Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Naungana na wenzangu kumpongeza Waziri wa Ardhi pamoja na Makamu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na wenzangu kuzungumzia nyumba za bei nafuu ambazo siyo nafuu. Nilimsikia Mheshimiwa Waziri mwenyewe wakati anazungumza katika vipindi mbalimbali akizungumzia bei ya nyumba zinazoitwa nyumba nafuu, lakini siyo bei nafuu. Mimi naona kwa kuwa, yeye ameligundua hilo naomba alisimamie! Haiwezekani nyumba ya vyumba viwili ikauzwa milioni 70 halafu unasema ni nyumba ya bei nafuu! Hilo naomba alisimamie ili wananchi wetu wenye kipato kidogo waweze kufaidika na nyumba hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia, nizungumzie mradi wa viwanja eneo la Mvuti katika Manispaa ya Ilala. Tulihamasishwa, kwanza napenda ku-declare interest kwamba, nilishakuwa Diwani wa Kata ya Msongola, lakini pia, nimekuwa Diwani wa Kata ya Chanika kwa miaka 10 mfululizo ambako katika Kata hizo pia, imeweza kutoka Kata ya Majohe, Kata ya Buyuni na Kata ya Zingiziwa, kwa hiyo, nina uzoefu karibu katika Kata tano katika Jimbo la Ukonga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Mvuti tulihamasisha wananchi na wananchi walikubali kuingia katika mradi wa upimaji viwanja katika Mitaa ya Kidole, Sangara, Mkera na Luhanga, lakini tangu mradi ule wananchi walivyokubali hakieleweki nini kinachoendelea kwa sababu, wamekatazwa kulima na hawajengi, lakini mradi hauendelei!
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa wengi wameanza kukata mazao yao ikiwepo michungwa na miembe wakichoma mkaa wakitegemea kwamba, nyumba wakati wowote zinakuja, ili nao waishi kimjinimjini, lakini hali inakwenda taratibu. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja niweze kujua mradi wa viwanja katika Kata ya Msongola katika maeneo hayo niliyoyataja umefikia wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, napenda kujua taarifa kuhusiana na nyumba za Buyuni katika mradi wa viwanja elfu 20 vya Buyuni. Katika eneo hilo imehusisha mitaa ya Kigezi, Mbondole, Zavala na Vikongolo, kuna nyumba zaidi ya 2000 hazijulikani mwenyewe ni nani! Wengine wanasema Shibat wengine wanasema za Mchina! Katika nyumba hizo wanaoishi pale ni karibu watu 20 tu maeneo yaliyobaki yamerudi tena kuwa pori! Sasa zile nyumba sasa hivi zimeshakuwa zina mgogoro kwa maana kwamba, zinawapa matatizo wananchi! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yale watu wanabakwa, maeneo yale wezi wanakwenda kujificha, lakini maeneo yale tena yameshakuwa, mtu huwezi kupita jioni kwa sababu, nyumba ziko nyingi wanaoishi ni wachache, mapori yamerudi tena na nyumba zile hazijulikani mwenyewe nani na kwa nini watu hawakai, lakini kwa uchunguzi wa haraka tumeambiwa kwamba, zile nyumba pamoja na kwamba, zimekamilika bei ni kubwa sana ndiyo maana wananchi hawakai! Sasa majengo yamejengwa yako tupu yanaendelea kuharibika! Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze nyumba zile ni za nani na kwa nini hawahamii mpaka sasa hivi wakati zimekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia suala la Kazimzumbwi. Kazimzumbwi inagusana na Mitaa ya Kigogo, Kimwani, Nyeburu, Nzasa na Ngobeje. Hapa naomba niongee kwa kina. Suala la mgogoro wa ardhi wa Msitu wa Kazimzumbwi na wananchi wa Kata ya Chanika haujaanza jana wala juzi, ni wa muda mrefu, lakini niseme wanasiasa tunazidisha sana mgogoro ule kuufanya usimalizike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshiriki vikao mbalimbali vya kutatua mgogoro ule, lakini utakuta wakati wa uchaguzi ukifika wagombea wa vyama mbalimbali wanaenda kuwashawishi wananchi msikubali, msifanye hivi. Kwa