Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ELIAS J. KWANDIKWA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika, kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia Hotuba ya Waziri wa Fedha. Hotuba ambayo ni muhimu sana; na nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuipongeza Wizara na Watendaji wote, na wote waliohusika kutuandalia kwanza Mpango ule wa Maendeleo kama tulivyousikia; lakini pia hotuba hii nzuri. Niipongeze kwa dhati kwa sababu ukiangalia bajeti hii utaona imezingatia mambo muhimu sana, imezingatia pia mwelekeo ambao tunautarajia. Ukiisoma bajeti hii utaona yako maeneo muhimu sana. Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, imezingatia maboresho ya mfumo wa kodi na tozo na mabadiliko makubwa sana na sura ya bajeti na mambo mengi ambayo tumeyaona. Kwa hiyo, nipongeze kwa dhati juu ya kuwa na bajeti nzuri namna hii, inatupa matumaini kwamba kweli tunaelekea kwenye uchumi wa kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba mwaka huu ni mwaka wa kizio (it‟s base year) kwa hiyo upo umuhimu wa kuangalia data na kumbukumbu zetu za mwaka huu kwa ajili ya kuweza kuzitumia siku za usoni; ili kuona mwelekeo wa ukuaji wa uchumi unavyokuwa kuanzia mwaka huu. Ni mwaka ambao tumekuwa na Rais mpya, mchapakazi na ambaye anadhamira ya dhati kutupeleka sehemu nzuri, lakini ni mwaka ambao pia tuna Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano mpya na yamkini pia tuna Waziri wa Fedha ambaye kama anavyoonesha kwamba atatusaidia sana ili tuweze kuona hali ya uchumi inakwenda kule tunakostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwa na mimi nichangie tu upande huu wa data zetu nikizingatia kwamba Ofisi ya Takwimu inafanya kazi nzuri. Nilikuwa nafikiri ni muhimu niseme kidogo hapa, kwamba hii Idara inafanya vyema. Lakini nilikuwa nafikiria nishauri idara hii sasa iwezeshwe kwa haraka ili tuweze kupata data ambazo zitatusaidia kufanya analysis zaidi tunapo kwenda mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu utaona kwenye kitabu hiki cha hali ya uchumi ile price index iliyotumika ni ya mwaka 2007, inaonesha pale nyuma ilikuwa ina shida kidogo ya uwezeshaji, lakini nilikuwa nafikiria kwa sababu tumeanza mwaka na mambo mapya ni vizuri sasa; hao wenzetu wa takwimu wawezeshwe mwaka huu ili basi tupate price index mpya ambayo itatufanya tuweze ku-determine ukuaji wa uchumi unavyokwenda kwenye hii miaka kumi inayofuata na tuweze kuwa na indicator mpya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu katika hali ya kawaida, tutazungumza kwamba hali ya uchumi inakuwa lakini utaona bado tunaweza kuwa na maswali mengi ambayo tunaweza kujiuliza. Kwa sababu kutakuwa kuna gape kati ya nominal income na real income hasa kwenye maisha yale ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba wakati tukizungumza juu ya kukua kwa hali ya uchumi lakini ukienda kule chini utaona kabisa kwamba bado kuna hali isiyo nzuri. Kwa hiyo Idara hii ya Takwimu iwezeshwe ili basi takwimu zinavyokuja hapa tuweze kuona zinaenda na hali halisi. Utaona kabisa kwamba kama ni mishahara itaonekana haitoshi kulingana na hali ya maisha, utaona kama ni bei ya mazao haitoshi kulingana na maisha. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiria kwamba Idara ya Takwimu iwezeshwe ili iweze kuleta uhalisia.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakuja kuona kwamba bado tuna income gape kwenye society, kwa hiyo, tuone hili gape likizibwa ili lisitupe nafasi ya kuburuza wale wanaoishi maisha ya hali ya uduni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuangalia kwenye kitabu cha hali ya uchumi, kumbukumbu nyingi zinaonesha zimechukuliwa hasa katika maeneo ya mjini, na sehemu kubwa utaona majedwali yanaonesha hali hii imechukuliwa katika masoko ya Dar es Salaam na yameacha kuchukua maeneo ambayo pia yametajwa kwamba ni maeneo ambayo yana umasikikini mkubwa, wananchi wanaishi chini ya mstari ule wa umaskini. Kwa Mikoa kama Kigoma, Geita, Kagera, Singida, Mwanza utaona kwamba upo umuhimu sasa hizi data zichukuliwe kwenye maeneo haya zikichanganywa