Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hotuba hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kusema kwamba naunga mkono hotuba hii ya bajeti. Mheshimiwa Profesa Maghembe anahitaji apate fedha akafanye kazi. Pamoja na yote hayo, kuna changamoto nyingi sana ambazo ningeomba leo Mheshimiwa Waziri anisikilize. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo sasa hivi ni tatizo la wafugaji na hifadhi za akiba au mapori ya akiba yanayomilikiwa na TANAPA. Tunapoangalia sasa hivi tunaona kwa udogo wake lakini naona kuna mfukuto mkubwa sana unaweza kujitokeza na ukaleta matatizo ya kijamii katika nchi yetu. Leo hii mfugaji hathaminiwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana wafugaji wanapoingiza mifugo kwenye pori, ni kinyume cha sheria tunafahamu, lakini kwa sababu mazingira jinsi yalivyo hatujaweza kujenga utaratibu mzuri na mahusiano mazuri kati ya wafugaji, wakulima na hifadhi zetu za Taifa. Tunajua kwamba sheria inakataza na Mheshimiwa anasimamia kwenye sheria, lakini bado kuna tatizo kubwa kwamba ni namna gani tuweke matumizi bora ya ardhi ili mfugaji huyu naye aone kwamba anathaminiwa na anapewa nafasi katika nchi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mahali katika nchi hii unaweza ukapuuza wafugaji, haiwezekani! Lazima wapewe nafasi yao na lazima waoneshwe ufugaji bora na wa kisasa au ufugaji ambao ni endelevu. Leo hii ardhi haiongezeki lakini watu wanaongezeka na mifugo inaongezeka. Mara nyingi tusipokuwa wabunifu na naomba Mheshimiwa Waziri anapokuwa anahitimisha hotuba yake hii hebu atuambie katika Wizara yake amejipanga vipi kuweka mkakati kuona kwamba, hawa wafugaji wanapewa stahiki yao, wanaelimishwa, wanasaidiwa namna ya kufuga vizuri lakini pia waboreshe mazao ya mifugo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii haiwezi kutokea hivi hivi kama Serikali haiweki mkakati madhubuti. Kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri amesema lakini hajagusia namna gani anaweza kumsaidia mfugaji. Ameangalia zaidi sheria za kulinda hifadhi za Taifa, tunapenda ziwepo lakini bado kuna umuhimu wa kumsaidia mfugaji ili naye aweze kuona ubora na faida ya kufuga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili lipo katika maeneo ya Kijeleshi. Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyokuja katika ziara ya Mkoa wa Simiyu alikuta matatizo katika Wilaya za Busega, Bariadi, Itilima na Meatu. Ina maana ukanda mzima wote wa Simiyu una mgogoro mkubwa sana na tusipotafuta ufumbuzi wa haraka ni tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha ajabu baadhi ya askari wa wanyamapori si waadilifu na si waaminifu kwani wanawatesa wafugaji hawa, wanatesa mifugo hii. Mheshimiwa Waziri alitoa tamko wakati nauliza swali hapa Bungeni alisaidia mifugo 6,000 iliyokuwa imefungiwa porini kwa siku tatu na wanaomba rushwa, wanaomba hela na wakipewa hela hazifiki zinapotakiwa kwenda, hazikatiwi risiti yoyote ile. Namwomba Mheshimiwa Waziri pamoja na watu wake hili suala likemee kwa nguvu zote na naomba tupate ufumbuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hiyo haitoshi suala hili ni mtambuka, lazima Waziri wa TAMISEMI, Waziri wa Ardhi, Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo na Waziri wa Maliasili washiriki kikamilifu. Tusipopata solution itatupa shida sana huko tunapoelekea. Leo wafugaji wanagombana na wakulima, wanagombana na hifadhi, tutafika wapi? Namwomba sana Mheshimiwa Waziri tusaidie katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu suala zima la kudorora kwa sekta ya utalii. Tunajua uchumi wa dunia umebadilika sana, lakini napenda kuona Mheshimiwa Waziri anakuja na mkakati. Biashara ya utalii inazidi kudorora lakini ukiangalia