Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema, kuniwezesha kusimama leo na kutoa mchango wangu katika mada iliyoko mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuongoea katika Bunge hili, naomba pia nichukue fursa hii kuwashukuru wapiga kura wa Jimbo la Malinyi, Jimbo hili siyo jipya tumebadilisha jina zamani lilikuwa linaitwa Ulanga Magharibi. Nawashukuru sana kwa kunirudisha kwa awamu ya pili najua wana imani kubwa kwangu na naomba niwaahidi kwamba, sitawaangusha, nitawatetea, tutafanya kazi pamoja kuleta maendeleo katika Jimbo na Wilaya yetu mpya ya Malinyi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu Malinyi na Wilaya ya Ulanga. Mvua zinaendelea kunyesha, mvua hizi zimeleta madhara makubwa, zimeharibu miundombinu, zimeharibu na mashamba. Sasa hivi ninavyozungumza maeneo mengine hayafikiki kabisa, kutokana na uharibifu wa barabara uliosababishwa na hizo mvua. Kama mtakumbuka siku ya Jumanne, nimetumia Kivuko kile kilichozama Kivuko cha Kilombero, saa kumi na mbili jioni nimetoka Jimboni nimetumia kile Kivuko, lakini saa moja na nusu Kivuko kilekile kimezama na kimepoteza ndugu zetu pamoja na mali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Serikali wamekuwa karibu sana na wananchi na wamekuwa wasikivu mara moja, siku ya pili asubuhi tulikuwa na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Profesa Mbarawa, ameahidi na nawaomba tafadhali Serikali ahadi ambazo mmeziahidi naomba niwakumbushe maana muda unakwenda. Ahadi ya kwanza ya kurudisha haraka mawasiliano, Ulanga na Malinyi wako kwenye Kisiwa, kwa hiyo tumeahidiwa mawasiliano yatarudishwa, pamoja na ngalawa zilizoletwa, au boti zile za Wanajeshi hazitoshelezi. Tuliomba na tunaendea kuomba, warudishe kivuko kingine pale, maana bila kivuko pale jamani wale watu wanaishi katika maisha hatari na wale watu wanaishi katika maisha magumu gharama za bidhaa zinazidi kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inayotishia nyingine stock za dawa zinakaribia kuisha mwishoni mwa wiki hii, hatujui baada ya wiki hii tutaishije kwa wale ambao watapata bahati mbaya ya kuugua. Pamoja na maombi hayo na kwa kuwa Serikali imeahidi, tunaomba ahadi ile itimizwe, umaliziaji wa ujenzi wa lile daraja la Kilombero. Serikali wameahidi kwamba kabla ya mwezi wa 12 mwaka huu daraja lile litakuwa limekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, sasa naomba nijikite mchango wangu katika mada iliyokuwa mezani kwetu na nitajikita katika maeneo matatu, mawili hasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu ugharamiaji wa Mpango huu. Tumeshuhudia na taarifa ambayo tumeipokea bado miradi mingi kutegemea na Mpango wa mwaka jana, haikuweza kutimizwa. Changamoto kubwa hatuna fedha ya kutosha, wenzangu wameshauri, na mimi ninashauri ile ripoti ya Chenge one, ripoti ya Chenge two ifike muda sasa Serikali mtusikie, muanze kutekeleza hasa ninyi wataalamu ripoti ile imechimba kwa kina zaidi na wataalam hao kwenye Kamati ile tunaendelea kuishauri mtekeleze angalau machache muone namna gani mnaweza mkaongeza pato la nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutegemea na taarifa ya ripoti ya tafiti iliyofanywa na Dkt. Ngowi na wenzake wa Chuo Kikuu cha Mzumbe wakishirikiana na Norwegian Church Aids imebainika kuna upungufu mkubwa, watu hawalipi kodi. Wale wanaostahili kulipa kodi karibu milioni 15 nchi hii hawalipi kodi na asilimia ambayo imetoa ile ripoti ni asilimia 12 tu ndiyo wanaolipa kodi, maana yake nini asilimia 88 nchi hii tunakosa mapato. Kwa hiyo, kama Serikali wakija na mfumo mwingine na wigo wakiupanua zaidi, haya mambo tunayozungumza hapa, miradi inashindwa kukamilika itakuwa imefikia mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri Wizara hii ya Fedha na Mipango, hebu wasilianeni, muungane na watu wa NIDA, iwapo kama wenzetu wa NIDA watamaliza zoezi la Utambulisho wa Kitaifa, ni rahisi kuoanisha zile nationa ID na kumbukumbu za watu hao ambao wanakwepa siku zote kulipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili, utahusu maeneo wezeshi kwa viwanda, na nitayabainisha maeneo kama matatu ama manne. Tunazungumzia viwanda ambavyo tunavyovilenga ni vile viwanda vitatumia malighafi ya kilimo, mifugo na uvuvi. Nikitoa mfano katika maeneo ambayo ninatoka maeneo ya Wilaya ya Malinyi, Kilombero na Maeneo ya Wilaya ya Ulanga. Maeneo haya yamebainishwa katika Mpango wa SAGCOT lakini kwenye Mpango huu wa mwaka huu, hakuna chochote kinachozungumzia SAGCOT. Jamani mpango ule ni kuwawezesha wakulima kulima kilimo cha biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kilimo cha biashara kitoe tija kuna mambo manne tu, kuna suala la nishati, miundombinu, maji na masoko. Suala la nishati Jimbo letu la Malinyi, ni vijiji 20 tu ndio vimeunganishwa na ule mradi wa REA kwa umeme. Kama vijiji vyote vingepata umeme hii ingekuwa na tija sana kwa wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na upande wa pili kuongeza ajira kwa watu wanaojihusisha na kilimo, sasa niiombe basi Serikali wamalizie ile miradi ya REA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba ili kilimo kiwe na tija kuwe na barabara. Barabara zetu Wilaya ya Malinyi, Ulanga ni aibu, sasa hivi huwezi kufika maeneo mengine kwenye Wilaya ya Malinyi, kama ile Tarafa ya Ngoilanga ina watu 60,000 lakini leo hawafikiki kabisa sababu ya ubovu wa barabara. Mkandarasi yuko site, lakini amekimbia kwa sababu Serikali wenyewe wanajua, kwa hiyo naomba nisisitize katika mpango huu.
La kwanza, malizieni ile barabara ambayo tunaizungumizia, kuanzia Kidatu, Ifakara, Lupilo kwenda Mahenge, kutoka Lupilo kwenda Malinyi Kilosa kwa Mpepo, Londolumecha - Namtumbo. Barabara hii yenye kilometa 396 ni muhimu sana. Maana siku zote mnaendelea na mchakato. Hata kwenye taarifa hii mliyoiandika watu wa mipango bado mmeweka barabara hii inaendelea na mchakato ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri, kwa sababu Mkandarasi yuko site, mumuongezee spidi amalizie huo mchakato wa upembuzi yakinifu. Baadaye tuzungumzie mwaka kesho tuanze kujenga hii barabara. Haitakuwa na tija tu peke yake kwa wakazi wa maeneo haya, barabara hii ni shortcut ya kutoka Mikoa ya Kusini kuja Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nimalizie ya mwisho kuhusu Utawala Bora. Wilaya ya Malinyi ni mpya na Wilaya hii ipo pembezoni, tunaomba mtuwezeshe ujenzi wa majengo ya Wilaya hii.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako tayari umekwisha.
MHE. DKT. HADJI HUSSEIN MPONDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)