Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa kutenga bajeti kubwa ambayo haijawahi kutokea, asilimia alizotenga tuna uhakika kwamba umeme sasa utakuwa umefika sehemu zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba leo mnachozungumzia hapa ni suala la umeme. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda yuko pale bila ya umeme hatofanya chochote, lakini hamuelewi huo umeme mnaozungumza ni umeme gani. Umeme tunaozungumza sasa hivi ni ule ambao unatokana na nguvu za kule Kidatu, Kihansi na ule mwingine unaotoka kwenye bwawa la Mtera, yale maji yanatoka katika Wilaya ya Kilolo. Vyanzo vitano vya maji ambavyo vinajaza Kihansi vinaanza kwenye vyanzo ambavyo vinatoka kwenye Wilaya ya Kilolo, sehemu ya Muhu na Mkasi. Maji yanayojaza bwawa la Mtera yanatoka kwenye vyanzo vikuu ambavyo ni Mto wa Lukosi na Mto Mtitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulishaongea na Mheshimiwa Waziri nikamwomba kwamba ni vema sasa tukaenda kule akatembea aone uhalisia. Kwamba wale wanaopika chakula kizuri wenyewe hawali. Mpaka hivi ninavyomwambia kuna Kata ya Kimala, Idete, Ukwega, Udekwa, Kising‟a, Nyanzwa na Mahenge wanausikia tu umeme kwenye bomba, wakati wakijua kabisa kwamba chanzo kikuu ni Wilaya ya Kilolo. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa alishaniahidi kufika kule, naomba afike ili aangalie ni jinsi gani atanifikiria tuweze kupata umeme vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nishauri tu, kwamba kwa kuwa mwaka wa juzi, mwaka wa jana tulikuwa kwenye kujenga maabara, maabara zile hazitakuwa maabara kama hakutakuwa na umeme, kwa kuwa sasa wananchi wenyewe hali zao si nzuri sana niiombe Serikali, Wizara ya Elimu ikishirikiana na Wizara hii tuweze kuhakikisha kwamba kwenye shule zote za sekondari ambako tumejenga maabara waweze kuingiziwa umeme, hilo atakuwa ametatua na ametusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine na-declare interest, nilikuwa Mkuu wa Wilaya, nikiwa Mkuu wa Wilaya nililetewa kesi hizi zinazohusiana na vinasaba, bahati nzuri nitazungumza yale ambayo ni ya ukweli na Mungu ananiona. Mfanyabiashara yule baada ya kukamatwa alikuja ofisini kwangu, baada ya kuja ofisini kwangu nikaomba watu wa EWURA waje, walipokuja walituelimisha jinsi gani watu wanavyotorosha mafuta. Baadaye alikubali kweli mafuta yale yalikuwa ni ya transit na alikuwa anakwepa kodi.
Baada ya kufanya utafiti ikaonekana kwamba zaidi ya wafanyabiashara 316,000 walikuwa wanakwepa kodi. Wafanyabiashara wa mafuta siyo mchezo ni ma-giant. Kwa hiyo, unaweza ukakuta kelele yote hii ambayo inapigwa hapa ni kwa sababu wale nao wana uwezo wao. Hivi jiulize, kama EWURA wasingeweza kudhibiti mafuta bei hii ambayo ipo sasa hivi ingekuwepo? Tulishafikia mpaka shilingi 3,000 kwa lita, leo tunanunua mpaka Shilingi 1,200 yanashuka, ni kwa sababu ya udhibiti mzuri wa EWURA.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi EWURA wasikatishwe tamaa. Kwa sababu juzi nilisikia hapa kwamba hata tenda za kupata mtu wa kutoa vinasaba hazikutangazwa, kitu ambacho siyo kweli, zilitangazwa kwenye magazeti na kwenye tovuti na ushahidi upo, kwa nini tuseme uwongo? Naomba, badala ya kuwakatisha tamaa tuwape nguvu kitu gani tufanye ili mafuta yadhibitiwe, wananchi wetu bei zikipungua waweze kusafirisha mazao yao, waweze kusafiri, kwa sababu bila kudhibiti hiyo nawahakikishieni mifumuko ya bei haitapungua, itaongezeka. Nawaomba wasikate tamaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza sana watu wa EWURA, endeleeni na kazi hiyo, ongezeeni nguvu. Hawa ambao wanapambana nao wapo wengi wameshawakamata. Mtu anayekamatwa siku zote anakuwa na ugomvi na Polisi, akishaona Polisi anaona huyu mtu hafai. Tumuongezee. Mimi najua watu wameshaambiwa maneno hapa kama alivyosema yule bwana mdogo, siwezi kuwavunja, wana interest zao. Kama mtu ana interest a-declare interest hapa. Mheshimiwa Waziri asikate tamaa, moto ni ule ule, hapa kazi tu, kanyaga twende. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kuhusu viwanda. Kama tunakwenda kwenye viwanda, tumeamua Serikali yetu kuwekeza kwenye viwanda, umeme lazima uwe wa uhakika. Kuna sehemu ambazo tumeweka maeneo kwa ajili ya EPZA, ziangaliwe zile ili Processing Zone zile tuweze ku-process mazao na kuyapa thamani ili kuweza kuuza na kupata bei zinazofaa. Mheshimiwa Waziri wa viwanda apige kelele atakavyoweza, kama umeme hautafika itakuwa haina maana yoyote. Washirikiane vizuri na Waziri wa Kilimo kwa sababu viwanda vyake pia kama hakutakuwa na mageuzi ya kilimo hatafanya chochote! Kama wasambazaji wa pembejeo wataendelea kuwa wababaishaji hatafanya chochote, ubora wake utabakia kwenye vitabu na maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ulanzi unatengenezwa pale Iringa, tunashindwa kwa sababu ya umeme, hebu Mheshimiwa Waziri aje atembelee, wenzetu Kenya wanasema ni bamboo juicy, lakini ndiyo ulanzi huo huo. Ulanzi siku ya kwanza unakuwa ni togwa, togwa ni juicy, siku ya pili unakuwa mkangafu, mkangafu ndiyo unaanza kuwa pombe, siku ya tatu unakuwa mdindifu, mdindifu ndiyo unalewa, yeye alisoma Tosamaganga najua alikuwa anapiga ule! (Kicheko/ Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Mambo ya Ndani alisoma shule ya Tosamaganga na Naibu Waziri wa Maliasili alisoma Tosamaganga na wenyewe wanatoka Tosamaganga, kwa hiyo asiposaidia wakajenga viwanda atakuwa hajafanya kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nafikiri ni kengele yangu ya mwisho au bado?
NAIBU SPIKA: Bado Mheshimiwa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba kwa kweli tufanye hivyo na kuna mambo mengi, kuna sehemu nyingi, kuna viwanda kwa mfano hata kule Busega hawana umeme, wangepata umeme wangeweza pia angalau wakachinja hata wale ng‟ombe badala ya kuleta ng‟ombe Dar es Salaam kwenye malori wangeleta nyama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hawawezi kuleta nyama kama hamna umeme, Eeh! hakuna mabarafu yale zitaoza zile. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie ili tupate umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja!