Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kupata fursa hii ya kuweza kuchangia hoja hii ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kwanza, napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Lukuvi alikuja Muheza na alituletea ahueni kutokana na ziara yake hiyo. Wananchi wa Muheza wanamshukuru sana kwa sababu aliweza kurudisha mashamba karibu matano ambayo yanaonekana kwenye ukurasa wa 104 wa hotuba yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mashamba hayo ya katani yamekuwa ni ahueni sana kwa wana Muheza kwani yalikuwa yanawafanya wana Muheza wawe vibarua tu wa mashamba ya katani. Sasa hivi tunatengeneza mipango maalum ya kuhakikisha kwamba tunakuwa na master plan ya Wilaya ya Muheza ili kuhakikisha kwamba mashamba hayo ambayo tumeyapata yanakuwa kwa manufaa ya wana Muheza. Wananchi watagawiwa maeneo yao ambayo yapo na tutatenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kitu muhimu sana ambacho tumekiweka na tunakisisitiza na tunahakikisha kwamba kwa kweli tunataka kuibadili Muheza. Nashukuru kwamba Waziri wa Viwanda yuko hapa, Waziri wa Kilimo yuko hapa, Waziri wa Miundombinu yupo hapa, Waziri anayeshughulika na TANESCO yuko hapa, Waziri wa Maji yuko hapa, tatizo sasa hivi linalotupata ni miundombinu, hatuna tatizo tena la ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua baadhi ya mashamba hayo yamevamiwa, lakini wana Muheza ni watu waungwana tutakaa chini, tutaongea na tutaona namna ya kutatua tatizo hilo. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na tunataka kuhakikisha kwamba ardhi hiyo tunaitumia ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili ni kwamba, yapo mashamba mengine ambayo bado hayajafutiwa hati. Mashamba ambayo yameshafutiwa hati ni kama shamba la Lewa, Bwembwera, Luhuwi, Kilapula, Kwa Fungo, Kihuwi lakini shamba la Kibaranga na Azimio bado sijayaona kwenye hiyo list. Kwa hiyo, tutashukuru kama mashamba hayo pia na yenyewe yataweza kufutiwa hati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo pia mashamba ambayo wanamiliki watu lakini hawalimi katani jinsi inavyotakiwa kulimwa. Wengine wanalima katani pembeni pembeni ili ukipita uone kwamba hili shamba linalimwa lakini ukienda katikati kuna pori kubwa sana. Nitampa Mheshimiwa Waziri list ya mashamba hayo na yenyewe pia tufanye mpango kwa wote ambao wanaweka mapori Muheza, mashamba hayo tuweze kuwanyang’anya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Waziri alipokuja alijionea mwenyewe watu walikuwa wengi sana, migogoro ya ardhi ni mingi sana na hii ambayo imeoneshwa kwenye page 33 kwamba ni migogoro sita ipo mingine ambayo sijaiona hapa na ambayo nitaiorodhesha na kumkabidhi. Hata hivyo, napenda kumshukuru kwamba migogoro hiyo imeanza kushughulikiwa. Mwezi uliopita timu yake ilikuwa Muheza na imeanza kutatua migogoro hiyo, napenda kumpongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migororo hii ya ardhi najua iko mingi, lakini nina hakika kwamba yote tutaitatua kwa wema tu na tutaelewana vizuri na wananchi wataelewa vizuri tu. Kwa hiyo, hii mingine iliyobaki Waziri pamoja na timu yake ningefurahi sana kama ningeambiwa watarudi ili waweze kushughulikia matatizo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Nyumba linafanya kazi nzuri ya kujenga nyumba, lakini kama walivyosema wenzangu tatizo kubwa ni bei zake, VAT iliyoko pale ni hela nyingi sana haina unafuu wowote kwa mwananchi. Sisi Muheza tumeshawapa eneo sehemu za Kibanda lakini tungeomba msukumo wa Waziri, tunataka wajenge nyumba za bei nafuu ili wananchi wa Muheza waweze kununua nyumba hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Rais ameshatoa maelekezo haya mashirika yetu sasa yawekeze kwenye viwanda na mashamba na sisi tunayo mashamba na sehemu za kuweka viwanda. Ningependa shirika hili liwe mfano waje Muheza tuwape eneo waweke viwanda, tunataka kutengeneza kitu kinaitwa economic corridor ya Muheza. Kwa hiyo, nafasi tunazo na ningeshukuru sana kama National Housing watakuwa wa kwanza kuja kuwekeza Muheza na tunawakaribisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ambalo tunalo pamoja na kuwa na mashamba hayo ni la vifaa kwenye Ofisi ya Ardhi, kwani vifaa hakuna kabisa inabidi tukodi labda kutoka Korogwe au Mkoani Tanga. Ningeomba Waziri awasaidie wale vijana wa pale ili wapate vifaa vya kupimia, tuanze kazi ya kuangalia tunapima namna gani kufuatana na master plan ambayo tutaitengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kumwomba Waziri kwamba awasaidie TIC (Tanzania Investment Center) wawe na land bank inayoeleweka. Wana shida sana pale ya land bank. Wafadhili wanakwenda pale wanataka kuwekeza, wanataka kuleta mambo chungu nzima lakini land bank ambayo wanayo TIC ni ya watu binafsi. Kwa hiyo, ningeshukuru sana kama Waziri atashughulika na kuwasaidia TIC waweze kuwa na ardhi, mwekezaji anapofika anapelekwa moja kwa moja kwenye site na kuoneshwa kwamba ardhi hiyo hapo badala ya mwekezaji kuanza ku-negotiate na mtu binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, namtakia Mheshimiwa Waziri kila la kheri na tunamkaribisha Muheza. Wana Muheza wanamkumbuka kwa jinsi alivyowaletea ufumbuzi na tunamhakikishia ardhi hiyo tutawagawia wana Muheza na tutaweka sehemu maalum za uwekezaji na tunawakaribisha sana. Nawashukuru sana.