Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii, kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhuhana Wataallah aliyenijalia uzima na afya njema hadi nikichangia mapendekezo ya mpango mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti nami nisiwe mwizi wa fadhila, niwapongeze kwa dhati kabisa wananchi wa Jimbo la Mtambile kwa kunichagua kwa kura nyingi kwa kipindi cha Nne mfululizo, toka mwaka wa 2000. Miongoni mwa Wabunge senior mimi ni senior, nikimuona Mheshimiwa Bahati Ali Abeid pale na Mheshimiwa Faida Bakar kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze moja kwa moja kwenye ukurasa wa 34 kwenye Mpango huu ambao unashughulikia zaidi kuhusu utawala bora na naomba ninukuu kwenye (vi), inasema, kuimarisha mfumo kujitathmini kiutawala bora (APRM) yaani African Peer Review Mechanism. Utawala bora ni jambo pana, jambo kubwa. Hakuna utawala bora kama Katiba inavunjwa katika nchi hii, hakuna utawala bora kama sheria hazifuatwi katika nchi hii, hakuna utawala bora kama haki za binadamu hazilindwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yanayotokea Zanzibar ni kitu gani, ni utawala bora au bora utawala! Inasikitisha! Inaumiza! Inasononesha sana. Leo hii tunaimba kila wakati tukisema kwamba tunataka amani na utulivu, lakini amani na utulivu wa midomoni. Inakuwaje leo kuna watu wanatembea kwa magari wakiwa na silaha za moto, tena wakiwa wamebeba misumeno, wanapita wanapiga watu, wanavunja vibanda, na Polisi wapo. Hee! jamani. (Makofi)
Mwaka jana tulipitisha Sheria hapa ya The Firearms and Ammunition, nani wamiliki wa silaha. Leo niulize jamani, inakuaje watu wanaachwa, wanapita wamevaa ma-socks maninja, kama Janjaweed, wakiwa na silaha za moto, wanakatakata vibanda vya watu, wanapiga watu, na Jamhuri ya Muungano ipo! Tabia hii mbaya lini mtaacha Serikali, hawa si watu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Ulinzi na Usalama kwa kipindi kirefu, kwa muda wa miaka 10 sasa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama. Naombeni sana Polisi mnisikilize kwa makini na naombeni sana Idara ya Usalama wa Taifa mnisikilize kwa makini sana. Usalama wa nchi hii ni wetu sote! Haiwezekani, haiingii akilini kwamba upande mmoja wa Muungano mmeuacha watu wanafanya watakavyo. Hii ni aibu, ni tabia mbaya. Ni aibu kwa Taifa hili, ndani ya nchi na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili halikubaliki! Hili halikubaliki! Ni aibu. Nadhani kama tatizo ni uchaguzi, uchaguzi halali wa huru na haki ulioangaliwa na Mataifa mbalimbali, uliokubalika na Mataifa mbalimbali, ulikuwa tarehe 25, Oktoba. Umeshapita, Rais halali wa Zanzibar ambaye kwamba hatua zote za uchaguzi kuanzia kupiga kura, kuhesabu kura, matokeo yalibandikwa katika mabanda yote na Mawakala wakapewa matokeo na mshindi alikuwa ni Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alipata kura 207,847 sawa na asilimia 52.84. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Taarifa !....
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuendelea. Kwamba matokeo yote katika hatua zote za uchaguzi kuanzia kupiga kura, kuhesabu kura na baadaye majumuisho katika maeneo mbalimbali, Majimbo yote yalibandikwa kwenye kuta. Matokeo ya Rais wa Zanzibar yote yamewekwa kwenye kuta, Mawakala wote walipewa ushahidi kamili, wapo. Wawakilishi wote walipewa vyeti vyao 27. (Makofi)
MWENYEKITI: Naomba urudi kwenye hoja iliyo mezani.
MHE. MASOUD ABDALLAH. SALIM: Utawala bora, Wawakilishi wa CUF 27.
MWENYEKITI: Suala la Zanzibar naomba lisizungumzwe kwenye ajenda hiyo kwa sababu halihusiani na Bunge la Jamhuri ya Muungano. Naomba tuheshimiane na tuheshimu Kiti, Mheshimiwa kama una hoja ya kuchangia katika maeneo mengine suala hili limo ndani ya mikono ya Serikali, tunaomba uheshimu vinginevyo kama hujasikia itabidi nichukue hatua ya kukutoa nje tafadhalli sana.
(Hapa Wabunge fulani walipiga kelele)
MWENYEKITI: Endelea na hoja nyinginem, kama ni hiyo naomba ukae.
