Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema sisi sote tulioko hapa na kuendelea kutupa pumzi ya uhai pamoja na kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Monduli walioniamini kwa kunipa kura za kutosha kuingia katika Bunge hili kwa ajili ya kutetea masilahi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa maelezo yaliyoko kwenye kitabu chake. Haya ni maelezo ambayo na ninyi mtakuja kukumbuka kwamba mmesaliti nafsi zenu kwa taarifa hizi ambazo mmeziandaa. Historia ya dunia inaonesha kwamba katika vita ambavyo ni vikubwa siku zote, ni vita vya ardhi; na katika maeneo ambayo kwenye nchi yetu tumekosea ni katika ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanikiwa kudhibiti kabisa suala la ukabila na masuala mengine ambayo yangeweza kuleta mgongano katika Taifa letu, lakini katika vita ambavyo vitakuwa vikubwa kwenye nchi yetu ni suala hili la ardhi kama Serikali haitachukua hatua sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia taarifa ya Wizara, hakuna mahusiano kati ya Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili na Wizara ya Mifugo na Kilimo. Nataka tu nitoe tahadhari kwa Waziri pia wa Maliasili kwamba asitutafute ugomvi wa wafugaji. Kauli ambazo zimeendelea kutolewa kuonesha kwamba kila siku wafugaji ni wavamizi wa ardhi ambayo mmetukuta na wanyama hatutaweza kukubali leo wala kesho. Kama tukishindikana kwenye Bunge, tutarudi kwa wananchi wetu na hatuko tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wetu wamechomewa maboma Ngorongoro na maeneo mengine kwa sababu ya tatizo la ardhi. Ni wajibu wa Serikali kutatua matatizo yaliyopo badala ya kwenda kuwaumiza wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaleta taarifa halafu hupewi bajeti. Tuna vijiji 12,000 zaidi nchi nzima, lakini mna mpango wa kupima vijiji 200 katika mipango ya matumizi bora ya ardhi. Tunapeleka wapi Taifa? Tunayo Ripoti ya Tokomeza iliyoletwa kwenye Bunge lililopita, sisi hatukuwepo, inayoonyesha namna gani ambavyo wananchi wamedhulumiwa na kupewa majanga makubwa kwa sababu ya maliasili na Mheshimiwa Waziri anadiriki kusema eti ile ripoti ilikuwa ya uongo. Halafu tunanyamaza, tunasema bajeti ipite. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge tusikubali bajeti hii ipite mpaka Waziri atuambie anahitaji bajeti kiasi gani kwa jili ya kutatua migogoro yote ya ardhi iliyoko kwenye nchi yetu. Hii ndiyo Wizara ambayo tukifanikiwa kuiweka vizuri, nchi yetu itakuwa na utulivu mkubwa sana, hii ndiyo Wizara ambayo tukifanikiwa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, nchi yetu itakuwa na amani muda mrefu, hii ndiyo Wizara ambayo tukifanikiwa kuidhibiti vizuri, nchi yetu itakuwa na amani katika suala la wanyamapori na wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kila mtu afaidi katika Taifa hili, ni lazima kila mtu awe na haki ya kutumia ardhi kwa sababu hakuna maeneo mengine tunaweza kuwekeza bila kutumia ardhi. Mheshimiwa Waziri anatuletea shilingi bilioni 20 sijui, eti kwenye Wizara ambayo ni sensitive ambayo sisi wote ni watumiaji wa Wizara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuja pamoja na hili suala la Mheshimiwa Rais kuhusu watu kuogopa, atuambie anahitaji bajeti ya kiasi gani ili atatue migogoro yote ya ardhi iliyoko nchini kati ya wakulima na wafugaji; kati ya wanyamapori na wananchi; ili matatizo haya yafike mwisho, pamoja na bomoa bomoa ambayo inaendelea kwenye nchi nzima. Kama bajeti ya Wizara haioneshi future ya matatizo hayo kwa nchi yetu, tunaelekea wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri anisaidie mambo matatu; kwanza atuambie, kwa nini benki za Tanzania hazithamini hati miliki za kimila katika mikopo kwa wananchi wetu na ni hati za Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine namuomba Mheshimiwa Waziri anisaidie kuniletea Kamishna wa Ardhi Monduli, kwa sababu kuna mashamba matatu ambao wengine walikuwa ni wamiliki wa nje na