hiyo, kunakuwa na vurugu, zile Kamati hazifiki mwisho, uchaguzi ukiisha yanakwisha, uchaguzi ukikaribia vurugu zinaanza tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa sasa hivi uchaguzi umekwisha, hatuna uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hatuna uchaguzi wa Mbunge, aende kule akafanye kazi ili wale wananchi wawe na jibu la uhakika badala ya kuwa na majibu ya kisiasasiasa. Huyu anakuja asubuhi anasema nendeni, huyu anakuja anasema toeni. Naomba kwa kipindi hiki akafanye kazi tuje na jibu kuhusiana na Msitu wa Kazimzumbwi na wananchi wa Kata ya Chanika na mitaa husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie tena suala la mashamba pori. Mara nyingi limekuwa linazungumziwa kwamba mashamba pori yachukuliwe lakini bado haujatolewa mwongozo wananchi wanayachukua kwa utaratibu gani? Kuna wananchi wakishasikia huku Bungeni mmesema mashamba pori marufuku, wanavamia mashamba, wanakamatwa, wengine wanapigwa na wengine wanapelekwa mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba wanapotoa mwongozo kwamba yale mashamba makubwa yachukuliwe, watoe na ufafanuzi wanachukua kwa utaratibu gani ili wananchi wasipate matatizo. Wakati huohuo kuna mashamba makubwa ambapo wamiliki wana hati zao na wameyanunua kwa ajili ya kujenga shule, zahanati au hosteli kwa siku zijazo. Kwa hiyo, ni vizuri basi masuala haya yawe yanatolewa ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kumaliza kuongea kabla sijazungumzia viwanja vya CCM. Kuna watu hapa wakikaa wanazungumzia CCM ina viwanja, ni vyetu. Utaratibu wa Chama cha Mapinduzi huwezi kujenga tawi kama huna kiwanja ambacho ni halali. Kwa hiyo, kila tawi lazima lihakikishe uhalali wa kiwanja chake ndipo linaitwa tawi Ukiona tawi ina maana lina wanachama si chini ya 50. Unapoona Tawi la Mjumbe wa Shina ina maana si chini ya wanachama 10.
Sasa mtu anakuja anakaa mwenyewe anazunguka tu viwanja vyote vya CCM, viwanja vyote ni vya CCM, ni vya kwetu, ni vya halali yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, wale wote kupitia Chama cha Mapinduzi watakaoleta maombi ya kupata hati ya viwanja vyao alifanyie kazi ili Chama cha Mapinduzi viwanja vyake viweze kuwa na hati.
Maana kuna watu wana uchu yaani mtu anasimamisha bendera moja….
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na uendelea kunilindia muda wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ni kwamba mara zote anayeanza kusema anaonekana mwema wa mwisho anamalizia. Nasema viwanja vya Chama cha Mapinduzi visiwatie presha ni vyetu! Kama mnataka viwanja vingi njooni ndani ya Chama cha Mapinduzi mtapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tena bahati nzuri au bahati mbaya ndani ya Chama cha Mapinduzi ukiona Mjumbe wa Shina kaweka bendera moja ina maana ana watu 10, ukiona tawi lina bendera moja lina watu zaidi ya 50, tofauti na vyama vingine yaani mtu mmoja anapata uongozi bendera 200 zinamwagwa.
Naomba muelewe kwamba Chama cha Mapinduzi viwanja vyake ni vya halali hatujaiba. Kama kuna mtu ana uhakika tumeiba aende mahakamani, tutapambana naye. Namwomba kwa mara nyingne Mheshimiwa Lukuvi, maombi yote ya Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya hati za viwanja vya Chama cha Mapinduzi ayasimamie kama kawaida kwa sababu wale maombi yao ni halali siyo kwa wizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja kwa sababu wale Mawaziri ambao wako kwenye Wizara hii wanajiamini wanaweza kufanya kazi na wana uwezo wa kutoa maamuzi, siyo watu wa kuyumbayumba. Akisema bomoa, bomoa, jenga, jenga na huo ndiyo msimamo wa kiongozi, lazima uwe unaeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja.