wizara ya Viwanda na Biashara, nikatoa mifano miwili, mitatu, midogo sana. Ukitaka kuuza cement kupeleka Uganda ili upate kibali unalipia 2% ya thamani ya mzigo ule. Wakati Uganda na Kenya hulipii, wao wanaleta tu kama wanataka kuleta. Sasa utaona kwamba vikwazo ni vingi katika kupata leseni, ardhi maeneo na maeneo. TIC pale, EPZ, NEMC, TBS kila mmoja ana mawazo yake na kila mmoja na maamuzi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru tu Mheshimiwa Mpango sasa hivi umekuja kidogo na suala zima la material, umeongea vizuri kuna maeneo pale umeweka mambo yamekaa vizuri. Ila naomba tu na Waheshimiwa Wabunge wote tukubaliane, angalau 1% ya bajeti hii itoke iende kwenye research and development ili sasa Serikali iweze kuona kabisa maeneo gani wayafanyie kazi. Nakuhakikishia ukishayagundua matatizo, mwaka 2017/2018, 2018/2019 nchi ita-take off vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nisemee bandari yetu ya Tanzania. Bandari ya Tanzania inapigwa vita bila sisi kujua kama inapigwa vita.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya tulikubaliana kwamba waweke Ofisi ya Umoja wa Forodha kwamba mizigo yote ya kutoka Zaire; kontena zote zinazotoka Zaire walipie Kenya na Tanzania tukakubaliana hivyo. Tanzania tukawahi kufanya ofisi hiyo, tukaweka hapa, Wazaire sasa, badala ya kuja kutoa mizigo yao hapa, wameondoka wamekwenda Kenya, wamekwenda na Beira. Wakenya wamefanya utafiti wakaona kwamba tukiweka ofisi hapa ili Wazaire walipie ushuru ndani ya Mombasa hawatopata mzigo hata mmoja. Ndiyo sababu kubwa ya bandari yetu kupungukiwa na mizigo ya transit.
Mheshimiwa Naibu Spika, Umoja wa Forodha Wazaire wamekimbia, sababu nyingine ilikuwa ni suala zima la VAT; mmeweka VAT katika transit goods. Kuna kampuni kubwa sana kama hii Impala, wakileta mzigo, meli zake moja mwezi mzima ma-transporter wanabeba mizigo hiyo ya mbolea kwenda nchi jirani, wameondoka, wanashusha Beira, wanashusha Mombasa. Tume-lose a lot of money. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine ni restriction. Namshukuru Mheshimiwa Dkt. Pombe Magufuli, kulikuwa kuna Beira, kulikuwa na hizi za check points; ukitoka bandarini mpaka border ni check points sita; ameondoa zimebaki tatu, mimi namshauri aweke hata mbili tu. Wakenya wameweka mbili, sasa wenzetu Wakenya wanatufuatilia sisi kuona namna gani tumeweka sheria ili wao waondoe zile sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe mfano mdogo, mmekuja hapa na sheria ya kuweka VAT katika masuala ya tourism, mmekubaliana. Wao wameondoa, hili suala la kuweka ofisi kwa ajili ya kulipia ushuru wa Wanazaire, tulikubaliana, wao hawakufanya! Ukitazama Malawi wanatupiga vita; wameenda kuongea na Mozambique, wameweka reli pale, kuna mizigo inayotoka Beira kuja Malawi. Kwa hiyo, tunapigwa vita bila sisi kujua tunapigwa vita kiasi gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii research and development ikiweza kufanya kazi yote, itatambua, itajua matatizo yako wapi na tutafanya kazi vizuri; nchi itatoka. Tuna billions of money! Kenya wana kontena milioni sita kwa mwaka, Singapore milioni 30 kwa mwaka, Dubai milioni 24.5 kwa mwaka, sisi tunaongelea kontena milioni moja kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tukiweza kuwa na kontena milioni mbili tu za transit mara dola 1,000 tuangalie ni fedha kiasi gani tunazozipoteza, simply kwa sababu ya kuchukua maamuzi madogo tu ambayo hayahitaji fedha. Ni kuyatambua matatizo yako wapi, kukaa mezani, kuyaleta pale kwenye Baraza la Waziri, leta hapa tubdilishe sheria ndogo hizi ili hawa wafanyabiashara wa nchi jirani warudi na kujenga imani kutumia bandari yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha unakosa fedha nyingi mno kwenye transit goods, mimi siongelei mizigo ya ndani. Mizigo ya ndani wala sina tatizo nalo, wafanyabiashara hawana tatizo na kulipia ushuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la viwanda, hakuna maendeleo katika suala zima la viwanda kama vikwazo (restrictions) ambayo yako ndani ya viwanda hayatatoka. Ni mengi mno, nikiyataja hapa ni mpaka kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Waheshimiwa waliochangia asubuhi, tumewekewa kodi kwenye mafao haya ya Wabunge. Sasa hilo suala zima naomba lishughulikiwe, lifanyiwe kazi. Kama alivyosema Mheshimiwa Bashe, ma-DC na wengine hawakuwekewa. Sasa huko nje mitaani ni kweli kabisa Waheshimiwa Wabunge tumechongonishwa vibaya sana. Ama itolewe kwa wote ama iwekwe kwa wote kabisa kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana, ahsante sana.