biashara ya utalii imekuwa ikiingiza mapato makubwa sana katika nchi hii. Leo hii mahoteli hayana watu, hayana biashara, migahawa haina biashara, watalii hawaji na bado hizi gharama zingine za kuendesha utalii ni kubwa mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachomwomba Mheshimiwa Waziri hebu ajaribu kutusaidia kuja na package namna gani ya kuweza kufufua suala zima la utalii katika nchi yetu. Tusione kwamba watalii wanakuja tunafurahia, lakini tuone wanakuja na kutuma fedha ili ibaki hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda kuzungumzia ni suala zima la geti ya Ndabaga ambayo ndiyo kielelezo na kioo cha Western Corridor upande wa Serengeti, lakini ukifika pale lile geti hali-reflect kwamba unaingia kwenye hifadhi kubwa ya Serengeti, limechakaa, liko hovyo hovyo, halina ukarabati wowote ule. Naomba haya mapokezi yaweze kuboreshwa ili kusudi hata mtalii anapokuja aone kwamba nimeingia kwenye kioo cha hifadhi kubwa hapa duniani, naomba Waziri alizingatie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kumgusia Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, nikamwambia tujitahidi kuboresha kwa sababu wanasema reception counts before somebody enters into the house, kwa maana kwamba mapokezi ya nyumba, unapofika pale mbele ya uso wa nyumba ndiyo kielelezo kwamba nyumba yako iko vipi kwa ndani. Naomba sana hilo tuweze kulifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine ni suala zima la Hifadhi ya Sayaka, ni pori la akiba la zamani. Mheshimiwa Kiswaga aliwahi kuuliza hapa swali, ile hifadhi haipo, hakuna miti, hakuna nini, huwezi kusema ni hifadhi, wananchi wanalima, mazao yanakatwa eti ni hifadhi. Naomba jamani unyanyasaji wa namna hii tuachane nao. Namwomba Mheshimiwa Waziri atume watu wake waende kwenye hifadhi ya Sayaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Sayaka iko katika Wilaya tatu za Magu, Bariadi na Busega. Kwa upande wa Busega kuna Kata za Nyaruhande na Badugu na upande wa Magu Kata ya Sayaka. Naomba tuangalie kwa ukaribu kama tunadhani ile ardhi haina maana tena ni bora tukajaribu kuacha sehemu za vyanzo vya maji ili wakulima waweze kufanya kilimo cha kujikimu, watu wapate chakula. Leo watu wanalia wana njaa na mnasema kuna hifadhi ambayo imezuiwa wakati haipo. Kwa hiyo, naomba sana hili suala liweze kuangaliwa vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine ni suala la tembo waharibifu. Sisi watu wa Busega na sasa hivi nimepata message nyingi wanalia kwamba tembo wanavamia, wanakula mazao yao na kuharibu mashamba yao na hakuna fidia yoyote ile. Naomba Mheshimiwa Waziri tutafute mkakati mbadala wa kujaribu kuzuia wanyama hawa ambao wanakuja kushambulia binadamu pamoja na mazao yao, matokeo yake wananchi wanalima sana lakini siku ya siku wanakosa faida, hawawezi kuvuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la hii Operesheni Tokomeza. Kuna watu walinyanga‟anywa silaha zao wakati wa zoezi hili, silaha zao za jadi na silaha zingine ambazo walikuwa wamezisajili hazijarudishwa mpaka leo. Hivi Mheshimiwa Waziri nini dhana nzima ya kuwasaidia wananchi hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Waziri anapohitimisha hotuba yake atuambie ni nini hatma ya watu hawa ambao silaha zao zilichukuliwa wakati wa zoezi hili la Operesheni Tokomeza. Kwanza tujue silaha hizi ziko wapi na zinafanya nini na je, watarudishiwa? Ni vema haya yote Mheshimiwa Waziri akayaweka vizuri na nilishazungumza naye anayafahamu, ili kusudi hawa wananchi waweze kupatiwa haki yao bila kuwa na matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine utalii lazima tuendelee kuu-embrace vizuri. Leo hii Watanzania unafika airport…
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.