Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuweza kuongea tena katika Bunge lako la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja zangu zinajikita katika maeneo machache sana kama mawili hivi au matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza kabisa ni juu ya flagship project, makaa ya mawe Mchuchuma na Chuma Liganga. Kwa hiyo, tunapozungumza ni flagship project maana yake ni project ambazo zinatiliwa mkazo kwa kiasi kikubwa ili kuweza kuifanya nchi isonge mbele.
Mheshimiwa Naibu Spika, najikita kwanza kwenye fidia. Mradi hauwezi ukaanza kabla fidia haijalipwa na katika valuation ya ulipaji wa fidia, tunaona ripoti inasema wananchi wale wa Ludewa kwa maana ya Chuma na Liganga wanatakiwa walipwe shilingi bilioni 14. Hapo hapo nikijaribu kuangalia bajeti iliyokuwa imepangwa na Wizara hasa Wizara ya Viwanda inaonyesha ni shilingi bilioni 10.
Sasa nakuja kujiuliza swali la msingi, hii shilingi bilioni nne iko wapi? Kwa sababu katika majibu ya awali ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, pindi nilipokuwa nimeuliza swali tarehe 19 Aprili, tuliambiwa kwamba fidia inalipwa mwezi Juni, mwaka 2016. Kwa sasa tumebakiwa na muda mchache sana kuifikia Juni. Tumebakiwa na kama siku kumi au kumi na moja Juni hiyo ifike.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu tulishawaaminisha Wanaludewa kwamba tunalipa hiyo fidia na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri akasema miradi hiyo itaanza mwezi Machi, 2017, nikiwa namaanisha kwamba fidia hizo zitakuwa tayari zimeshalipwa, lakini bado napata utata mmoja, kwenye strategic plan. Kwa sababu naamini nilivyokuwa nimejibiwa kwamba hizi fidia zitalipwa mwezi Juni na mradi ule unaanza 2017 mwezi Machi, naamini kwamba ningeona kwenye ripoti. Ripoti ingesema kwamba mradi huu unaanza Machi, 2017 ili kutengeneza assurance. Tusipozungumza hivyo, bado mwakani tutakuja na hadithi hizi. Hatutaweza kum-pin Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala langu ni moja tu, tunapozungumzia project, project ina time frame. Kwa hiyo, mwisho wa siku ni lazima utueleze mkakati wako na namna utakavyoanza na maadam umeshatu-assure kwamba mwezi Juni, 2016 unalipa fidia, watu wa Liganga na Mchuchuma na Mradi unaanza mwezi Machi, 2017, kwa hiyo, ipo kwenye plan yako. Hiyo plan inapaswa na sisi tuifahamu. Bila hivyo, nasi inatupa matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili la Mchuchuma, kwa mujibu wa wataalam na Wizara unatarajia kutupa umeme wa megawatt 600, kwa maana ya hii Mchuchuma coal. Kwa hiyo, naamini kuna haja sasa ya kutengeneza nguvu ya kutosha, huu umeme tuufanyie kazi ili uweze kuongeza kwenye pato la nchi, ili twende kwenye uchumi wa viwanda ambao tunautaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachojua, kwenye flagship project kama hii, kuna maeneo mtambuka; kuna suala la VETA. Suala hili la VETA lilizungumzwa sana na hata kipindi hicho Hayati mtangulizi wangu, Marehemu Mheshimiwa Deo Filikunjombe, Mungu amweke mahali pema peponi, alilizungumza kwa kasi, aliliuliza ndani ya Bunge hili la Jamhuri ya Muungano na majibu nakumbuka yalitolewa na Mheshimiwa Mhagama kwamba feasibility study ilishafanyika, michoro ilishakuwa tayari, hati ipo na inatakiwa kuanza kujengwa. Kwa maana ya kuwaandaa vijana kushiriki kwenye mazoezi maalum kwa maana ya kazi na mambo mengineyo ambayo yatakuwepo katika hiyo miradi ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijaribu kuangalia documents zetu ambazo sisi Wabunge tumepewa, hiki Chuo sasa hakipo kabisa. Kwa hiyo, inamaanisha kwamba hatuna maandalizi ya kutosha kwa sababu ile VETA ilivyokuwa imewekwa pale, ilikuwa ni kuwaandaa watu katika kazi za ufundi ili ku-support operations ambazo zinakwenda kufanyika ndani ya miradi hii mikubwa inayokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hii shughuli ni mtambuka na inashirikisha vitu vingi, naiomba Wizara ya Madini, Viwanda na hata na Wizara ya Elimu ambayo inashughulika na mambo ya ufundi, tukae pamoja kuhakikisha kwamba miradi hii wakati inaanza, basi tuanze vile vile maandalizi ya ujenzi wa VETA. Kwa sababu ni kitu cha muhimu na bahati nzuri Bunge lako Tukufu lilishaelezwa kwamba kile chuo kitajengwa. Kama hakitajengwa, lazima tupewe sababu za msingi, zimeyeyukia wapi? Kwa nini hakijengwi? Kwa sababu tulishawaaminisha watu VETA ilishaenda mpaka Shaurimoyo kwa ajili ya kutayarisha eneo; eneo walipata limepimwa hati ipo, michoro ipo na BOQ zote zipo, kwa nini hiki chuo kisijengwe? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo, kwa kweli tunapaswa tulifuatilie na madamu kwa sababu Serikali ilishasema na sababu za kujengwa zilikuwepo, naamini zile sababu hazijakwisha, bado zipo, kwa hiyo, kijengwe ili tuweze kutoa mafunzo kwa wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna suala la Maganga Matitu Resources. Suala hili la Maganga Matitu Resources, hawa wako kwenye partnership na NCD.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.