Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mezani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri Lukuvi na Naibu Waziri Angeline Mabula kwa kazi nzuri wanayoifanya kuisimamia Wizara hii nyeti kwa Watanzania. Pia niendelee kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuleta mabadiliko kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la migogoro ya ardhi katika Jimbo langu la Karagwe. Katika hili niishukuru Serikali kwa kuwa wasikivu kwani tayari Jimbo la Karagwe tumeshatembelewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kutatua migogoro ya ardhi na changamoto nyingine za maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu alitutembelea, Mheshimiwa Profesa Muhongo, Mheshimiwa Mwijage, Manaibu watatu, kaka yangu Mheshimiwa Injinia Ramo, kaka yangu Mheshimiwa Masauni na Mheshimiwa Dkt. Kalemani. Hii ni kuonesha jinsi gani Serikali ya Awamu ya Tano inavyochapa kazi, tunawaunga mkono na kabla ya yote, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo matatu ya kuchangia na nianze na suala la land bank yaani benki ya ardhi. Upungufu wa viwanja vilivyopimwa ni changamoto ambayo iko nchi nzima na Serikali ya Awamu ya Tano kama wananchi wote wanavyofahamu ni Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda. Huu uchumi wa viwanda hatutaujenga mbinguni bali ni kwenye ardhi, kwa hiyo ni muhimu sana tukatatua migogoro ya ardhi kote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Mkoa wa Kagera, ukipata mwekezaji mkubwa bado tuna changamoto kubwa ya ardhi. Maeneo yanaonekana yapo, lakini ukienda kila sehemu wanakwambia eneo lina mtu, hatujatenga maeneo maalum kwa ajili ya kuvutia uwekezaji na kwa ajili ya kujenga makazi ambayo yana mipango mizuri. Ili sasa tuweze kuzuia ujenzi holela na migogoro ya ardhi, lazima tujipange tuhakikishe tuna benki ya ardhi kote nchini ikiwemo Mkoa wa Kagera. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufanikiwa katika benki ya ardhi, naishauri Serikali tusiziachie tu Halmashauri zetu, iwe ni Sera ya Kitaifa ambayo inaratibiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Mikoa yetu na Halmashauri. Katika hili, ningetamani kuona Aprili mwakani tunapokuja Bungeni kama Mheshimiwa Waziri walivyofanya kazi nzuri ya kuorodhesha migogoro yote ya ardhi nchini, basi tuwe tuna mpango mkakati wa namna gani tutajipanga kuwa na benki ya ardhi kote nchini kwa kila Wilaya na Mkoa tuvione na kila Wizara isifanye kazi kwenye silos. Kama ni Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, vikae chini tuwe tuna-coherent plan kwa ajili ya land bank. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuchangia ni National Housing. Kwanza nawapongeza sana National Housing kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kwa kweli mkakati wao unaonesha kwamba hata Tanzania shirika letu hili linafanya kazi katika karne ya 21 kwa weledi mkubwa sana. Katika hili hazikosi changamoto, nionavyo National Housing imejikita vizuri sana katika kusaidia kujenga nyumba kwa ajili ya watu wenye kipato cha kati na cha juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili si jambo baya, lakini nipende kuipa changamoto National Housing pia waangalie ni namna gani kibiashara yaani rate of return iwepo, lakini tujikite kusaidia asilimia kubwa ya Watanzania ambao wako kwenye bottom ya population pyramid ili waweze kupata nyumba za bei nafuu. Katika hili lazima kuangalia watumishi na wafanyabiashara wadogo namna wanavyoweza ku-afford hizi nyumba za bei ya chini na zijengwe kote nchini ili kuondoa tatizo la ukosefu wa nyumba na ambazo ziko katika mipango miji mizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichangie katika suala la urasimishaji ardhi. MKURABITA imejitahidi lakini bado kuna changamoto kubwa kwani ukiangalia katika nchi nzima na kama hotuba ya Mheshimiwa Waziri inavyoonesha ni vijiji 11,778 tu ambavyo vimepata hati miliki. Tanzania sasa hivi tuna takribani watu milioni 50, hizi ni hati kidogo sana. Kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali tujikite kuhakikisha tunapima vijiji vingi kadri inavyowezekana kwani katika Serikali ya viwanda, wananchi wakishapata hizi hati wanaweza wakazitumia kama dhamana kukopa katika mabenki. Hivi tunavyojipanga kuanzisha benki mbalimbali kwa ajili ya kusaidia wananchi walio wengi ambao hawajiwezi basi kwa kuwa na hizi hati miliki tutakuwa tumewasaidia kupata dhamana ya kwenda kukopa kwenye mabenki ambayo yatakuwa na mikopo ya bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MKURABITA kwa ushauri wangu napendekeza iwe chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa sababu ya uratibu. MKURABITA kama ikipata fedha za kutosha, sababu moja ya changamoto kwa mfano ni kufidia wananchi. Kuna ule mpango wa Land Tenure Support Program, inasikitisha kwamba kama wafadhili hawatupi hela basi hela inakuwa haipo ya kuendesha huu mpango. Kwa hiyo, niiombe Serikali mipango kama hii ambayo inapelekea wananchi wengi wa Tanzania kupata hati miliki waweze kuzitumia kama dhamana, tutafute kila mbinu kuhakikisha inapata fedha za kutosha na ardhi nchini zinapimwa kadri inavyowezekana ili tuweze kuwa na matumizi bora ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi ni hayo tu lakini sina shaka mipango ya Wizara yetu hii ni mizuri na naamini kabisa kama watafuata ushauri, basi mpango kazi wa mwaka 2016/2017 ukitekelezwa tutasonga kwa kasi kutatua changamoto za ardhi nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.