Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante! Napenda ku-declare interest kwamba, nilishafanya kazi katika ofisi inayohusika na mazingira na najaribu kuangalia uhusiano wa uchimbaji wa madini na mazingira. (Makofi)
Natambua kwamba uchimbaji wa madini au madini yenyewe unajenga uchumi wa nchi yetu na una faida kubwa katika nchi yetu, hilo halina ubishi. Hata hivyo, ni ukweli pia kwamba uchimbaji madini unaharibu mazingira kama usipodhibitiwa na kusimamiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo migodi mikubwa na najua kwamba kabla hawajapata leseni lazima huwa inafanywa tathmini ya athari kwa mazingira ambayo tunaita Environment Impact Assessment (EIA) - tathmini ya athali kwa mazingira na baada ya hapo leseni zinatolewa, baada ya kutoa ile EIA inakuwa kwamba tunasahau kabisa kwamba kuna jambo sasa la kufuatilia kwa karibu ile migodi mikubwa inavyofanya shughuli zake na kuweza kuona jinsi gani wanavyoharibu mazingira kwa namna ya maji yenye sumu, namna ya afya ya wale wafanyakazi na mara nyingi tunakuwa reactive jambo limeshatokea ndiyo tunakwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba leseni zinapotolewa pamoja na kwamba EIA inafanywa na Wizara nyingine, lakini kunakuwa hakuna uhusiano wa karibu sana na sector Ministry. Mapendekezo yangu ni kwamba EIA inavyotolewa na certificate inapotolewa, hizi Wizara ziweze kuzungumza ili kusudi hata wakati wa kwenda kufanya ukaguzi tupate wale wadau wakubwa wote ambao wanahusika na migodi na wale wanaohusika na mambo ya mazingira pamoja na Wilaya zile zenye madini yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesikia Wabunge wengi wakichangia wanasema kwamba, watu wanapata leseni wanakwenda kwenye maeneo yao wao wenyewe wenye Wilaya zao hawana habari. Ina maana kwamba, Serikali inafanya kazi mkono mmoja haujui mfuko mwingine unafanya kitu gani! Kwa hiyo, tunahitaji tuwe na timu ambayo anayetoa leseni, anayefanya EIA na yule mwenye eneo lake ambalo migodi ipo wote wafahamu ni kitu gani kinachoendelea katika lile eneo kwa ajili ya kudhibiti na kuhakikisha mazingira yanakuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika speech ya Mheshimiwa Waziri kwamba kuna maeneo mwaka jana 2015/2016 walitenga heka 7,731 kwa ajili ya wachimbaji wadogo na mwaka 2016/2017 wametenga hekta 12, 000 ni jambo jema. Nashauri kwamba, wachimbaji wadogo nao pia wanaharibu mazingira sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimepita Mererani, nilishapita wakati mwingine sehemu za kule kwenye diamond - Mwadui, wanachimba wanaacha mashimo, ile ardhi inakuwa tupu hakuna miti ni mashimo! Kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa sana kwa ajili ya kudhibiti na kuangalia kwamba mazingira yanarejeshwa katika hali yake ya asili. Najua wachimbaji wadogo wadogo wanakuwa na Environment Management Plans, lakini nani anawasimamia? Hakuna mtu anayewasimamia, wanachimba wanaacha!
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza kwamba Wizara inayohusika ya Nishati na Madini, Wizara inayohusika na Mazingira na yale maeneo ambayo ile migodi inachimbwa, ile midogo midogo, watafute jinsi ya kuya-incentivised wale wachimbaji wadogo kusudi wahakikishe kwamba lile eneo lililochimbwa na kuharibiwa linarudishwa katika hali yake ya asili ya miti na majani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia pia katika taarifa ya Audit ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu alivyozungumzia kuhusu petroleum exploration na pia nimeona kwamba Ofisi ya Rais Mazingira wamefanya inspection tatu tu katika miradi karibu 71 na inaelekea kwamba hakuna uwezo mkubwa sana. Hili ni eneo pia ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri alizungumzie ni jinsi gani inspections ya haya maeneo itaimarishwa ili kuhakikisha kwamba tunachunga mazingira yetu. Napendekeza pia hizi teams ziendelee kufanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee suala la umeme, najua kwamba mimi mwenyewe nilishavuta umeme nikaweka nguzo kama mbili, tatu na tunalipia gharama kubwa na naamini kuna wengi pia wanafanya hivyo na hizo nguzo baadaye ni za TANESCO pamoja na kwamba ni sisi ndiyo tumezilipia pamoja na LUKU tumezilipia.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Mheshimiwa Waziri anapomalizia hoja yake atuambie ni kwa jinsi gani watu ambao wameweka hizo nguzo za umeme kwa gharama zao na hizo nguzo ni za TANESCO ni kwa namna gani wanaweza ku- compensate? Je, inawezekana ku- compensate kwa kupitia bill za umeme kwamba wewe umeweka nguzo tatu, bei ni kadhaa na kwamba labda bill ya umeme uwe unalipa kiasi fulani na ufidie kwa ile miti ya TANESCO ambayo umeweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashukuru Mheshimiwa Waziri akitujibu hilo suala tuweze kujua ni jinsi gani TANESCO wanaweza kutu-compensate.
Mheshimiwa Naibu Spika, watu wengi sana wamezungumzia suala la Nyamongo na mimi nasikitishwa kwamba, nilikuwemo suala la Nyamongo lilikuwepo, nimetoka sasa sijui karibu miaka mingapi suala la Nyamongo bado linaendelea. Mheshimiwa Waziri, hii Nyamongo ina shida gani, kwa nini hii issue haiishi? Maana yake imekuwa ya muda mrefu sana na miaka mingi, pengine labda kuna kitu Waheshimiwa Wabunge hatujui, labda kuna tatizo fulani, tunaomba Mheshimiwa Waziri anapomaliza hoja yake, atueleze kuna shida gani na hili suala la Nyamongo ambalo tumelizungumza miaka nenda miaka rudi!
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii.