Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Mbarouk Salim Ali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Naibu Spika, sheria za udhibiti katika tasnia ya uchimbaji madini. Mwezi Julai, 2015, Bunge hili lilipitisha kibabe Miswada mitatu ya sheria za udhibiti katika tasnia ya uchimbaji. Miswada hiyo ilikuwa ni ya Sheria ya Petroli, Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi ya mwaka 2015 na Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika tasnia ya uchimbaji Tanzania ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote wa upinzani hatukuunga mkono namna Miswada hiyo ilivyoletwa Bungeni na namna ambavyo mijadala ya Miswada hiyo ilivyokuwa ikiendeshwa. Kwanza, Miswada yote mitatu ililetwa kwa hati ya dharura na pili mijadala yake iliendeshwa kwa pamoja na uamuzi wake ulifanyika kwa pamoja kinyume kabisa na kanuni na taratibu za kibunge za utungaji wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja za Wabunge wa Upinzani kwa wakati huo na mpaka sasa ni kwamba kulikuwa na uharaka gani wa kuleta Miswada hiyo katika hati ya dharura na kuendesha mjadala wa Miswada hiyo haraka bila Wabunge kupata nafasi ya kutosha ya kupitia na kuelewa maudhui ya vifungu vya Miswada hiyo? Ni nini kilikuwa kinafichwa katika Miswada hiyo hadi kufanya mambo haraka haraka namna hiyo?
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi na Wabunge wote wa Upinzani hatukuridhishwa na namna Miswada hiyo ilivyopitishwa. Hii ni kwa sababu sheria nzuri inapatikana ikiwa kuna maridhiano miongoni mwa Wabunge katika kupitisha Miswada mbalimbali ya sheria. Kwa maoni yangu, kitendo cha Serikali kutumia jeuri ya wingi wa Wabunge wa CCM kupitisha sheria mbovu kwanza ni kuudhalilisha mhimili wa Bunge lakini pia kunaiondolea Serikali sifa ya utawala bora kwa maana ya utawala wa sheria kwa kuwa sheria hizo zinakuwa mbovu na au za kulinda maslahi ya mafisadi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali ilivyokuwa wakati ule presha ilikuwa kubwa sana kwa sababu Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa inamaliza muda wake na inasemekana kuwa ilikuwa imeshaingia mikataba na makampuni makubwa ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta na kwa hiyo ilitaka kutunga sheria haraka haraka ya kuwalinda kabla haijaondoka madarakani ili isije ikaingia Serikali nyingine halafu ikatengua mikataba hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hofu kubwa ilikuwa ni uwezekano wa chama cha upinzani kushinda uchaguzi mkuu wa 2015 na kufuta mikataba yote ya kinyonyaji ambayo Serikali ya CCM iliingia na makampuni makubwa ya utafutaji na uchimbaji wa gesi na mafuta. Kwa kuwa Rais John Pombe Magufuli ameonekana dhahiri kuwa hapendi ufisadi wala mikataba ya kinyonyaji inayolikosesha Taifa letu mapato, atumie madaraka yake na kuagiza iletwe Miswada mingine ya sheria ya kuifuta ile iliyopitishwa kibabe ili Waheshimiwa Wabunge wapate nafasi ya kuipitia na kuiridhia kwa maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya umeme na gesi. Baada ya ugunduzi wa gesi katika nchi yetu, wananchi walitegemea kuwa bei ya umeme na gesi kwa matumizi ya majumbani ingeshuka kwa kiasi kikubwa ambapo wananchi wengi wenye kipato cha chini wangeweza kumudu gharama ili waweze kunufaika na huduma hiyo. Bei ya mtungi wa gesi wa kilogramu 15 ni Sh. 45,000/=. Bei hii ni kubwa kwa wananchi wa kipato cha chini kiasi kwamba hawawezi kununua gesi kwa matumizi ya nyumbani na kwa maana hiyo wanaendelea kumaliza misitu yetu kwa ajili ya kutafuta nishati ya kuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ipunguze bei ya gesi hadi kufikia angalau Sh. 20,000 kwa mtungi wa gesi wa kilogramu 15 ili wananchi wa kipato cha chini waweze kununua. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumewavutia wananchi wengi kutumia nishati mbadala na hivyo kuhifadhi misitu yetu ambayo ina maana kubwa sana katika utunzaji wa mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika kwenye umeme. Ikiwa gesi yetu inazalisha umeme, Serikali iiagize TANESCO unit moja ya umeme iuzwe Sh.50 ili Watanzania wanufaike na hii rasilimali ya gesi asili iliyogunduliwa katika nchi yetu.