Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchangia bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirejea hotuba yangu ya Wizara ya Viwanda, Waziri wa Ardhi nilimshukuru kwa kumtaja jina na hii ni kutokana na namna Wizara hiyo inavyoshirikiana na Wizara yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna moja napenda niliweke wazi, wawekezaji njoo muwekeze Tanzania na ninyi Watanzania mchangamkie kuwekeza, hatuna tatizo la ardhi. Mama mwenye nyumba wangu alipata nafasi ya kuzungumza akasema viwanda mtavijenga wapi, viwanda tuna maeneo ya kutosha. Ukisoma ukurasa wa 135, jedwali namba 11 la bajeti hii, miji kumi tu imeeleza maeneo yaliyopangwa lakini hayo ni hayo tu. Pia ukienda kwenye jedwali la TIC (land bank) kuna hekta 500,900 zinazoonyesha maeneo yaliyotengwa mahsusi kwa ajili ya kilimo na hasa kilimo cha miwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumueleza Mheshimiwa Kamanda Silinde kwamba mwekezaji niliyekuwa namwambia ameshaweka timu Songwe, anakwenda jimboni kwake, anakwenda kulima miwa na anategemea kuzalisha tani 120,000 za sukari. Nayasema haya kuwatoa wasiwasi watu wasije wakadhani kwamba nchi ya Tanzania haina ardhi na Wizara ya Ardhi haijanitengea ardhi. Niwashukuru sana, nikushukuru na mueleze bosi wako kwamba Mwijage amekushukuru sana ulipokuwa haupo kwenye kiti chako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetenga ardhi ya kutosha kwa ajili ya kujenga viwanda vya sukari na kilimo cha miwa. Mbunge wangu wa Temeke leo asubuhi aliniuliza swali likanipa shida juu ya hali ya sukari nchini. Niwahakikishie tunayo sukari ya kutosha.
Tumechukua jitihada za kawaida za kutenga maeneo, kwa mfano lipo eneo la Kigoma ambapo hekta 47,000 zitatengeneza kiwanda cha Kigoma Sugar, nimelizungumza hili la Songwe, tutaendelea na Songwe, lakini Kagera Sugar wanaozalisha tani 60,000 wanapanua eneo la Kitengule wazalishe tani 60,000 nyingine. Aidha, watu wa Oman wataingia ubia na Kagera Sugar ili kuzalisha tani 300,000 kutoka pale. Kwa hiyo, hii adha tunayopita ni kwamba tuliamua kudhibiti uingiaji wa sukari ili kuwajengea hamu wawekezaji waweze kuingia katika shughuli hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, adha iliyokuwepo sasa inakwenda kuisha, tunayo sukari ya kutosha, kuna maeneo yana matatizo, kuna Mbunge wa Mwanza ameniuliza kwamba Mwanza sukari iko wapi? Leo Mwanza hali ni mbaya, kilo moja ya sukari shilingi 4,000. Baada ya kunieleza, Bukoba wanapakia tani 600 kwenda Mwanza na kiwanda cha Kagera Sugar kimeanza kuzalisha leo, ni tani 250 zinazalishwa. Tarehe 25 Mei, Kilombero (K1) inaanza kuzalisha na wakimaliza kuzalisha full swing ni tani 600 kwa siku. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuwe na imani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi yaliyochukuliwa yalijenga imani na kuwaleta wawekezaji hapa ndani.
Ngoja nitoe maelekezo mama unielewe, niko kazini hapa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetoa maelekezo wafanyabiashara wote mnaoshughulika na sukari mkajitambulishe kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ili sukari mnayopewa Dar es Salaam muifikishe kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya waione.
Tayari zimeshatoka tani 10,000 kwa ajili ya kusambazwa, lakini kuna tani 31,000 ziko njiani zinakuja. Ngoja niwaeleze jambo moja, matumizi ya nchi ni tani 1,200 kwa siku, Kagera Sugar inazalisha tani 250, Mtibwa inazalisha tani 600, deficit ndiyo hiyo niliyowaeleza iliyoagizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie kwamba maeneo ya ujenzi hayana shida. Nichukue fursa hii kuwapongeza tena wale viongozi mnaokwenda mbele zaidi kutambua maeneo yenu na kuyapeleka Wizara ya Ardhi ili yapimwe. Nichukue fursa hii kuwapa pole Waheshimiwa Wabunge wa Tabora. Wabunge wa Tabora walinipa ardhi, nikatafuta mwekezaji, mwekezaji alipokuwa anapanda ndege akazuiliwa asiende Tabora. Niliwaambia wakati wa bajeti yangu kwamba ujenzi wa viwanda ni vita, kwa hiyo, vita hiyo nitaishinda, nitawasaidia watu wa Tabora, nitamleta hata kwa baiskeli huyo mwekezaji ili twende Tabora tuweze kuwekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu ambalo kimsingi halitafanikiwa kama sisi Waheshimiwa Wabunge hatutalisimamia. Tumeagizwa au imekubalika na Serikali kwamba katika maeneo ya vijiji na kata, tutoe maeneo tuyarasimishe, twende tuyapatie hati ili vijana wetu waweze kuanzisha shughuli na biashara ndogo ndogo. Kuna fursa zinakuja za ujenzi wa silos (godown), maeneo mtakayoyatoa kama alivyozungumza Mbunge mmoja yataweza kutoa nafuu katika ku-acquire ile land na kuweza kuweka infrastructure bila kutumia gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yaliyotengwa yapo kama nilivyowaeleza, yapo maeneo ya Mkurazi yameelezwa na nimeiona Momba hapa nimeiona imetengwa. Niwaeleze ukweli, nimepewa jukumu lingine bahati mbaya, nimsemee Mheshimiwa Mwigulu. Mheshimiwa Mwigulu maneno anayozungumza siyo hadithi za kufurahisha watu. Tuombe Mwenyezi Mungu atusaidie kabla ya mwaka huu kuisha nitakuwa na mtambo tayari wa kuunganisha matrekta 2,500 hapa Tanzania na matrekta hayo yatakwenda kulima ardhi hizi. Kwa hiyo, tunachopaswa kufanya Watanzania wenzangu, unapopata ardhi isalimishe kwa Mheshimiwa Lukuvi, Wizara ya Ardhi ili ardhi hiyo tuweze kuifaidi Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maelezo hayo mimi niseme Wizara yangu iko vizuri lakini niwatoe wasiwasi wawekezaji, msiwe na wasiwasi ardhi ipo. Nimetoa mfano wa Nzega, Maswa na Kagera ambako wananchi wametoa maeneo. Hata hivyo, mnapotoa maeneo nendeni mkayarasimishe Wizara ya Ardhi ili mpate title ili mwekezaji anapokuja iwe rahisi kuwekeza. Napozungumzia wawekezaji sizungumzii wa kutoka nje, mwekezaji ni pamoja na wewe. Tujenge kiburi, tujiaminishe na sisi tuanze kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.