Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii. Katika nchi yetu kuna miradi mingi ambayo tuliiandaa na sera yetu inasema kuhusu Zahanati na Vituo vya Afya, lakini tukiangalia sehemu nyingi Vituo vya Afya, havijakamilika, unakuta sehemu nyingine kuna jengo zuri sana Serikali imejenga, lakini vifaa vya mle ndani havijakamilika. Naomba kupitia bajeti hii Serikali ijitahidi sana, miradi yote ya vituo vya afya pamoja na zahanati walizojenga wananchi ziweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna vifaa kama dawa, vifaa tiba; katika sehemu nyingi, zahanati nyingi hazina vifaa tiba, wananchi wanapata taabu. Kwa mfano, sisi pale Mkoa wetu wa Katavi, Wilaya ya Mpanda, ile hospitali ni ya Wilaya lakini tunasema ni kama Hospitali ya Mkoa. Hakuna kabisa vifaa, wananchi wa Wilaya ya Mpanda wanapata shida, ina maana kama ni ya Mkoa, maana yake ndiyo Makao Makuu ya Mkoa, lakini hawana vifaa kabisa. Naomba kupitia bajeti hii, Serikali ijitahidi kufikisha vifaa ili wananchi wetu waweze kupata matibabu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa akina mama, kuna tatizo la maji vijijini. Tunasema maji vijijini kwa sababu sisi akina mama tunahitaji maji na utakuta maeneo mengi vijijini akina mama wanapata shida, wanaenda kutafuta maji sehemu za mbali, anaamka saa 8.00 za usiku, saa 9.00 za usiku anaacha familia yake. Naomba kupitia bajeti hii tunaomba sana Serikali itufikishie maji vijijini. Kwa sababu tutakuwa tumewakomboa sana wananchi kupitia maji hususan akina mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kupitia bajeti hii ambayo tumesema kuhusu shilingi milioni 50 za kila kijiji, napendekeza kupitia bajeti hii, fedha hizo ziende kila kijiji. Vile vijiji ndiyo vinawajua wananchi katika maeneo yao husika, maana kuna vijiji halafu kuna Mitaa. Mijini wanatumia mitaa; kwenye maeneo ya vijijini, kuna vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaomba zile fedha, kwa sababu kama mtaa ndiyo unawafahamu watu, Mwenyekiti wa Mtaa na ile Kamati yake ndio anawajua watu wa mtaani kwake. Sasa fedha zile shilingi milioni 50 zikifika pale wale watajuana ni jinsi gani watagawana zile fedha na kukopeshana ili waweze kupata faida ya Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi mazuri ambayo yanayofanywa Serikali, tunaomba Serikali kupitia vile vile michezo, mara nyingi bajeti hii imekumbuka michezo, sanaa lakini bado mfumo wetu wa michezo haujakaa vizuri, hususan vijana wetu wa vijijini wako vijana wachezaji mpira wazuri ambao wanaweza kulikomboa Taifa hili, lakini bado hatujawafikia na bajeti zetu haziwafikii kule wakatambulika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wako wasanii wazuri ambao wanajua mambo ya usanii huko vijijini, lakini kutokana na uwezo, hawawezi kufika mijini au hawawezi kufika sehemu ambayo anaweza akajulikana au akafahamika. Basi tunaomba kupitia bajeti hii sasa, Serikali ikatambue wale watoto walioko vijijini, ambao wanaweza kuja kulipatia faida Taifa hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi yanayotakiwa yafanyike ndani ya nchi yetu, kupitia bajeti hii. Pia kuna haya mashirika makubwa hususan bandari na viwanja vya ndege. Wao wanapata mapato ndani ya shirika kama vile bandari, lakini unakuta kuna mfuko wa Serikali na tumesema safari hii fedha yote iingie Serikalini, lakini vilevile kuna mambo wao kama shirika, wanatakiwa waboreshe ili waweze kupata faida zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunaomba kupitia bajeti hii, kama bandari kuna fedha ambazo wanaingiza katika Mfuko wa Hazina, tunaomba yale mahitaji wanayoyataka wenyewe kuboresha bandari ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi mzuri zaidi, wapewe zile fedha haraka ili waweze kuinua uchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile katika viwanja vya ndege, tunajua kuna miinuko ambayo inaruka ndege, kuna faida kubwa ndani ya viwanja vyetu, lakini wana mahitaji ambayo wanataka kuweka labda taa, na kadhalika, naomba basi Serikali iwape zile fedha haraka kwa ajili ya mahitaji yanayoweza kuleta faida katika viwanja vyetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo mengi yanayofanyika katika mashirika ambapo sasa hivi pesa nyingi zitakuja kwenye Mfuko wa Hazina. Maana yake sasa hivi fedha zinazotoka katika mashirika mengi tumesema kupitia bajeti hii zitaingia kwenye mfuko maalum. Naomba Serikali, pindi watakapohitaji fedha zile wafanye jambo fulani, naomba wapewe ili waweze kuongeza ufanisi ndani ya kazi zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali yetu kwa mpango mzuri kwamba kwa kupitia bajeti hii tumepanga kununua ndege tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba nchi yetu hapo katikati usafiri ulikuwa ni shida. Sisi tumefarijika sana kupitia bajeti hii kuona sasa Serikali yetu imekumbuka kununua ndege tatu, kusema kweli tumefarijika sana. Tunaomba sasa mikakati na utaratibu kuhusu Shirika la Ndege la ATCL, mikakati yake ipangwe vizuri tusije tukaharibu kama tulivyoharibu mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua shirika letu hili lina madeni mengi, lakini najua Serikali imeamua kufanya kitu ambacho safari hii hatuwezi kuharibika tena, kwa sababu madeni yale najua kuna bajeti ambayo mtaipanga, tulipe yale madeni, halafu shirika sasa lisimame kama shirika na sisi Tanzania sasa tuwe na Shirika la Ndege. Tutafurahi kwa sababu kama mimi Mkoa wangu wa Katavi, nashukuru Serikali naomba niipongeze, mlitujengea uwanja mzuri sana, lakini hakuna ndege hata moja inayotua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia hili sasa, hizi ndege tatu, nami najua sasa Mkoa wa Katavi, ndege itatua. Naomba niwapongeze kwa hilo, basi tununue hizo ndege ili sehemu nyingi ambazo ndege zilikuwa hazifiki, sasa ziweze kufika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukurru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuongea kengele ya pili isinigongee. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.