MHE. MASOUD ABDALLAH. SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee niko katika APRM (Africa Peer Review Mechanism) Mpango wa kujitathmini wenyewe kwenye utawala bora suala la Katiba, suala la Sheria lazima hapa lizungumzwe. Kwa hiyo ,Wawakilishi ishirini na sita walipewa vyeti vyao kama ilivyo kawaida. Naomba niendelee. (Makofi)
MWENYEKITI: Naomba nimruhusu Mwanasheria Mkuu...
MWENYEKITI: Haya endelea
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Muda wangu ulindwe, niko makini, naendelea kusimamia hoja yangu kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachowaonesha Watanzania, ninachowaeleza tena kwenye Bunge hili ni jinsi gani ya uonevu ukandamizaji wa demokrasia, tusiwe na malumbano tusiwe na jazba, naomba niseme kwamba, wakati huo Mwenyekiti wa Wilaya ya Chakechake ambaye ni Mbunge wa Chonga, Mohamed Juma Khatibu Mwachawa, masaa mawili kabla ya kufutwa kwa shughuli ile pale waliitwa Makao Makuu ya Polisi na wakaambiwa hivi, naomba mtulie, wafuasi wenu muwatulize kwa lolote litakalotokea! Sasa hoja kwa nini tusiseme kwamba kuna mkono ambao ulilazimisha! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee nije kwenye mambo ya usafiri wa baharini.
MWENYEKITI: Endelea naomba utulivu tafadhali Bungeni.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza mambo mengi katika hali ya kuwanusuru wananchi, sioni Mpango wa aina yeyote! Sioni mpango wa aina yeyote wa kununua meli kutoka Tanga kuja Pemba. Sasa Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mpango huu uko wapi? Mpango wa kunusuru maisha ya watu, sioni Mpango wowote katika kitabu chako wa kununua meli kutoka Dara es salaam kuelekea Mtwara, meli za uhakika! Sioni mpango wowote ambao utanunua boti za kisasa katika Bahari ya Hindi na kwenye maziwa, pale inapotokea ajali, watu kila siku wanakufa! Mpango uko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo ambalo halikubaliki. Ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa na lazima lifanyiwe kazi, lakini kubwa kuliko yote Rais aliyepita alisema wizi, ubadhirifu na ufisadi hautavumiliwa. Marehemu Dokta Abdallah Omari Kigoda, Mungu amlaze mahali pema peponi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Kigoda alisema kwamba, umaskini uliopo katika Mikoa ya Kusini kwa mujibu wa Viwanda vile vya Korosho, viwanda ambavyo vimebinafsishwa basi vitafanyiwa kazi, alituahidi kwamba, wale wote waliopewa viwanda na hawakuviendeleza atawaita, lakini sasa hadi leo hakuna aliyeitwa na kubwa zaidi tulikuwa tunauliza viwanda vile mmiliki wake ni nani?
(Hapa Kengele Ililia)
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni kengele ya kwanza tulia! Viwanda vile wamiliki wake ni nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe viwanda vile imebainika na imedhihirika kwamba viwanda vile vimebinafsishwa Tanzania ilikopa dola milioni ishirini kwenye miaka ya 1970 na 1980 kutoka Japani vikajengwa viwanda vya korosho kule Lindi na Mtwara badaye wamekwenda kupeana vigogo wa Serikali kama njugu, wakapeana tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Dkt. Mpango na Msaidizi wako mniambie viwanda ambavyo hasa nataka kuvitaja ni nani waliomilikishwa? Kwanza naomba uniambie Mtwara Mjini, ambacho kinaitwa Taasisi ya Fursa kwa Wote nani mmiliki wake? Mheshimiwa Naibu, Newala One nani mmiliki wake, mtuambie hapa? Likombe nani mmiliki wake? Masasi nani mmiliki wake? Lindi Mjini nani mmiliki wake? Nachingwea nani mmiliki wake? Mtama nani mmiliki wake? Aibu tupu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema tunakopa mabilioni ya fedha, wananchi wanaendelea kuwa masikini! Watu wanauza korosho ghafi badala ya kuuza korosho safi, tatizo nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huu mimi naona sasa kwamba ni vyema Serikali ikae makini kwamba kama iliahidi kwamba kuna wakati ambapo watu wale ambao wamepewa viwanda vile kwa bei ya kutupa viwanda vile haviendelezwi vimekuwa ni maghala virejeshwe. Huo ndiyo msingi, ili wananchi wale wapate faida iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya hayo, naomba nimalizie kwa kusema kwamba, tunaendelea na demokrasia ya kweli, nakipongeza Chama changu cha Wananchi CUF, nampongeza Rais halali Maalim Seif Sharrif Hamad wa Zanzibar na Baraza Kuu la Uongozi wa Taifa CUF kwa kutoingia katika uchaguzi,. Tunasema kwamba tuko makini, UKAWA tuko makini na Chama cha Wananchi CUF kiko makini. Ahsante sana. (Makofi)