Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi na mimi niweze kuchangia machache katika Wizara hii ya Ardhi. Nakuhakikishia tu, hata hawa wageni wangu 16 uliowataja hapo, wafanyabiashara wa furniture kutoka Keko wamekuja maalum kwa ajili ya kikao na Mheshimiwa Waziri, pamoja na viongozi wa Shirika la Nyumba kwa ajili ya kuzungumzia changamoto zetu zinazohusiana na masuala ya ardhi pale Temeke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na heshima yote hasa ya ushirikiano ambayo Mheshimiwa Waziri amekuwa akinipatia, bado niseme kwamba Mheshimiwa Waziri anahitaji kuwaaangalia kwa makini sana watendaji wake katika Wizara hii. Bado kuna watendaji wengi ambao wanaonyesha kutokuwa na dhamira nzuri na wanaamini kwamba ukiwa mtumishi kwenye Wizara ya Ardhi, basi umepata goli la kutokea au umepata sehemu ya kutajirikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kurasini ardhi yake sasa hivi inasimamiwa na Wizara ya Ardhi, siyo Halmashauri tena, kwa sababu kuna mpango maalum wa kulifanya eneo lile liwe mbadala au lisaidie shughuli za bandari pale, lakini pia kuna ule uwekezaji mkubwa wa EPZ. Kwa hiyo, maamuzi mengi pale tunategemea yafanyike kutoka Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko Wizarani sasa baadhi ya watumishi wasiokuwa na nia njema wamegeuka kuwa madalali wa eneo hilo. Nitatoa mifano michache tu. Eneo la Mabwawani; hili linaitwa Mabwawani kwa sababu DAWASCO ndiyo wanatupa majitaka katika eneo hilo, wanamwaga pale. Kwa hiyo, miaka ya 1980 kwanza ilikuwa ni sahihi kwa sababu hiyo sehemu ilikuwa bado haijachangamka, haukuwa mji, lakini kwa sasa pale ni mji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa DAWASCO, miundombinu yao yenyewe ya kuchakata zile taka imekufa. Kwa hiyo, kinamwagwa kinyesi kibichi pale na hilo eneo limezungukwa na makazi ya watu; watu wanakaa pale. Kwa hiyo, ikinyesha mvua, yale mabwawa yanatapika, ule uchafu wote unaingia kwenye makazi ya watu. Wananchi wa pale kwa kutambua ile kero, wakamtafuta mtu, bwana, njoo tununue hapa sisi tuondoke; tulipe gharama yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yule mtu alikuwa tayari kuwalipa ili wale wananchi waondoke. Alipokuja akaamua afuate utaratibu kuja Halmashauri kwamba pale nataka niwanunue. Halmashauri wakamwambia kwamba hilo eneo linasimamiwa na Wizara. Kwa hiyo, hebu nenda Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akaandika barua akapeleka Wizarani. Wizara wakamwambia, basi ngoja tuje tufanye uthamini hapo, lakini kwa sasa hatuna fedha ya kuwaleta wathamini kuja kufanya uthamini hapo. Kwa sababu wewe ndio unataka kununua, tupatie shilingi milioni 25 tufanye uthamini. Yule bwana akalipa ile shilingi milioni 25 kwenye akaunti ya Hazina, hela imeingia Wakafanya uthamini ili awalipe wananchi waondoke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya fedha ile kulipwa, Wizara inamwambia yule mtu, kwamba tutafanya uthamini wenyewe, kwa hiyo, hela yako tutakurudishia, ambapo mpaka leo haijarudi na ni miaka miwili imepita. Nilikuja ofisini, Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu, akamwita Kaimu Mthamini, anaitwa Evelyne yule mama, akaja pale, akasema, aah hii pesa tunairudisha. Mpaka leo nakuhakikishia hiyo hela haijarudi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi siyo suala la kurudisha pesa, ni kwamba wale wananchi wanataabika na wanahitaji mwekezaji awalipe, waondoke pale. Wizara sasa inasema kwamba lile eneo maana lile eneo limegawa kuna upande wa eka nane na upande eka nne. Wanasema zile eka nne kwa sababu zina mabwawa ya DAWASCO, tumempa DAWASCO ndio atawalipa fidia. DAWASCO amekaa hapo miaka yote, ameshindwa kuwalipa