wameshafukuzwa tangu mwaka 1980 lakini maeneo yale ameendelea kuhodhi, yamekuwa mapori karibu eka 9000 na sisi hatuko tayari kuendelea kuiacha hiyo ardhi, tutaichukua asubuhi kama Serikali haitatumia utaratibu wa kumnyang’anya mtu huyo shamba hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeahidi hatuko tayari tena kupoteza ardhi ya Monduli kwa sababu maeneo mengi ya Monduli ni ya wanyamapori na maeneo mengine ni ya Jeshi na Monduli ni sehemu ya pekee ya nchi hii ambayo hatuna mgogoro kabisa na Jeshi pamoja na kwamba wamechukua eneo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo dogo tulilobakiza walichukua wahujumu uchumi miaka 1980 na 1988 wakati wa mgogoro wa mama mmoja kule Namanga akapewa Lolkisale akaambiwa ni eneo la bure, wakachukua Mkuu wa Jeshi wa wakati ule, wakachukua akina Kinana na watu wengine, wanagawana kama ardhi haina wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenyewe tumekuja. Tunao vijana wasomi, tutatetea ardhi kwetu kwa kila namna na hatutaitoa ardhi hiyo. Wako watu wanaotaka kudhulumu ardhi yetu lakini hatuko tayari kwa sasa. Mwisho, haiwezekani, Mheshimiwa Waziri nimeona migogoro michache, mengine tuachie. Mengine tutamaliza wenyewe, tuachie, lakini tusaidie mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, mgogoro wetu na Babati ambapo DC wa Babati amekuwa akiingilia kila siku maeneo ya Monduli bila kumshirikisha DC wa Monduli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka niombe mambo machache. Moja, nimesema lile suala la uhusiano wa Wizara zile na lingine kuna tatizo la Sheria za Ardhi, ambapo tatizo hili ni kwamba wanawapa Wenyeviti mamlaka ya vijiji kugawa ardhi, lakini hakuna sheria inayochukuliwa kwa Wenyeviti wale wanavyogawa ardhi ya wananchi kienyeji.
Mheshimiwa Mwenyekii, Wenyeviti wengi wametumia nafasi hiyo kudhulumu ardhi na kwa sababu hakuna sheria ya direct inayochukuliwa zaidi ya kuwavua madaraka na ardhi imeshakuwa na migogoro mikubwa katika maeneo mengi.
Pili, naomba Wizara ishirikiane na NDC kule Engaruka kwenye eneo la Magadi. Wanatuambia wanataka ardhi square kilometer 79,000 karibu eka 100,000; ardhi hiyo hatuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tutatoa eneo la kiwanda tu, maeneo mengine ya Mipango Miji watuachie sisi tutawauzia NDC, lakini hatutatoa bure. Maeneo mengine naomba Mheshimiwa Waziri Wizara yako ishiriki, ije watuambie wanataka ardhi kiasi gani kwa ajili ya kujenga kiwanda. Maeneo mengine watuachie ardhi yetu, sisi tutapanga namna ya kutumia, wao wasitupangie. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, suala lingine ambalo natamani lishughulikiwe, Mheshimiwa Waziri naomba usikilize vizuri, liko tatizo la shamba ambalo tuliruhusiwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2005 kule Makuyuni. Shamba kitalu namba 7/2, Mheshimiwa Rais alipofuta shamba hili kwa mtu anayeitwa Stein ambaye alifukuzwa nchini mwaka 1980 tukapewa ardhi hiyo eka 9000 Makuyuni. Baadaye Hazina wakatuandikia barua kwamba tumwandalie hati. Hatuandai hati leo, wala kesho, wala milele, wala asiendelee kutusumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amesharudisha ardhi hiyo, hatuitoi, hatuitoi, hatuitoi! Tumeambiwa tuwatoe wananchi wetu kule eneo la Jeshi tukawape eneo lile, halafu leo tunaambiwa tumrudishie mtu ambaye sio raia! Hiyo ardhi hatuitoi leo wala kesho. Wala wasithubutu, wala wasijaribu maana hatuitoi. Tumegawana eneo hilo, tunasubiri mvua iishe tukaingie kwa sababu tulishamaliza. Hamuwezi kutuondoa kwenye eneo la Jeshi halafu tupewe ardhi na Mheshimiwa Rais halafu mtu mwingine aje kuturudisha. Mheshimiwa Rais mwenyewe atamke. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kwenye uongozi wetu, hiyo ardhi hatuitoi. Watu wa Hazina kuendelea kutuandikia vi-memo wakome. Sisi huwa hatupigwi, wala hatujinyongi, lakini tunaitetea ardhi yetu kwa namna ambayo tunaweza tukiwa hai. Hatuitoi hiyo ardhi. Hatuitoi, Monduli siyo shamba la bibi!