na maeneo mengine, ili tukipata wastani uwe wastani ambao utakuwa unagusa wananchi walio wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nizungumze juu ya hii dhana ya ukuaji wa uchumi kwa ujumla hii; kwamba tunataka twende kwenye uchumi wa viwanda, tuwe na uchumi wa kati. Sasa nilikuwa najaribu kujiuliza, kwa sababu kama Mheshimiwa Waziri wakati anamalizia kusoma hotuba yake alizungumza juu ya umuhimu wa wananchi wote kutakiwa kushiriki katika kuhakikisha kwamba uchumi unakua. Lakini walio wengi tunaweza tusielewe tunavyozungumza juu ya tunahitaji kwenda kwenye uchumi wa kati. Je, wastani wa pato kwa mtu unatakiwa uwe wapi, iwe ni dola 1,500 kwa mtu au 3,000 kwa mtu?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo yako mambo ambayo tunahitaji pia ili wananchi wetu kwa ujumla, ambao pia kila mmoja ana mchango wake katika ukuaji wa uchumi, aweze kuelewa kwamba tunataka twende kwenye uchumi unaotegemea viwanda na biashara. Tunahitaji pia wastani wetu wa kipato kupanda kwenda dola 3,000 kwa mtu kufika mwaka 2025; kila mwananchi aweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hii pia itawezesha wananchi wetu wengi ambao bado hawajapata ajira, wapate ajira ili waweze kushiriki vizuri katika ujenzi wa uchumi. Lakini pia bidhaa zetu tutakazozizalisha katika viwanda ziwe na ubora kiasi cha kumudu ushindani katika masoko ya dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ni muhimu sana jambo hili litafsiriwe vizuri, wakati mwingine Wizara ifanye utaratibu wa kutoa vipeperushi virahisi ili wananchi mpaka aliyeko huko chini aweze kujua kwamba kwa pamoja tunaelekea wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipenda nishauri kwamba ni vyema tutafsiri vizuri ili wananchi waelewe, na hasa watumishi walioko kwenye Halmashauri na watumishi wengine, waweze kuijua hii dhana nzima ya kwenda kwenye uchumi wa kati na wa viwanda, na hivyo tuweze kuielewa vyema na kushiriki ujenzi wa uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niseme kwamba Serikali imechukua hatua nzuri kwa sababu hapo nyuma tulikuwa na matatizo makubwa ya kutokukusanya kodi kiasi cha kutosha. Sasa inaonesha kabisa kwamba Serikali inafanya juhudi kubwa ya kufanya makusanyo. Ukiingalia hii bajeti ambayo imekuja leo utaona kabisa kwamba ipo dhamira ya Serikali ya kufanya tutegemee mapato yetu ya ndani; hili ni jambo la kupongeza sana Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kulikuwa na tatizo la kutokutolewa kwa mafungu, kwamba mtiririko wake haukuwa mzuri. Naamini kama juhudi za makusanyo zitaongoezeka kile ambacho tumekipitisha hapa kikiweza kufika na kwa wakati tutayaona maendeleo kwa haraka. Pia ninaona Serikali ina dhamira ya dhati kwa kusimamia nidhamu ya makusanyo na matumizi. Mwanzo ilikuwa ni shida lakini kwa hali iliyoko sasa hivi inatutia matumaini kwamba tunakwenda kwenye mwelekeo mzuri. Kwa hiyo, nishauri tu, tuweke hamasa kubwa kwenye makusanyo ya mapato ya ndani ili tuweze kujitegemea, lakini pia tusimamie nidhamu katika ukusanyaji na matumizi ya rasilimali zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nizungumze kidogo juu ya sura ya bajeti. Kuna mambo ambayo nilikuwa nafikiri niweze kushauri. Kwanza napongeza ukuaji wa bajeti hii, kutoka trilioni 22 kwenda trilioni 29, si jambo dogo, ongezeko la zaidi ya asilimia 23, ni jambo la kuipongeza Serikali. Pia uwiano wa matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo umeongezeka. Nilikuwa nafikiria kwamba tuiangalie vizuri kwa baadhi ya maeneo, kwa mfano kwenye Halmashauri zetu au Serikali za Mitaa bajeti ya maendeleo iongezwe. Kwa sasa hivi tuna kama trilioni 1.3 ambayo tunaipeleka kwenye Serikali zetu za Mitaa. Hali itakapokuwa nzuri tusukume hizi pesa za maendeleo ziende zaidi kwenye Serikali zetu za Mitaa ili isaidie kuondoa baadhi ya matatizo yaliyo mengi huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa pia na juhudi za Serikali kuangalia suala zima la usimamizi wa kodi. Kwa hiyo, ni…
NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa Kwandikwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naunga mkono hoja.