Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia bajeti hii. Sambamba na hilo naomba nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema, nimpongeze sana Waziri wa Fedha kwa hotuba yake yote aliyoitoa ya Hali ya Uchumi pamoja na hotuba ya Bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kwanza kwenye pato la ukuaji wa uchumi lakini nikirejea ukurasa wa 16 wa Taarifa ya Hali ya Uchumi. Naipongeza sana Serikali kwa kuifanya nchi yetu Pato la Taifa likakua kwa asilimia 7.0 kwa mwaka 2015. Nitoe masikitiko yangu kwamba kwenye eneo la kilimo ambapo asilimia 70 ya wananchi wetu ndiyo wanakitegemea imebainika kwamba uzalishaji wake umeshuka. Mwaka 2014 ilikuwa na asilimia 3.4 mwaka 2015 imeshuka kwa asilimia 2.1. Jambo hili hatutakiwi kulifumbia macho na halitakiwi tu kubakia katika vitabu. Tujiulize anguko hili limetokea kwa sababu ya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, inawezekana wakulima wetu wamekata tamaa ama kwa kucheleweshewa pembejeo, pembejeo hazifiki kwa wakati lakini sambamba na hilo ni kwamba Vyama vyetu vya Msingi na Vyama vya Ushirika, vimekuwa vikidhulumu sana wakulima wetu. Kwa hiyo inawezekana kabisa Wakulima hawa wamekata tamaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasababau ya makusudi sana kwamba nchi yetu tufikie kipato cha kati, lakini naomba niishauri Wizara, tukitegemea mvua za masika kwa kweli hatutafika. Ipo sababu ya msingi kabisa Serikali ikaona umuhimu wa kuweka kipaumbele katika kilimo cha umwagiliaji kwa sababu tukitegemea tu mvua za msimu mwisho wa siku tutakuja kukwama, kwa sababu tunaona kuna kipindi mvua za msimu zinakuwa ni nyingi sana, kuna kipindi zinakuwa ni chache. Ningeomba niishauri Serikali iweke mkakati wa muda mrefu wa kuhifadhi maji ya mvua ili mwisho wa siku tuweze kukajikite zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni budi sasa nchi yetu ikajitahidi kupata wataalamu wengi zaidi na kujifunza kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa wenzetu ambao wameweza kufanikiwa katika kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano; wenzetu wa Israel wamefikia hatua nzuri, wenzetu wa Indonesia, wenzetu wa China na maeneo mengine duniani ambayo sikuyabainisha. Hebu Serikali yetu ifanye dhamira ya dhati kwa kuwapeleka wataalam wengi zaidi ili kusudi na sisi tuweze kujikita katika hili suala la kilimo cha umwagiliaji. Mwaka huu katika kilimo kumekuwa kuna shida sana hasa kwenye maeneo yale ambayo yanayolima mtama, maeneo ambayo yana uhaba wa mvua. Ni kwamba kumekuwa na ndege wengi sana ambao wamekuwa wakiharibu mazao, lakini kwa masikitiko makubwa sana, nchi yetu haina ndege ya kuweza kunyunyiza dawa. Ninaunga mkono mpango wa Serikali wa kununua ndege kwa ajili ya abiria, lakini hebu tuone kwamba je, kwa nini Serikali isifikirie zaidi kwa kununua ndege ambayo itasaidia kunyunyiza dawa kwenye yale maeneo ambayo watakuwa wanahitaji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea zaidi kujikita kwenye suala la kilimo. Tumeona kwamba kwenye bajeti ya kilimo ni asilimia 4.9 ya bajeti, lakini bajeti hii bado ilikuwa haijafikia hata nusu ya lile Azimio la Maputo la mwaka 2003. Je, tujiulize, hivi ni kweli kabisa tunavyosema kwamba tunataka tufikie hatua ya kati na tunategemea mali ghafi kutoka kwa wakulima, kwa asilimia 4.9 ya bajeti yote, kweli tutafikia hilo lengo? Mimi naomba Serikali ione kwamba hili jambo inabidi tujipange upya kuhakikisha kwamba angalau bajeti ya kilimo nayo inafikia zaidi ya nusu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kwenye pembejeo hasa matrekta, kulikuwa na matrekta ambayo yalitolewa kwa wananchi wakakopeshwa. Labda tu mimi nipate ufahamu, yale matrekta yaliyokopeshwa, wale wananchi waliokopa, je, wamerudisha kwa utaratibu mzuri? Je, ni muendelezo gani ambao unafanyika kuwe kuna revolving kwamba wale ambao waliokopeshwa yale matrekta wanayarudisha na wananchi wengine zaidi wanafaidika kupata yale matrekta. Isiwe utaratibu kwamba watu wakiona kwa sababu matrekta haya ni ya Serikali basi mtu akichukua halipi. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kufahamishwa pia, je ni wananchi wangapi ambao pia wameendelea kufaidika baada ya wale wa mwanzo kuchukua mkopo huo? (Makofi)
Naomba pia nizungumzie suala la mifugo. Inasemekana kwamba miongoni mwa nchi ambazo zina mifugo mingi Tanzania pia ni mojawapo, lakini bado sekta ya mifugo haijaleta tija sana kwenye Pato la Taifa. Kwa hiyo naomba niishauri Wizara na nimshauri Waziri kwamba hebu katika bajeti kwa ajili ya ujenzi wa majosho, majosho kwa kweli bado yako katika hali mbaya sana, pamoja na dawa kwa ajili ya mifugo kwa sababu kama kweli tunasema kwamba tunataka tuanzishe viwanda vya kusindika na viwanda hivyo ni pamoja na viwanda vya nyama, sasa kama tukiwa na mifugo ambayo hali yake ni dhoofu kweli hivyo vya kusindika tutaweza kuvipata? (Makofi)
Naomba nishauri kwamba hebu tuone kwamba lazima suala la majosho liangaliwe upya lakini pia kuna baadhi ya yale mashamba ambayo yalitelekezwa kabisa, mashamba ya mifugo. Mashamba yale yamevamiwa na wananchi na mengine yameachwa zaidi ya miaka 22. Hebu tuone Serikali iwe na nia ya dhati ya kufufua mashamba yale ili kusudi sasa kama kweli tunataka kupata hivyo viwanda vya kusindika tuweze kuvipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi wamezungumzia sana kuhusu suala la afya na mimi pia naomba nizungumze. Katika bajeti yetu, Wizara ya Afya imetengewa asilimia 9.2 ambayo vilevile haijafikia lile Azimio letu la Abuja, Serikali ivute soksi kuhakikisha kwamba angalau tunafikia asilimia ile ili kuboresha afya za wananchi wetu. Kwa kweli inabidi Serikali ijipange zaidi, kwani tunapozungmzia afya, kama mtu asipokuwa na afya bora maana yake elimu haitakuwa bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.