Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba unisaidie niweze kutumia dakika zilizobaki za Mheshimiwa Ester Mahawe halafu na za kwangu niendelee kuzitumia. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianze kwanza na suala zima la uhifadhi wa misitu yetu. Mimi wakati mwingine huwa nashangaa sana. Sijabahatika wala sikufanikiwa kuwa mmoja wa waongeaji wa jazba sana; ndivyo nilivyoumbwa, halafu sioni ubaya. Lakini ninajaribu kuona namna ya kuwashawishi na kuwashauri Wabunge wenzangu, sisi ni viongozi, kuna mambo mengi sana yanaudhi, wala haina siri, lakini ukishakuwa kiongozi lazima uwe na kifua cha kuweza kumeza mambo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si swali la kujiuliza sana, ni kitu cha kawaida kabisa kwamba hakuna hata mmoja wetu hapa ambaye hajui umuhimu wa kutunza misitu yetu. Ni jambo lililo wazi kabisa kwamba mifugo ina faida kubwa sana kwa nchi yetu, lakini nakuhakikishia, mifugo haiwezi kuwepo kama tutaruhusu hii misitu yetu inayotuletea mvua ili misitu ichipuke na wanyama wapate mahala pa kulishwa, kama itateketea. Nchi itakuwa jangwa kama tukiruhusu mifugo iingie kwenye hifadhi na kuanza kulisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanaotoka mikoa ya wafugaji wanajaribu kujenga hoja tu kwamba ng‟ombe hawana tofauti na nyati. Hebu wajaribu kufuatilia vizuri, wana tofauti kubwa sana na nyati. Miaka 30 iliyopita kwenye miaka ya 1980 Shinyanga ilivyo leo haikuwa hivyo na mifugo ilikuwepo na hakukuwa na contradiction yoyote na misitu nayo ilikuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba sana, Waheshimiwa Wabunge tuuone ukweli, nchi yetu itageuka kuwa jangwa na hii mifugo tunayoitetea leo haitakuwa salama wala haitakuwa hai kama nchi yetu itakuwa jangwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache siasa, tuwaambie wananchi wetu ukweli. Kwenye kampeni watu wote tumezungumza mambo mengi, lakini sasa turudi tuwaambie ukweli kwamba tukiruhusu sasa mifugo ikaenda kulisha kwenye misitu yetu nchi itakuwa jangwa, kwa hiyo, hata hiyo mifugo nayo itakufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko ninakotoka Wilayani kwangu Kibondo ukihesabu mifugo ya wananchi wa Wilaya ya Kibondo, naomba nisizungumze kama mbaguzi, haizidi 60,000, lakini kwenye Pori la Moyowosi tuna ng‟ombe zaidi ya 300,000, kila siku ni ugomvi, kisingizio ni kwamba wanakwenda kunywa maji Mto Malagarasi, sasa hivi kina cha Mto Malagarasi kimeshuka, nchi inakwenda kuwa jangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuchangia kuhusu suala la wanyamapori na uhifadhi na nitaongelea Pori la Moyowosi au Kigosi. Suala la ujangili linaendelea kutetemesha sana nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kibondo kuna ofisi kubwa sana ya Moyowosi, nilifanikiwa kwenda kutembelea pale, nikaongea na wafanyakazi kama mwanakamati wa Kamati ya Maliasili na Utalii. Nilipata changamoto zao nyingi sana, Mheshimiwa Waziri naomba uzishike. Pale kwenye ile ofisi wana magari matatu mazuri kabisa, lakini OC haifiki, matokeo yake wanaweza wakasikia bunduki ya kuua mnyama imelia somewhere lakini mafuta ni mpaka waombe kwa wale waliomiliki vitalu, hiyo ni aibu. Naomba sana hilo Serikali ilitilie umuhimu na iwasaidie sana wale wahifadhi waweze kufanya kazi zao bila matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nitakwenda kwenye sekta ya utalii. Si siri ndiyo sekta ambayo inaingiza fedha nyingi sana za kigeni kwa Taifa letu. Ina-contribute 25 percent ya fedha za kigeni katika uchumi wa nchi yetu, lakini sekta hii bado haijapewa kipaumbele cha kutosha, tunaomba sana Serikali sasa igeuze macho, iangalie sekta ya utalii. Tukiwa