fidia, leo unampa hilo jukumu DAWASCO eti awalipe fidia, DAWASCO wameiweka wapi hiyo hela? Mfuko gani wa DAWASCO una hela ya kumlipa mtu fidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni haraka kwa sababu wale wananchi pale wapo kwenye mazingira magumu. Tunahitaji mtu aje awalipe, waondoke wakatafute maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tu kwa akili ya kawaida, tunasema hapa tuna mradi mkubwa wa EPZ, hapo unampa DAWASCO aendelee kuboresha eti amwage taka; au ndiyo mnatuchulie poa watu wa Temeke; hapa nyumba, hapa choo? Hiyo moja. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri sasa ikawaandikia barua Wizara, njooni mfanye uthamini basi haya maeneo, wananchi wajue tu kwamba hapa hivi tunalipwaje? Barua ikaenda Wizarani, ikakaa kweli kweli! Mpaka mimi nimekuja tena Wizarani, Mthamini akasema aah, nawajibu. Akajibu kwamba Halmashauri ifanye uthamini wenyewe, sisi hatuna wathamini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dana dana zinaendelea ili mradi tu hilo jambo lisifike mwisho. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nataka upate hiyo picha na ujue kwamba pale kuna matatizo na tuna kazi kubwa ya kufanya. Kwa hiyo, sitachoka kuja ofisini kwako tuhakikishe hizo kero tumezimaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Mheshimiwa Waziri iliwahi kutoa barua ya kuwataka Halmashauri wakavunje pale; kuna lile jengo linaitwa Monalisa, lile godauni pale Toroli; yule Oil Com kiwanja chake kamaliza, akaingia tena barabarani, kajenga fence kwa pembeni na kwa nyuma kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, amezuia njia sasa za gari. Kwa kule nyuma watu wanalazimika kuhama nyumba zao kwa sababu vyoo vimejaa lakini huwezi kupeleka gari ya kunyonya taka, anayeitwa mwekezaji kazuia njia. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, hata ghorofa ulilolivunja ni kwasababu uliamua livunjwe. Ukimpelekea barua Halmashauri ndiyo akavunje, hilo haliwezi kutekelezeka, kwa sababu inawezekana kabisa kwenye ule ujenzi huyo Halmashauri ndio ana mkono wake. Kwa hiyo, kwenye hizi kero ambazo zinawagusa wananchi moja kwa moja, nakuomba Mheshimiwa Waziri husichoke. Uingie kwa miguu yote miwili, twende tukaokoe hawa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni tatizo la mpaka kati ya Temeke na Ukonga kule, limekuwa ni la muda mrefu sana na limesemewa hapa kwa muda mrefu. Halmashauri ya Jiji pia walilishughulikia na sasa hivi lipo Wizarani kwako.
Tunawaomba mje tumalize ule utata pale. Msitake kunigombanisha na Mheshimiwa Waitara, sisi wote team UKAWA. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mje mtusaidie, mpaka wetu pale ujulikane sasa, ili tatizo lifike mwisho. Hatuna ugomvi, mkija tu, tutayamaliza kwa sababu mimi na Mheshimiwa Waitara wote ni ndugu moja. Kura zake zikija kwangu siyo tatizo na zangu zikienda kwake, wala halina utata. Yawekezana zamani ilikuwa tatizo sana kwa sababu ya watu kutetea kura zao zisihame. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri uje tuweze kulifanyia kazi jambo hili kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, issue za Kurasini nahitaji Mheshimiwa Waziri uje hasa uzione. Issue ni nyingi, watu wanadhulumiwa, watu wanaishi kwenye maisha ya taabu! Eneo moja pale lilikuwa na soko, pembeni huku kote watu wameshaondoka, ni fence tu sasa hivi hapa watu wanasubiri uwekezaji. Sokoni pale hakuna biashara inayofanyika na watu ndio wanaendesha maisha yao pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na hili nimelisema hapa mara kadhaa, suala la watu waliokuwa pembeni ya reli ya TAZARA. Wizara yako imesema kabisa zile mita 60 pale wahame...
MWENYEKITI: Ahsante.