Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nakushukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia leo tarehe 21 Mei kwenye hotuba ya Wizara ya Ardhi, inayoongozwa na Mheshimiwa William Lukuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze moja kwa moja na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 143. Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake anaonyesha kwamba maeneo ya ardhi yaliyonunuliwa na Shirika la Nyumba la Taifa hadi Aprili, 2016 katika Wilaya mbalimbali nchini, Jimbo langu linajitokeza katika Wilaya ya Masasi ambapo Shirika la Nyumba limejenga nyumba chache pale na inaonekana eneo hili ni la ekari 16 na kwamba walilinunua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho, aweke sawa taarifa hizi, kama kulipa fidia ya shilingi milioni 22 katika eneo la ekari 16 ndio kununua eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, naomba pia Mheshimiwa Waziri atakapokuja kufanya majumuisho yake, atuambie ni vigezo gani Shirika la Nyumba wanavitumia katika kulipa fidia ya eneo lililopo katika mji kwa shilingi 22,500,000 kwa eneo la ekari 16 za wananchi ambao wamehamishwa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge lililopita, Mheshimiwa Waziri alituelekeza tuorodheshe migogoro iliyopo katika maeneo yetu. Mimi binafsi niliunda kikosi kazi na tukaorodhesha migogoro mbalimbali iliyopo katika maeneo ya Mji wa Masasi wakati wananchi wa eneo la Kata ya Mtandi, Migongo, Napupa, Mkomaindo, Jida, Mkuti na Mwenge Mtapika, wamekuja wakaleta malalamiko yao mengi, tukapata orodha ya wananchi takribani 1,123. Kwa pamoja wananchi hawa wanadai fidia ya zaidi ya shilingi milioni 800.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha migogoro, jambo hili halipo. Sasa naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni mgogoro mkubwa kwa kiwango gani unatakiwa uoneshwe kwamba ni mgogoro ambao umedumu kwa takribani miaka kumi kwa sasa, wananchi hawa wanaendelea kuhangaika, wamehamishwa kwenye maeneo yao na hawajapewa fidia?
Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa sababu ametupa documents za kusoma, nataka pia tujaribu kuangalia hizo sheria ambazo zinawaruhusu watumishi wa Idara ya Ardhi kupima maeneo ya wananchi, kuwahamisha maeneo hayo, kuyauza kwa watu wengine na kujenga nyumba zao, halafu wananchi hawa wanaendelea kuidai Serikali fidia. Hizi ni sheria za kutoka wapi? Tunaomba pia Mheshimiwa Waziri aweze kutupatia ufafanuzi wa jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Mheshimiwa Waziri wananchi wa Masasi wanakusubiri. Sisi Wabunge tunapofikia hatua ya kuleta migogoro kwako, maana yake migogoro hii imekuwa ni sugu na viongozi waliopo katika Halmashauri zetu wameshindwa kuishughulikia, ndiyo maana yake! Kwa sababu hatuwezi kuwa na migogoro miaka kumi, kila siku tunazungumza haya haya, mpaka leo hayajapatiwa ufumbuzi.
Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kufanya hitimisho, utuambie utakuja Masasi lini ukae na wananchi wa hizi Kata nilizozizungumza hapa waweze kulipwa mahitaji yao? Hali yao siyo nzuri na wanasubiri kauli yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Masasi limepitiwa na barabara ya kutoka Masasi kuelekea Nachingwea. Pambezoni mwa barabara hii ambayo kwa sasa inasubiri upanuzi, wapo wananchi ambao tayari wameshafanyiwa tathmini ya eneo hili. Kwa maana hiyo, wanatakiwa kupisha upanuzi wa barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini hii imefanywa muda mrefu na sasa ni miaka mingi imepita, wananchi hawa wameambiwa watalipwa fidia zao ili watafute maeneo mengine ya kukaa, lakini mpaka sasa hivi wananchi hawa wapo stranded hawajui wafanye nini kwa sababu hawajalipwa fidia zao. Mheshimiwa Waziri kwa sababu eneo la fidia linakuhusu wewe, naomba utoe ufafanuzi, ni lini Serikali itawalipa fidia zao wananchi hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, nilipokuwa napitia makabrasha ya Wizara ya Ardhi, sijaona mipango ya upimaji wa miji hususan Mji wa wa Masasi. Naamini kwamba harakati za upimaji wa mji na kuyarasimisha makazi ni jambo muhimu sana kwa sababu kadri tunavyozidi kusonga mbele ndivyo wananchi wetu wanavyozidi kujenga kwenye makazi holela na kwa maana hiyo, hatua zetu za upangaji wa miji zinazidi kuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atoe pia ufafanuzi, mpango huu hasa ukoje? Ni maeneo yapi na ni lini Mji wa Masasi nao utaingia katika mpango huu wa upimaji ili kusudi wananchi wakae katika maeneo yaliyorasimishwa waweze kupata umiliki wa maeneo yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema maneno haya machache, namuomba Waziri akija hapa atoe ufafanuzi wa maeneo hayo niliyoyaeleza na mimi naunga mkono hoja. Ahsante sana.