kama nchi ya pili kwa vivutio vingi vya utalii baada ya Brazil hatustahili kuwa hapa tulipo. Tunatamani nchi yetu i-contribute hata 50 percent ya Pato la Taifa kupitia utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo litawezekana tu kama tutawezesha Bodi ya Utalii kufanya matangazo stahiki. Bodi ya Utalii ya Tanzania kwenye bajeti iliyopita haikufikia hata Shilingi bilioni tatu ilizopewa kwa ajili ya kufanya matangozo ya utalii. Matokeo yake Bodi ya Utalii ya nchi jirani ya Kenya ilipewa zaidi ya bilioni 50 kufanya matangazo ya utalii kwa ajili ya nchi ya Kenya, ambayo unaweza ukaenda kwenye mbuga mojawapo ya kwao ukazunguka kilometa sita ukaona swali mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kutokana na matangazo wanayoyafanya watalii wengi wanashuka Kenya, wanadanganywa danganywa, uongo uongo weanakuja kuangalia wanyama kwetu halafu wanarudi Kenya wanaingiza pesa nyingi sana Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wala sishangai sana kuona kwamba hata Mlima Kilimanjaro, Kenya ndio wanaoutangaza zaidi kuliko Tanzania, hiyo ni aibu.
Ninaomba sana Bodi ya Utalii iwezeshwe, ipangiwe fungu kubwa la pesa ili iweze kutangaza utalii wetu na nchi iweze kufaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mali kale. Nilipata mshituko mkubwa sana, kama miezi miwili iliyopita nilipomuona binti mmoja wa Kikenya akiitangazia dunia kwamba Olduvai Gorge iko Kenya na kwamba sasa dunia iende ikaangalie unyayo wa mtu wa kale kabisa duniani ambao unapatikana Kenya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, Serikali ilichukua jukumu la kukemea na wale wakakanusha. Lakini kusema kweli tayari damage iliyofanyika kwa yale maelezo ya yule binti ni kubwa sana hayawezi kukanushwa tu kirahisi rahisi kama vile na ikaweza kuleta impact kwa uchumi wetu wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Serikali ichukue juhudi za makusudi za kuhakikisha vivutio vyetu vinatangazwa na TANAPA, TTB pamoja na Ngorongoro. Bila kufanya hivyo wenzetu wataendelea kuchukua advantage ya sisi kukaa kimya na tutaendelea kupata shida ya kutopata mapato stahiki kutokana na vivutio ambavyo Mungu ametujalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa TDL. Ninazo taarifa kama Mwenyekiti wa Kamati ni-declare interest kwamba kuna three percent ya gross ambayo inatakiwa iende kuimarisha Chuo Cha Utalii, iimarishe TTB na shughuli za ku-promote utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mashaka kama hiyo pesa kweli inafika, naomba sana hili lifuailiwe ili TTB ipate nguvu, lakini na Chuo chetu cha Utalii ambacho kwa hapa Afrika ya Mashariki ni chuo cha kipekee sana kiweze kupata facilities za kuwafanya vijana wetu waweze kujifunza utalii, na ajira nyingi kwenye hoteli zetu zichukuliwe na Watanzania badala ya kuchukuliwa na watu kutoka nchi jirani zinazotuzunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa nizungumzie Chuo cha Misitu cha Olumotonyi. Wakati tunafanya ziara ya kamati tulizungukia chuo kile, kila hali mbaya sana. Tunaiomba sana Serikali, ukitaka kupata faida lazima uwekeze. Huwezi kutegemea kuvuna kama hujalima na kupanda. Kinachoonekana sasa hivi Serikali inataka ivune mahala ambapo haikupanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Misitu ni chuo muhimu sana kwa maendeleo ya Tanzania, ni chuo cha kipekee kwa Afrika Mashariki na Kati kinachofundisha watu uhifadhi wa misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana kipewe kipaumbele, kiwezeshwe fedha, kiongezewe bajeti ili kiweze kutufundishia vijana wetu tuweze kupata tija kutokana na chuo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo naunga mkono hoja.